KWANINI MINAZI BAHARINI & TENDE JANGWANI?
Kwanini Minazi ni Mirefu, ina tabaka gumu kwa nje, na huota kando ya Bahari?
Minazi huwa na majani imara sana, mizizi imara sana, huchelewa sana kukua, hutumia miaka 10 mpaka kukomaa kuanza kuzaa. Huwa mirefu ili kupata mwanga mwingi zaidi wa jua, lakini pia hulenga kutofunikwa na kina cha maji ya Bahari. Majani yake huwa marefu laini, yenye kambakamba ‘’fibers’’ nyingi na ngumu ili kutoshambuliwa na wadudu na kupoteza maji kirahisi. Kwa kuwa pwani hakuna virutubisho sana, na kuna chumvi nyingi, nazi hutumia zaidi mafuta kama namna yake ya kupata nishati kuliko kuegemea sukari.
Minazi huangusha Watoto wake baharini, kiwango kikubwa cha maji ya chumvi hulainisha tabaka lake la nje, na mtoto wake kwa ndani huanza kutanuka kadri ugumu wa koti lake unavyolegea. Ipo siri kubwa sana hapa, kadri Mmea unapowekeza zaidi kwa mbegu, au Watoto wake, hutumia mafuta zaidi ya sukari. Na hii ndiyo sababu, Wanyama hutumia sana mafuta kama chanzo chao kikuu cha nishati, na sio sukari. Watoto wa binadamu huzaliwa na vitumbo vya mafuta, maziwa ya Wanyama hujaa mafuta sio sukari. Na ndivyo hivyohivyo ilivyo kwa nazi, mawese ya michikichi, maparachichi, n.k. yote huwa na mafuta sana, tofauti na Mgomba ambao huishi miezi 6 tu mpaka 12, na huzalisha ndizi zenye sukari nyingi sana.
Kwanini Tende huota jangwani?
Tende na matunda mengi sana ambayo hushamiri sana kwenye ukame, huwa na sukari nyingi sana. Mimea hii hutunza sukari, hasa aina ya ‘’Sucrose, au fructose’’, kwa kuwa sukari huwa na tabia ya kufyonza sana maji. Kitendo hiki huisaidia sana kuweza kudumu katika kipindi cha ukame jangwani. Kwa tende kuwa na sukari nyingi, hujipatia nishati nyingi sana kwa kuivunja sukari yake iliyofyonza maji kipindi ambacho huwa hakuna maji ya kutosha ya kuwezesha ‘’Photosynthesis’’. Ukiangalia mtende na majani yake, utagundua ipo katika mkakati wa kuzuia kupoteza maji kama yalivyo majani ya mnazi. Majani haya hufungua kidogo tu matundu yake kupoteza maji mchana, huwa na namna ya kuzuia maji yake yasipotee kwa kuwa na mithili ya utandu laini kuzunguka matundu yake kuzuia maji yasipotee sana.
Maji ni kila kitu kwa viumbe. Wanyama asilimia 70% ni maji, au asilimia 90% ya molekuli zao ni maji, huku asilimia iliyobakia 50% ni mafuta, na 50% ni protini. Mimea mingine kama jamii ya ‘’Cactus’’ ambayo hushamiri sana jangwani, yenyewe mchana huwa haifungui kabisa matundu yake ‘’stomata’’, huwa ukiyafungua tu jioni ili kufyonza mvuke. Ngamia hudumu jangwani kwa kuwa huwa na Nundu la mafuta ambalo huvunjika kuzalisha maji, sio sukari. Gramu 10 za mafuta hutoa gramu 10 za maji, huku gramu 10 za wanga zikitoa gramu 6 tu za maji. Mimea nayo ya jangwani hutumia sukari kwa kutunza maji, kwa kuwa kwao sukari huwa na faida zaidi kwa kuwa jangwani huwa kuna jua kali sana, hivyo sukari huwa na faida mbili ya kutunza maji na kutunza nishati.
Jiulize swali, mimea inapambana ili kuishi jangwani kwa kutumia mwanga, maji, na sukari. Ngamia anapambana jangwani kwa kutumia mafuta, mwanga, na maji. Binadamu anapambana kwa kutumia nini?




Join the conversation