Jipatie maarifa kutoka vitabu bora vilivyoandikwa na Dr Brighton shoo kuusu imani, sayansi, afya, teknolojia, asili, malezi, saikolojia na mazingira

Siri ya Vitunguu saumu, Tangawizi, & Pilipili kama Dawa

Vitunguu saumu, binzari, tangawizi, na Pilipili kama dawa

 Je ni kweli Mbogamboga zinaongeza uwezo wa Tiba ya Mwili?

Ni kweli kabisa ukiachana na kinga ya mwili, Mimea ni Tiba kubwa sana ambayo huwawezesha wala mbogamboga na matunda kutoumwa sana. Kumbuka kuwa, Viumbe wengi wala mimea huila tokea chini katika ardhi, kwenye uchafu mwingi. Ng’ombe huweza kula Mimea iliyochanganyika na kinyesi na mikojo yake, na ndivyo ilivyo kinyume kwa viumbe wala nyama. Wala nyama wengi huwa wasafi sana, mfano mzuri ni Simba, Chui, na hata Binadamu. Tabia hii ya Usafi sio Bahati mbaya, wala haimaanishi ni maendeleo ya Ubongo, Maana Tembo ana akili kuliko simba lakini ni Mchafu kuliko Paka.

Mimea huwezesha tiba kwa kuwa kiini cha magonjwa ni kuathiriwa kwa mfumo wa balansi ya vimelea, hasa bakteria. Mimea ina uhusiano mkubwa sana na vimelea hawa maana huwatumia sana katika ukuaji wake. Mimea huwapa chakula vimelea wote, lakini pia huwa na kemikali za kuwapunguza ukuaji wake wanapomaliza kuila. Mimea kupitia kambakamba ‘’fibers’’ hutengeneza mazingira ya uvundo ambayo bakteria wengi na vimelea hupendelea, hii ni kama huwavuta vimelea wote kuachana na sehemu zingine na kurudi kwenye utumbo. Na kitendo cha hizi ‘’fibers’’ kusaidia kiumbe kujisaidia kwa ufanisi kila wakati, huwezesha kuzuia viumbe kukaa kwa muda mrefu tumboni bila kuwa na mzunguko wa kukua na kutolewa, na ndiyo maana si vema siku kupita bila Kwenda haja.

Viumbe wala nyama huwa na asidi kali sana mwanzoni tu mwa tumbo, hii ni kwa kuwa huwa hawawezi kuchakata kambakamba, au wanga za mimea, hivyo kiwango cha bakteria kidogo tu huweza kuwafanya waanze kuumwa. Ukiwa daktari mtafiti sana utagundua magonjwa mengi sana hufanana kati ya binadamu, na Wanyama wala nyama kama Paka, na mbwa, kuliko ilivyo kati ya binadamu na Wanyama wala mimea kama mbuzi na kondoo. Wanyama wengi wala nyama kama Mbwa, pia hutumia sana mimea wanapohisi kuumwa, na sababu nitaielezea vizuri mbeleni kidogo, lakini tujiulize maswal yafuatayo;

Kwanini Mimea mingi kama Tangawizi, na Binzari ni Dawa?

Ukielewa sana lugha ya mimea kama kitabu hiki kinavyolenga, unaweza gundua kuwa Mimea kama Tangawizi na jamii za binzari ni mimea ambayo imewekeza zaidi uhai wake katika mizizi, na ni mimea ambayo ina uwezo mkubwa sana wa kudumu katika Joto, vivuli, na unyevu. Nilipokuwa mdogo, Mama yangu aliwahi nambia walipokuwa wakilima Tangawizi, hata ukame na Mioto ya pori kuandaa mashamba inapopita, Tangawizi hubakia imara chini ya ardhi. Hata Leo hii inafahamika kuwa Chai ya Mdalasini ‘’cinnamon’’, na Tangawizi ‘’ginger’’ ni dawa bora kabisa za Homa ‘’Cold flu’’. 

Sababu ni kuwa; Mimea hii kutokana na kuwa hupambana sana katika mazingira ya chini, mwanga kidogo, unyevu mkubwa ambao huhamasisha sana kuoza kwa uvundo na bakteria, huwa na mbinu yake ya kuwa na kiwango kikubwa sana cha ‘’Antioxidants, Anti-inflammatory, na Caretonoids’, mfano ‘’Curcumin inayoifanya Binzari kuwa ya njano, au ‘’6-dehydrogingerdione’’ iliyo kwenye tangawizi. Hizi huzifanya kufyonza mwanga wa jua japo unafika kidogo chini, lakini kwa ufanisi mkubwa sana. Pia huwa ngumu zenye nishati kubwa ya joto hata kama kutakuwa na maji maji ya unyevu kwa mvua nzito, na huwa na ukali unaotokana na ‘’Curcuminoids, au phenolic acids’’ kuwafanya bakteria kushindwa kabisa kuiathiri, au kuifanya ivimbe ikalainika.

Unapokula Tangawizi, au Binzari, huwa zinahisi wewe ni hatari, au huwa unakula kemikali zake za ulinzi za kupambana na vimelea, na hivyo kiwango kikubwa ambacho huingia mwilini mwako huwaathiri bakteria na vimelea wote ambao wangeweza kukuletea shida. Kiwango chake kikubwa cha kemikali za kujipambania ‘’anti-inflammatories’’ pia hukusaidia kuondoa msisimko mkubwa wa uvimbe, ambao huwa ndiyo gia ya kwanza ya bakteria kukushambulia kwa kuzalisha sumu zao. Unjano wake ambao ni Ishara ya ‘’caretonoids’’ husaidia kupata Vitamin A ambayo husaidia sana kuponesha michubuko katika kuta za mwili.

Matumizi ya Binzari huwa na matokeo mazuri sana inapochanganywa na pilipili ‘’Black pepper’’, au mafuta ya Wanyama ili iweze kufyonzwa na mwili. Na husaidia sana kwa shida za maumivu, au uvimbe wa viungo ‘’Arthritis’’, na hii ni kwa kuwa; huchochea sana joto la mwili kuongeza spidi ya damu, ambayo husukuma chembechembe za kuzuia uvimbe ‘’anti-inflammatories’’ kama Curcumin katika joint ambazo huwa na maumivu. Tangawizi nayo huchochea joto la mwili, na huwa na matokeo mazuri zaidi inapokuwa na mdalasini, tofauti na binzari, hii huwa na spidi sana na hupenyesha kirahisi sana kemikali zake kama ‘’Gingerols’’ ambazo hupasha mwili, hii huwa tiba nzuri sana kwa shida za mafua, huchochea kutembea kwa chakula tumboni, na husaidia mapafu kuondoa msongamano wa makohozi, au shida za asthma.

Unajifunza nini kuhusu Joto, na Tiba ya Vitunguu saumu?

Vitunguu saumu japo kwa asili hushamiri sana katika maeneo ya kanda za baridi sana, Maeneo ya Asia ya kati’, Lakini huwa na sifa za kuchochea sana Joto la mwili kama wenzake tangawizi, na binzari. Vitunguu saumu ‘’Garlic’’ sifa yake ya upekee sana ni uwezo wake mkubwa sana wa Kusaidia kwa shida za moyo, kwa kushusha sana kiwango cha ‘’Cholesterol-LDL’’, lakini pia ni Maarufu sana kwa uwezo wake wa Kuua vimelea ‘’Anti-microbial’’, huua Bakteria, Virusi, mpaka fangasi. 

Kitunguu saumu siri yake ya matibabu ni kiwango chake kikubwa cha madini ya ‘’Sulfur’’ kama nilivyoyaelezea awali. Huwa nayo mengi sana kupitia kemikali yake inayoitwa ‘’Allicin’’, haya huwa kama sabuni kwenye Damu ‘’detergents’’, yaani huzifanya seli zote kuchangamka kutojikusanya Pamoja, hasa seli za kuganda za damu ‘’Platelets’’ ambazo hupooza sana damu, husisimua sana seli nyeupe za damu, na Cholesterol huifanya kuwa ‘’sulphated’’ hivyo husaidia sana Moyo, hii ndiyo sababu nilianza na kuelezea Namna Mimea husaidia kinga za viumbe.

Maajabu haya ya Vitunguu saumu yanatokana pia na asili ya maeneo yake ambayo huweza kufikia hata baridi kali kabisa ya nyuzi hasi ‘’-17 celcius’’, hivyo Hii mimea huwa na uwezo wa kuzuia kuganda kwa chembechembe zake, au kusimama kwa metabolikia zake, na unapoitumia, unahamasisha pia Metabolikia yako ambayo huwa ikizidiwa sana unapokuwa ukiumwa. Vitunguu saumu huwa na madini mengi, Pamoja na protini na wanga ambazo unapokaanga huunda ‘’melanoids’’ zinazoifanya kuonekana ya ‘’kahawia, au njano’’ kupitia matendo yanayoitwa ‘’mailard reactions. Unaweza ongeza ufanisi wake pia kwa kuichanganya na Binzari, zamani ilikuwa ikitumika kama Dawa kuu, kwa kuwa huwezesha kinga ya mwili, lakini pia allicin huvimaliza nguvu vimelea.

Je, Kuna Uhusiano wa Joto la Homa, Joto la Vitunguu saumu, Tangawizi, au Pilipili?

Kitabu hiki kitawafungua Wataalamu wa Tiba za Mimea, na asili, kutofananishwa na Waganga wa kienyeji ambao hutibu bila kujua wamewezaje kutibu. Mwili unapokuwa katika homa, tokea katika Ubongo katika ‘’Hypothalamus’’ sehemu inayoratibu metabolikia za mwili ikishirikiana na Ini, hutengeneza hisia ya baridi kali, ijapokuwa mwili huwa na joto kali. Mwili hutengeneza hisia za baridi ili mtu akatafute joto zaidi kuuongezea mwili uwezo wa kupambana na mashambulizi dhidi ya vimelea, au virusi, au hali tatanishi. Kinachomuua mtu katika homa ni kutoweza kufikia Joto ambalo mwili hulihitaji kufanya metabolikia iwe imara, bila kuharibu kabisa mfumo mzima wa fiziolojia ya mwili. 

Mtu anapotumia Pilipili, au tangawizi, hasa na Mdalasini, katika namna ya Chai, kama pilipili ambavyo husisimua sensa za joto ‘’TRPV1’’ na kuufanya mwili kupata joto, ndivyo ilivyo kwa tangawizi, mdalasini, au binzari, ambazo huwa na ufanisi sana wa kuongeza joto kama tulivoona na kusaidia sana mwili kupandisha metabolikia yake, na kuipunguza nguvu homa. ‘’vitunguu saumu huwa bora zaidi kwa shida za tumbo, na moyo pia’’. 

Mimea hii ilisaidia Mabilioni ya watu enzi za Mlipuko wa virusi vya COVID-19, tofauti kabisa na Ibuprofen na NSAIDs zingine, ambazo hukinzana na Ubongo katika mapambano yake dhidi ya hali tata, kwa kuishusha joto lake, kwa kuathiri chembechembe za ‘’Prostaglandins’’, na kuathiri kabisa kemia ya maji mwilini. Mimea hii huufuata mwili hukohuko katika upambanaji wake kwa kupandisha metabolikia ya mwili, kutoa kemikali zinazowamaliza nguvu vimelea, kuuponyesha mwili, na pia kuupatia virutubisho.

Mtazamo huu hufanya niamini kuwa Pilipili haipo kwa ajili ya ndege, ipo kwa ajili ya Wanyama wasife kwa homa ili kesho wasambaze zaidi mbegu zake. Katika Ikolojia, hakuna kiumbe kinataka ufe, hata bakteria wanataka uendelee kuishi ili uendelee kuwapa chakula. unakufa tu kwa kuwa umeshindwa kujimudu. Hii ni kama ambavyo watu hupenda kuchuma mboga wasing’oe kabisa mizizi ili kesho wairudie. Kama Simba angekukula leo na kesho akakuona tena, atakupenda zaidi sawa kabisa na Wanasiasa wanaopenda uendelee kuishi ili waendelee kula kodi yako.