Jipatie maarifa kutoka vitabu bora vilivyoandikwa na Dr Brighton shoo kuusu imani, sayansi, afya, teknolojia, asili, malezi, saikolojia na mazingira

Je unaweza kuishi kwa kula Wanyama tu?

Je unaweza kuishi Kwa kula Nyama tu?

Je unaweza kuishi kwa kutokula kabisa Mimea, au kula Wanyama tu?

Bado vipo visa vingi sana na tafiti kadhaa zinazoonyesha kuwa zipo jamii za watu, au watu ambao wamekuwa wakiishi kwa kula Nyama, maziwa, au damu kidogo tu, bila kabisa kutumia Mimea. lakini hata hivyo, bado uhalisia wa visa hivi ni mdogo sana. Na hii ni kwa kuwa; bado wengi huwa tayari ni watu ambao walishawahi kuwa walaji wa mimea, au wamekuwa walaji sana wa bidhaa za nyama kutokana na shida kadhaa za magonjwa au changamoto za kiafya, au ili kupunguza uzito. Kumbuka Mwili wa binadamu una badilika sana kulingana na mazingira yake, na ndiyo maana wapo wanaoweza kuishi kwa kula Mimea tu, au Wanyama tu. 

Lakini katika mtazamo wa kina wa afya, hata Utafiti mkubwa kabisa wa Dr Price, aliyezunguka Dunia nzima, na mtaalamu wa kwanza kugundua jamii zilizoacha kula vyakula vya asili yao, na kula sana mazao ya kigeni viliathiriwa sana. Akionesha kana kama Wamaasai waliokuwa wakila zaidi nyama tu, maziwa, na damu kidogo wakiwa bora sana kiafya ukilinganisha na Wakikuyu wa Kenya, ambao walikula sana Viazi vitamu, magimbi, ndizi, mtama, mahindi, uwele, maharagwe, mbaazi, kamande, miwa, asali, na mbogamboga kidogo za majani za pori, bado utafiti wake una ukweli Nusu. Bado zingeweza kutafsiriwa kama jamii zilizo nje zaidi katika mwanga, shughuli nyingi za misuli, na usasa kidogo sana, kuwa ndizo zilikuwa na afya zaidi. 

Tamaduni za Wamaasai pia ni ngumu sana kuweza kupima mwenendo wa afya zao kutokana na kuhamahama kwao, Wamaasai pia wana akili sana za matibabu ya asili, tena hasa ya Wanyama ‘’Veterinary medicine’’, na hata kwa binadamu huweza kuunganisha mifupa kiasilia, ni wajasiri sana wanaweza kukimbiza hata simba katika umri mdogo. Wamaasai walishakuwa wakifanya biashara na makabila kama Wabarbaig, biashara za mazao tokea zamani. Bado watafiti wengi hukosa baadhi ya doti za muhimu sana za kutofautisha mfumo wa ulaji, kiasi na aina ya vyakula, mazingira, na tabia za jamii husika ‘’anthropolojia’’.

Ulaji wa Wanyama, au bidhaa za Wanyama tu una hatari kubwa sana pia, ijapokuwa sio kama vitabu vya afya vinavyofundisha watu, kuwa ni shida ya lehemu mbaya ‘’LDL-cholesterol’’, huo ni mtazamo wa kale uliopitwa na wakati, kuwa kiwango kikubwa cha mafuta ya Wanyama ‘’saturated fats’’ huusiana na shida za moyo. Ulaji wa nyama peke yake huambatana na hatari kubwa sana ya kupungukiwa madini ‘’electrolytes’’ mwilini, jambo ambalo linaweza ufanya mwili kuwa dhaifu sana, kupungukiwa ‘’antioxidants’’ kama Vitamin C, na hii inaweza harakisha kuzeeka. Ukosefu wa kambakamba ‘’fibers’’ ijapokuwa wengine hupuuzia madhara yake, lakini kuna Ushahidi mkubwa wa upungufu wa kambakamba na afya dhoofu ya vimelea wa tumboni, ambao husaidia sana kuzalisha mafuta mazuri ‘’SCFAs’’ kama ‘’propionate, butyrate, na acetate’’, na huzalisha maelfu ya kemikali muhimu kama tulivyoona ‘’sulfur, serotonin, dopa, n.k.’’

Ijapokuwa wala nyama tu huwa na matokeo ya ukuaji mkubwa wa misuli, mifumo imara ya homoni, na mifupa, lakini faida hizi zote huelekea zaidi katika ufanisi tu wa hata umri wa kuweza kuzaa, baada ya hapo, Ni mimea tu ndiyo huweza kukuwezesha kufika safari ndefu zaidi ya uhai. Na Bahati mbaya zaidi ni kuwa, Urefu wa uhai hauna uhusiano mkubwa sana na ukubwa wa umbile la mwili, ijapokuwa inafahamika kuwa watu wenye misuli na mifupa yenye nguvu huishi miaka mingi zaidi kwa kuweza kubeba miili yao, kutoanguka, na kuweza kubalansi vizuri kiwango cha sukari katika damu. Lakini hayo hayahusiani na ukubwa wa umbile la mwili, yanahusiana na wastani wa mwili wa mtu, na nguvu zake za misuli na mifupa. Ni rahisi kuhisi Mguu wa Nyumbu una nguvu kuliko mguu wa simba kwa kuangalia umbile, lakini kuna tofauti katika umbile na nguvu. 

Sokwe wana misuli mikubwa zaidi ya binadamu lakini huishi miaka nusu tu ya binadamu, na sababu kubwa ni kuwa; chembechembe zinazoufanya mwili uwe imara na wenye nguvu ni ‘’Mitochondria’’, na hizi kwa binadamu zimejaa zaidi katika Ubongo na Moyo, sio misuli ya mapaja, mikono, na makalio. Na ndivyo ilivyo watu wengi wanakufa sana kwa shida za moyo na Ubongo, sio misuli. hii inaweza kukueleza kwanini watu wengi wanaoishi miaka mingi sana duniani si watu wenye miili mikubwa sana, mfano tazama Wajapani, au Tazama Wapare, na wachagga, kwa Tanzania.

Wala nyama tu baadhi hujikita kukataa kula mimea kwa kusema wanajiepusha dhidi ya madhara ya kemikali sumu za mimea ‘’anti nutrients’’ kama lectins, phytates, oxalates, n.k. Mtazamo huu ni matokeo ya Imani zaidi ya uhalisia, kiwango cha hizi kemikali cha kuweza kuleta madhara huwa ni ngumu sana kuweza kukifikia. Ajabu zaidi ni kuwa, kemikali sumu kidogo mwilini huwa na faida sana, na huu ni mtazamo wa biolojia ya kina sana, ni kama awali nilipoelezea umuhimu wa ‘’Reactive oxygen species’’, hivyohivyo na hizi kemikali husaidia sana kuratibu utendaji wa mifumo ya kupambana na kemikali sumu, mfano; Glutathione husisimuliwa pia na chaneli za Nf-Kb, au NRF2, ambapo hizi chaneli zote huitaji uwepo wa kemikali sumu kidogo mwilini. Mwili huwa imara sana unapopata kemikali sumu kidogo kutoka katika mimea ili kusisimua mfumo wa kinga, na metabolikia za kwenye ini. Ulaji wa nyama tu huathiri sana Vimelea wanaotegemea wanga tu mwilini, ijapokuwa husaidia sana kutatua shida za uvimbe tumboni kama ‘’Crohn’s diseases’’, na hapo ndipo huwa nasisitiza, ulaji uwe kwa mkakati wa kusaidia mwili kulingana na hali yake, sio Imani zisizo na uhalisia.

To be continued....

Unaweza jifunza zaidi kupitia kusoma kitabu changu Cha "Vita za Vyakula '