Je unaweza kuishi kwa kula Mimea tu?
Je unaweza kuishi kwa kula Mimea tu?
Inawezekana na watu wengi zaidi huishi kwa kula Mimea asilimia kubwa zaidi, au mimea tu. Swali gumu zaidi ni kuwa, je inawezekana kuishi kwa kula mimea tu na kuwa na afya njema kabisa? Bahati mbaya kila binadamu huanza kwa kunywa maziwa ya Wanyama, aidha mwanamke, au mtamba wa ng’ombe mpaka Miezi 9, au mpaka Miaka 2 kama nilivyonyonya, au inavyopaswa, au shauriwa.
Hivyo awali kabisa lazima uanze na Wanyama, ukianza na Mimea utakufa. Idadi ya watu wanaokula mbogamboga na matunda na kuhamasisha sana ulaji wa Mimea tu ‘’strict vegeterianism’’, wengi wao awali walikuwa ni walaji sana wa nyama, jambo ambalo kisayansi zaidi huwafanya kuonekana hawaelewi sayansi ya muda na ulaji.
Ulaji wa nyama na bidhaa za Wanyama huwa na faida zaidi katika umri wa utoto mpaka umri wa kuweza kuzaa, baada ya hapo huongeza zaidi hatari kwa kuchochea seli dhaifu ‘’senescent cells’’ kwa kiwango kikubwa cha madini chuma ‘’ferroptosis’’, na shida za uchujaji wa kemikali za Nitrogeni katika figo. Hivyo watu hawa huwa walishanufaika sana na bidhaa za Wanyama, na unapofika wakati kwao sahihi ambao hawazihitaji zaidi na kuhitaji zaidi Mimea, huwatangazia wengine kuwa Mimea ni sahihi zaidi kwa kujiweka wao kama mfano, kufundisha wanaopaswa kuanza mwanzo. Hili huwafanya kutokuwa kielelezo kizuri cha Maarifa.
Unaweza kuishi kwa kula Mimea tu na kuwa na afya, lakini kwa masharti yafuatayo;
Kwanza kuwa na Maarifa makubwa sana ya kujua Mimea ili iweze kukuwezesha unapaswa kutumia jamii mbalimbali, zaidi ya 70-90 kwa mwaka, au 20-30 kwa wiki. Bahati mbaya jamii nyingi huwa na aina chache sana za mimea wanayokula, mfano mzuri Ifakara, Morogoro nilipokulia, na sehemu kubwa ya Tanzania, Watu hula zaidi ‘’Mchicha, chainizi, matembele, kisamvu, kabichi, mlenda pori, mwidu, mnafu, majani ya maboga, Sukuma wiki, figiri, spinachi, delega, maharagwe, njegele, broccoli, njugu mawe, choroko, kunde miti au mbaazi, kunde za kutambaa, nyanya maji, nyanya chungu, bilinganya, bamia, pilipili hoho, vitunguu maji, na karoti’’.
huu ni wastani ambao kwanza wengi huwa hawaufikii hata Nusu kutokana na Uchumi, na upatikanaji wake, na Kibaya zaidi hizi mboga 27, hata ukiongeza na jamii zingine zilizopo mahali na mahali zikafika 37, watu bado huzila na wanga kuu tatu, yaani; mahindi, mchele, au ngano. Sehemu kadhaa utapata walahu Mihogo, viazi vitamu, viazi mviringo, mtama, au uwele. ukajumlisha na Matunda ambayo mengi huwa ya msimu, bado wengi huwa hawafikia hata Robo ya kiasi cha Mimea ambayo wangepaswa kula kwa mwaka mzima. Hii ni sawa na kusema, Ukiachana na sera za hamasa, kwa hali ya mtu wa chini kuishi kwa kula Mimea tu, Bado Maarifa ya kujua ninakula chakula Fulani kwa sababu Fulani, hakuna. wengi huishia tu shida za ajabu ajabu kwa kula vyakula aina 20 tu kwa mzunguko wa mwaka mzima.
Mla mimea ‘’typical vegan’’ huwa na aina za nafaka ‘’cereals’’ si chini ya 7 zisizojirudia kwa wiki, mfano ‘’millet, sorghum, barley, rye, rice, corns, na oats’’, katika nyakati kadhaa hutengeneza unga wa kundekunde ‘’legumes’’, kama njugu, soya, maharagwe, njegele, n.k. Hutumia Mbogamboga nyingi na protini katika milo yake, kinyume na utaratibu wa Kiafrika ambapo Sahani hujaa Wanga, na mboga huwa kidogo sana. Hutumia matunda mengi sana, Mimea ‘herbs’’ mingi ambayo huwa katika mfumo wa chai, huwa wana mapishi aina mbalimbali, anaweza tengeneza keki za ndizi, mihogo, katika sehemu hii ninashindwa kueleza mimea mingi ambayo huwa wakiitumia, kwa kuwa mingi haifahamika katika jamii yangu.
Pili kuwa vizuri kiuchumi. Mtu wa hali ya kawaida ana uwezo wa kula Samaki wa 5,000TZS, au akala Robo kilo tu ya Ini kwa 2,500TZS, na akawa amepata aina zote za protini ‘’amino acids’’, madini ya ‘’Copper, zinc, na Chuma’’ ya kumsaidia sana, Vitamini zote ikiwemo Vitamin B-12, Vitamin K-2, na hata kiwango cha kutosha cha Omega-3, vitu ambavyo kama ingelikuwa ni kupitia ulaji wa Mimea, ingelimpasa mtu kutumia ‘’Supplements za B-12, au Cobalamine’’ jambo ambalo kwa supplement ya Kopo moja tu si chini ya 30,000TZS, mpaka 95,000TZS. Ili uweze kula mbogamboga aina mbalimbali hupaswa kutafuta supplements ambazo kwa moja ninayoifahamu, inayoitwa ‘’Veggie-veggie’’ huuzwa si chini ya 80,000TZS. Kwa kula Mimea tu huwa kuna uhitaji sana wa Supplements za madini kama ya ‘’Magnesium, Calcium, n.k.’’, haya nayo huuzwa kwa mfano ‘’Magnesium glycinate’’ mpaka 160,000TZS.
Mfano tazama chini:
Multivitamins:
Standard Vegan Multivitamin (60 tabs): ~Tsh 60,000 – Tsh 75,000.
High Strength/Large Supply (180–360 tabs): ~Tsh 100,000 – Tsh 200,000.
Premium/Comprehensive Blends: ~Tsh 118,000 – Tsh 330,000+.
Targeted Vitamins:
Vegan Vitamin D3 (60 caps): ~Tsh 90,000 – Tsh 97,000.
Vegan Omega-3 (Algae Oil): ~Tsh 90,000 – Tsh 150,000.
Minerals & Blends:
Magnesium: ~Tsh 50,000 – Tsh 90,000.
Super Green Blends: ~Tsh 50,000 – Tsh 70,000.
Watu huisi ulaji wa nyama huambatana na Ulafi, badala ya ulaji sana wa Wanga hupelekea watu wanapokutana na nyama kuwa na ulafi sana, ambapo kisayansi huwa sio ulafi, huwa ni uhitaji sana wa madini na virutubisho vinavyotokana na kula mimea michache sana, hasa Michele, au mahindi yaliyokobolewa, na maharagwe au mboga zilezile kila kukicha.
Nilipokuwa mdogo katika jamii yangu, Watoto wengi kwa kutoka katika familia za hali ngumu, tuliishi kwa wali na ugali maharagwe zaidi, na mboga za majani aina chache, wengi tulikula nyama mara mojamoja sana kutokana na uchache wa Wanyama, gharama za kukidhi kuila maranyingi, lakini tulikula sana Samaki msimu wa masika kutokana na mito mingi. Niligundua Watoto wengi walipokuwa wakienda katika masherehe walikuwa wakiparamia sana nyama, sababu ni huu upungufu. Na hii ndiyo sababu Ng’ombe ambao hupimwa na kutupwa kwa kuumwa Kimeta ‘’Anthrax’’, bado kuna watu huenda kuwafukua na kuwala. Jamii nyingi za masikini wakisikia sherehe huwaza nyama, haya ni matokeo ya Umasikini unaowafanya kula zaidi vyakula visivyo na virutubisho, hivyo huhaha wanapoona nyama au mayai, wala sio roho ya ushetani ya kukemewa.
Tatu, uwe na uwezo wa kupata vyakula vya asili zaidi, visivyokobolewa, Kupata nishati unashauriwa zaidi kutumia hasa jamii ya vyakula kama mtama, ngano nyekundu ‘’rye’’, uweze kupata jamii nyingi sana za matunda, mbogamboga, asali, supplements nyingi sana, na uwe na kiasi sana katika kula kwako kuepuka uraibu. Wapo ‘’vegans’ wanaoweza kuishi kwa kula mimea tu hata kufikia umri wa kuzaa, na kuishi miaka mingi. Lakini ni vigumu sana kwa watu kuweza kuishi mtindo huu bila kuwa na msukumo wa ndani wa kujizuia wenye misingi ya Imani, jambo ambalo binafsi huwa naona lina umuhimu pia kwa kuwa maisha sio kuishi tu, ni kuhisi maana ya maisha yako.
Mama mmoja mnyenyekevu wa kisabato aliyeishi sana Marekani alikuwa akinilalamikia kuwa amezunguka sana Afrika, na amegundua Waafrika tofauti na wazungu hawawezi kujizuia kwenye nyama, na wanakula sana nyama hata kama ni Wasabato. Niliona uchungu aliokuwa akiupitia alipoona uasi huo mbele ya macho yake, lakini binafsi sikuona shida kabisa. Waafrika ni Wawindaji hata leo, ndiyo maana hakuna wakimbiaji zaidi ya Wakenya katika ‘’Olympic’’. Afrika haina mbogamboga za kutosha, zote ni ngeni, tena mpaka zipandwe kwa gharama na maarifa makubwa, wengi huishia kula vyakula dhaifu Kabisa kiafya. Wazungu chungu mzima wamejaa Afrika kushangaa vyakula vya Waafrika eti ni vivutio vyao ‘’maana wao ndo watalii’’. Na tena hata huwafukuza Wamaasai kwenye makazi yao ‘’Ngorongoro-Serengeti’’. Kila sehemu Tanzania kuna Mbuga, hata Baba yangu alikwisha zaliwa kipindi ambacho hakukuwa na Mbuga, Wanyama walisambaa kila sehemu na watu waliwala sana.
Serikali za Afrika miaka ya juzi tu 1950-60’s ndipo zilitenga mbuga na hifadhi kufukuza watu, na kuanza kuwalazimisha watu walime mashamba ya wakoloni, ya Kahawa, Mahindi, n.k. Kiufupi huwezi badili Biolojia ndani ya siku, hata kama sote tunaamini Ulimwengu una miaka 6000 badala ya bilioni 13.8.




Join the conversation