Jipatie maarifa kutoka vitabu bora vilivyoandikwa na Dr Brighton shoo kuusu imani, sayansi, afya, teknolojia, asili, malezi, saikolojia na mazingira

SAYANSI & SIKU YA 5-6 YA UUMBAJI

SAYANSI & SIKU YA 5-6 YA UUMBAJI

SIKU YA TANO 05

20. Uumbaji Wa Wanyama Na Viumbe Wote Hai Mwanzo 1:20-31 

Nguvu Ya Fizikia Dhidi Ya Biolojia

Miongoni mwa vitu vigumu Zaidi kuweza kuvielezea ni sayansi ya Maisha. Maisha yamejaa maarifa ya kila aina, kuanzia Maarifa yanayoweza onekana hata yasioyoonekana. Sayansi ya Biolojia ni mara chache sana kuikuta ikitumia kanuni kama kanuni za hisabati, hii inatokana na kuwa, tofauti na masomo ya sayansi za fizikia, miamba, na anga, ambazo zimejikita katika kusoma tabia za matter, na nishati zisizo na akili, ambazo zinatabirika, na tabia zake ungeweza zielezea kupitia kanuni moja. Mfano tabia ya jiwe linalorushwa, lngeweza elezewa kabisa kwa kutumia milinganyo ya Isaac newton, hata ikafahamika jiwe hilo litatua wapi, litatua na spidi gani, litakaa hewani kwa muda gani n.k. lakini haya yote hayawezekani kuyatambua kwa ndege anayeruka! ambaye hatambuliki ataamua nini kila baada ya sekunde chache, ndege huwezi muandikia mlinganyo. Sayansi ya biolojia imejawa na staajabu kubwa za maarifa makubwa Zaidi yaliyo jificha katika asili.

Kwa miaka mingi sana wanafizikia wamekuwa wakisukuma sana gurudumu la kuwezekana kwa kutokuwepo kwa Mungu. 


hasa kutokana na maendeleo makubwa ya kiinjinia yanayotokana na nadharia zao, na uwekezaji mkubwa wa serikali na matajiri wengi katika fizikia. Na hii ilichangiwa sana na mapinduzi ya viwanda, na migogoro ya kivita. fizikia ilipata heshima sana hasa kutokana na aina yake ya utatuzi wa migogoro, ambayo haihusishi amani na upendo, bali uharibifu na hofu. ambao ni msingi mzuri Zaidi wa kiutawala. Fizikia ilikuwa ni sayansi iliyoanza na nguvu sana katika karne za kumi na saba. Ikija na mapinduzi ya matumizi ya uhuru wa kifikra. Lakini baada ya miaka kadhaa ya mapinduzi ya kifalsafa kuelekea falsafa za kukataa utawala wa kirumi, na dini yake. Mithili ya watu wanaokimbia tatizo la ubepari wa kirumi, wakakataa na kweli ya kikristo wasijue hata aliyekuwa amejivika vazi hilo awali hakuwa mkristo wa kweli. matokeo yake ikawa ni kama mtu anayechukia risasi, baada ya mpiga risasi. Ujinga ukatawala Zaidi, na fizikia iliyozaliwa bora kabisa toka kwa mababa waliomuamini Mungu kama Newton, Descartes, Galilei, na Leibniz ikazidi kudorora katika falsafa za ukana Mungu. na kadri vizazi vinavyo zidi Kwenda, ndipo zama za ujinga zikazidi kwa kushikiliwa kwa maarifa na watu wachache.

Leo hii wimbi la mashabiki wa nadharia za sayansi za kutokuwepo kwa Mungu linaongozwa na wanafizikia wengi sana, na wenda na kikundi kidogo cha wanabiolojia wa mabadiliko, hasa wenye mitazamo dhaifu ya kijenetikia ‘’Reductionists’’. ambao hata ukiwafatilia, hakuna kikubwa wanachojua Zaidi ya kukariri hisabati za tabia za sheria za asili, na tafsiri dhaifu sana za maarifa. taaluma za ufundi zinazidi kushuka kiwango, kwa kushindwa kabisa kwa karne hizi kutatua matatizo Kama upungufu wa ajira, njaa, ukame, usafiri n.k. Fizikia sio tena mapinduzi ya ufahamu, imekuwa ni Sanaa ya biashara ya vitisho na uongo. Leo hii ukiuliza kuna kipi kipya katika fizikia? Hautapata Zaidi ya taaluma za elimu zisizo na msingi wala uhalisia na umuhimu. Mafanikio makubwa ni kuua watu kwa mabomu ya teknolojia za kawaida sana, ila toka ndege ya abiria wengi igunduliwe, hakuna tena ndege ya mtu mmoja mmoja wala elimu za kuchukua umeme kutoka kwenye anga kama Tesla alivyoota, saivi husemwa kuwa haiwezekani, ila Watoto hufundishwa unaweza rudi nyuma ya wakati.

Pichani ni Nikola Tesla, injinia aliyegundua taknolojia nyingi zaidi kuwahi kutokea. Umeme wa AC tunaotumia, Motors za mashine za usumaku, Rimoti, Radio, Transformer "Tesla coil", na nyingine 300+, alikuwa ana mwamini sana Mungu akiamini Maarifa yanatoka Mbinguni 


Nimeongea yote haya ili mradi msomaji atambue kuwa, uhai wa Wanyama ni kitu kigumu Zaidi huwezi linganisha na roboti. Leo hii wana biolojia wenye uwezo mdogo wa kimaarifa, wanasukuma gurudumu la kuwa, uhai ni matokeo ya mabadiliko ya bahati. au evolution. Wengi wao hawajui hata feni inavyofanya kazi, wameona namna ilivyo ajabu mwili kutengeneza protini zake, wameona namna mwili unavyofanya mahesabu ya ajabu katika kupambana na hali za magonjwa, wameona ubongo ulivyo wa ajabu kuweza kuumba roboti kama binadamu. Lakini bado wanaaminishwa kinyume kabisa na walichokiona. wanaaminishwa uji wa moto ukipoa unaweza unda seli, na wanakubali. ilihali wanajua namna seli ilivyo ajabu kuelezewa, huwezi ilinganisha na CPU ambayo nayo tu haiwezi tokana na uji wa madini ya Silicon yakipoa, hizi sio akili za watu wazima.

Pichani ni Mwanabiolojia maarufu Prof Richard Dawkins asiyemwamini Mungu, na kusukuma zaidi ajenda zake. Hata mchango wake kibiolojia wa "gene centered view" kupitia kitabu chake Cha "selfish gene" umepitwa na Wakati bado akiwa hai.


Wanafizikia wasioamini Mungu na kuibatiza Sayansi yao kuwa Haina Mungu wameshindwa kuelezea tu namna madini ya chuma yanaweza undwa tokea kwenye milipuko waliyojitengenezea, wakaipa miaka mabilioni ili walau ionekane inawezekana, ila wanawashawishi wasomi walio na akili Zaidi yao, ila hawana nguvu kama wao, waamini kuwa miaka mamilioni sasa, itatosha madini ya chuma yaweze kutengeneza 3D structure ya haemoglobin ya kusafirisha damu!! Haingii akilini kwa mtu anaetambua u complexity wa chembechembe za uhai, mawasiliano ya kikemikali za Maisha, mfumo wa fahamu, ufanyaji kazi wa kijenetikia n.k akae meza moja na mwanafizikia wa mabomu, au mwanafizikia wa Space, ashawishiwe kuwa kama vile madini ya uranium yanavyolipuka, ndivyo ATP inavyofanya kazi kuzalisha nishati. Hapo ni kama kulinganisha jiwe na nzi, kusema tabia za jiwe zimwelezee nzi.

Maisha hayawezi umbwa kwa kitu kisicho Maisha. Maisha yana akili na uwezo wa ajabu. Unavunja sheria zote za utimamu kuamini sifuri inaweza zaa moja bila moja. Jiwe halitakuwa na akili hata liishi milele. Vumbi, maji, kaboni, oksijeni, moto n.k havitakuja kamwe kuwa na akili, Maisha ni akili na hakuna namna ya kuyaelezea Zaidi ya hiyo. 

Msingi Wa Elimu Za Mabadiliko Ya Evolution

Msingi wake ni kuwa viumbe wanaweza badilika. Mfano wa kielelezo Kama Ng’ombe anaweza badilika leo hii, akawa watofauti kidogo na alivyokuwa miaka kumi nyuma. basi yawezekana huko zamani alikuwa wa tofauti kabisa, tena hata kama nyangumi. na inawezekana huko zamani, mnyama fulani alikuwa kiumbe aliyeishi majini na nchi kavu. Na inawezekana huko nyuma, huyo kiumbe alikuwa samaki, na inawezekana huko nyuma alikuwa mnyoo, na inawezekana huko zamani alikuwa kama bakteria, na inawezekana huko nyuma alikuwa kama mitokondria, na inawezekana huko zamani, ilikuwa ni protini, na inawezekana huko zamani yalikuwa tu ni madini katika uji uji, ina inawezekana huko nyuma yalikuwa ni mavumbi.

Kutokana na makosa yanayofanyika katika miili ‘’mutations’’ na kupelekea mabadiliko, basi wao huchukua hiyo kama miongoni mwa sababu za haya mabadiliko, kiukweli mabadiliko haya hupelekea udhaifu. na siyo tena kiumbe mpya bora. Hakuna Ushahidi wa kiumbe yeyote wala mabaki ya kiumbe yeyote yule aliye Katikati. Mfano kiumbe aliye kati ya samaki kama nyangumi na ng’ombe, ambao husemwa kuwa wakihusiana.’’no transition fossils’’.

Watu hawa wanasababu nyingi za kumkataa Mungu, kuliko kutetea nadharia zao za mabadiliko. Na baadhi husema, mbona hata Mungu wenu aliumba tokea mavumbini, wanasahau kuwa ni Mungu aliumba, na sio mavumbi yaliyoumba. Idadi kubwa ya watu wanaotia huruma hukimbilia nadharia hizi, kwa lengo la kupata uhuru wa kuamua chochote, bila kuambiwa kuwa watubu wametenda dhambi. na ajabu ni kuwa bado wakitenda dhambi kama ya wizi, serikali iliyowafundisha awali kuwa hakuna dhambi, inawasaliti kwa kuwaua tena. Kiufupi ni machafuko. Huwezi kimbia Maarifa. Maisha ni akili na ni matokeo ya akili. 

Tofauti na sehemu zilizopita, sehemu hii sitagusia sana biolojia pana inayomfunua Muumbaji, hii tutajikita hasa na fizikia na jiografia za ulimwengu, ila kwa ufupi sana juu ya siku ya 5 na 6 za uumbaji wa Wanyama, ifuatayo ni sehemu ndogo inayo elezea kidogo hisabati ya wanyama.

Hisabati Ya Wanyama



Dunia ina mamilioni ya aina mbali mbali za Wanyama. kuanzia Wanyama wadogo kabisa, wadudu, samaki,vyura,reptilia kama nyoka,samaki,ndege,minyoo na wengine wengi sana, kama nyani na binadamu. Haipingiki ya kuwa binadamu anatawala kwa kiwango kikubwa jamii hii ya Wanyama. lakini pia haipingiki ya kuwa, binadamu hawezi kuongoza au kubadili mfumo wowote ule wa jamii hii. ijapokuwa ni rahisi kuhisi binadamu ana uwezo wa kuiondoa jamii Fulani, au kuiboresha jamii Fulani, kwa uwezo aliokua nao. ukweli ni kuwa, hata ukilipua bomu la nyuklia watakufa binadamu. lakini wapo Wanyama watakaoishi kwa mizoga itakayobakia hapo. ni sawa na huu mfano, aliyeunda bomu la nyuklia alikufa kwa ugonjwa wa virusi, na akaozeshwa na kuliwa na bakteria na minyoo, ambao baadae wote wakaongeza chakula cha mimea. ambayo ikaliwa tena na mtoto wa mtengeneza bomu. ni uongo kuhisi kuna teknolojia kubwa sana duniani ya kuweza kutawala na kuongoza kila kitu, ili hali binadamu mwenyewe hawezi kujitambua kikamilifu. Mfano, nani anajua ufahamu “consciousness” unakaa wapi? Au nani anaweza fufua hata inzi? ila tunaweza tu kuua. ‘’hauonekani bora kwa kuweza kuharibu pakubwa Zaidi, ila kwa kutengeneza pakubwa Zaidi. Maana siku zote, zipo njia zisizo na mwisho za kuharibu, ila ipo njia moja tu ya kutengeneza. ndiyo maana unaweza muua inzi kwa moto, maji, ngumi, sumu, umeme, n.k. lakini hakuna njia za kumfufua? 

Hebu tafakari haya maajabu. Ukiwa ndo kwanza unatengenezwa katika mimba tumboni kwa mama yako. kuna uwezo na taaluma kubwa sana yenye maarifa ya uumbaji ambayo hatujui iko wapi, ila tunaona matokeo yake. mfumo huu huongoza ufanyaji kazi kwa kuongoza usomaji wa maelekezo ya kuunda kiumbe. Maelekezo haya huwa yameandikwa kwenye nyuklia, au sehemu ya ndani kabisa ya seli za mwili. hiki ni kama kitabu cha ujenzi wa mtu kisayansi huitwa ‘’DNA”. Ambacho hutoa maelekezo kwa mfumo wa vipisi vya ujenzi wa sehemu moja moja maalumu. Mfano, ujenzi wa nywele, au meno, n.k. hivi vipisi vya kitabu vinaitwa “Genes” ,haya maelekezo ni kama vitabu vya ramani za nyumba. ambavyo hutoka nje ya nyuklia baada ya kuacha kumbukumbu yakiwa chini ya wafanyakazi wanaoitwa ”RNA’’ambao hawa, huchukua kopi ya kile kitabu na kuleta nje ya seli, na huwa wengi, na hufanya kazi tofauti tofauti. moja kwa moja huanza kazi ya ujenzi wa mwili kwa kutumia mfano wa matofali ‘’Amino Acids’’ kujenga mwili kwa kushirikiana na mifumo mingine na kemikali nyingine za mwili ikiwemo Mafuta,madini, na virutubisho vinginevyo.

Nini Sayansi Haisemi Hapa Kwenye Ujenzi

Baada ya hayo matofali ya mwili kuundwa “Amino Acids’’, Ni nini kinacho yawezesha kuunda kitu mithili ya tairi, au gia, au breki. Namaanisha, ni kipi kinachoyawezesha kuunda muundo 3D wa sehemu Fulani ya mwili, ili hali kwa matofali hayo hayo ingeweza undwa tishu tofauti kabisa. Yaani, kama ambavyo kwa uji ule ule wa chuma, tungeweza tusiunde gia tukaunda breki au kisu. Mfano wa kisayansi wa ujenzi ni huu, cheni ya Amino Acids 150 zingeweza kwa kujibadilisha badilisha tu, tena mara mbili mbili tu, zingeweza kuunda miundo 1045 ya tishu. na hapo ikijizungusha kwa spidi ya 1012 kwa sekunde. na bado ingetumia miaka 1026. Lakini cha kustaajabisha, huu ujenzi huenda na kuunda tishu moja kwa moja. mithili ya kama kuna mtu pale. Mfano tishu ya umeng’enyaji iitwayo “lysozyme’’ huundwa tu ndani ya dakika mbili. Mwanasayansi aliyeitwa Christian Anfinsen alishinda tuzo bora ya sayansi kwa kugundua miongoni mwa taaluma za mwili, ndani ya maajabu haya ya ujenzi wa miili ya viumbe inayoitwa “Protein Folding’’. Hii huonesha namna ilivyo ajabu kuundwa kwa protini, wengi wanavyotengeneza picha ya uundwaji wa protini ni kama huishia katika kielelezo cha kuleta bati zilizo kamili, na kusahau, bati hizo hizo zingeweza jenga mifumo mingi isiyohitajika kwa umbo la paa. Kwa kurejea kitabu changu cha Ubongo wa Mtu mweusi mtu anaweza jifunza namna Mfumo mpana zaidi wa maarifa, kuliko Biolojia hii ya jenetikia, unavyohusiana na uundwaji wa viungo na seli za viumbe hai.

Bado wengi hufundishwa tu kuwa matendo ya kijenetikia ya uundwaji wa protini, toka DNA, kama ndicho kiini cha msingi cha Maisha. Looh! Viumbe sio supu ya protini.katika Ubongo wa mtu mweusi nimeelezea namna DNA ni kitu kidogo sana, na tena sio kiini cha uhai kwa mtazamo wa kisasa zaidi wa sayansi. Sehemu kubwa ya uhai bado inaelemea katika mifumo ya taarifa, ambazo zinapatikana katika seli, tishu, mifumo mikubwa ya fiziolojia, na tena kwa kushirikiana na sehemu za chini, kama channel za protini, mpaka genes. Kuna nguvu kubwa sana ya taarifa zisizorithishwa katika genomes, tena zina nguvu zaidi ya genomes. kuna nguvu kubwa sana ya ‘’epigenomes’’. Umeshawahi jiuliza kuhusu ‘’Chaperones’’, hizi hushepu protini inayoundwa, lakini nani aliziambia tunataka shepu Fulani tu? Kama siyo Mungu. basi ni sawa na kitendawili cha Kuku na Yai, nani alianza. Bila kuamini Mungu huwezi kujibu hata maswali mepesi mfano; seli haiwezi kuundwa bila maji, ila seli kwenye maji inakufa? Hakuna Uhai bila chembechembe za Enzymes na Protini, unahitaji Protini kuwa na Enzymes, na unahitaji Enzymes kuwa na Protini, je kipi kilianza? Seli ni kama keki, haijalishi kuna viungo vyote, inajalisha mpangilio, kiasi, muda, joto, maarifa, n.k. je, ni nani aliyeongoza makadirio katika uundwaji wake? Ulimwengu wa awali kwa mtazamo wa big bang ulikuwa na Joto sana, seli inahitaji Oksijeni , nitrogen, n.k. je, ingekuwaje seli zisiungue na kukosa madini haya kutokana na ‘’Strong Oxidation’’? haya ni maswali mepesi sana yanayo thibitisha unahitaji Mungu, kama tunavyohitaji Mpishi Jikoni ili tule.

Ukiwa tumboni kabla ya kujua chochote kile, tayari mwili wako huwa unaanza kuumba Jicho litakalo fanya kazi na Mwanga, Ambao haujawahi uona bado. jicho huumba seli za kusensi mwanga wa rangi ya kijani, blue, nyekundu n.k. ilihali hujawai ziona hizo rangi, mwili hutengeneza unyayo uliokomaa kuliko Ngozi ya juu yake, kama tayari unajua ya kuwa dunia ni rafu, au mwili huunda meno, na vimeng’enya chakula cha wanga, au protini ya mimea, ili hali haijawai ona hii mimea. bado mimba huwa inakua kwa muda maalumu tu, ambao utaiwezesha kupita kwenye njia ya mama, na huwa kwa kawaida hisabati hii ikifanikiwa kwa asilimia kubwa sana. kiasi kwamba hata kufeli kwake huwa kuna sababu zinazoweza elezeka.

Siyo kwa mdudu tu, hata kwa binadamu. mifumo hii ya kubeba na kuunda mifumo ya akili ni ya ajabu sana.

Hebu jaribu kutafakari mfumo wa mwanaume unavyokomaa baada ya kubalehe na ghafla huanza kuhitaji mwanamke ambaye naye, anakua tayari amekomaa kwa huo muda. Lakini hawa wote waliandaliwa na mifumo ya akili, miaka kumi na nne na miezi kadhaa nyuma! bila makosa, lengo linatimia. sio tu kwa via vya uzazi, bali hata kwa fahamu zao. akili za hizi jinsia huonekana kuhitaji kuwa Pamoja, hii ni kama hesabu yenye kutafuta thamani ya kitu baada ya miaka kumi na nne, na inatimia. wakati wewe hesabu ya kujua tu mwakani utakua na shingapi kama saivi, huwezi kujua!

Kwanini Ulimwengu Unaonesha Kuwa Na Maarifa Mengi Zaidi Ya Wanyama?

Mnyama kama binadamu hajui kwanini jua lipo pale, kwanini mimea hutoa chakula kwa Wanyama, kwanini ndege wanaruka na samaki wapo kwenye maji, kwanini mwezi au sayari hazijawai kosea na kuangukia duniani na kumaliza Maisha! ila sisi hasa tunachojua ni vitu hivi vinawezaje kuwezesha Maisha, na vinafanyaje kazi, yaani ‘’How’’. na pia wengi huegemea tu katika kujua kuwa sisi ni watawala. Nahisi huu ni ujinga. unawezaje fika kwenye sherehe ambayo ilihali ukijua hutadumu pale, umealikwa tu. ‘’maana sote twajua Tutakufa”. unafika kwa sherehe na kujiita mgeni rasmi, na kuanza kujaribu badilisha taratibu za pale. kwa kigezo cha mbona sifanywi chochote, hakuna anayekuuliza unajijibu tena mwenyewe, Mbona simwoni mwenyewe. na unajua hiyo sherehe imeundwa kwa thamani, na uwezo mkubwa Zaidi yako, na isingewekwa bure. Hivo ndivyo ilivyo kwa wanadamu wenye taaluma, ili hali wakijua ulimwengu unaonesha hisabati kubwa ya uumbaji, na wakikiri hata tu kompyuta bora Zaidi isingelingana hata tu na uwezo wa ubongo wa Paka, ambaye angejua Kuamua yeye mwenyewe, na kufanya matendo

makubwa ya hisabati. kama vile kujua kukadiria urefu wa alipo mdudu hewani, akamwangalia akajua mahala au angle alipo, kupitia macho na ubongo wake akakadiria kani au force ya kuruka! akajua na huyo mdudu atakavyofikiria pakukimbilia, akamkadiria hukohuko, na akajua wapi atapodondokea wakati wa kushuka.

Tafakari Za Akili “Logic”

Uumbaji Wa Asili Na Wa Kisasa

Yawezekana ukawa ukijisemea naenda Shamba, ukimaanisha unaenda sehemu isiyo na teknolojia. na sehemu isiyo na maarifa kabisa. lakini Shamba ndiyo Kisima cha teknojia, na maarifa makubwa zaidi. na tena Zaidi ya miji iliyojaa ujenzi wa teknolojia zilizo hafifu na duni sana.

Sifa Za Teknolojia Iliyo Ya Juu

Haitumii vifaa vya saizi kubwa. Mfano badala ya Kompyuta kubwa kama nyumba, basi teknolojia kubwa ni kale kadogo kanakoweza hata bebeka.

Unaweza tafakari teknolojia ya ndege hawa wawili na utagundua ipi ni ya kushangaza zaidi

Hutunza habari nyingi sana kwenye sehemu ndogo sana.

tafakari kama DNA ingetoa taarifa zote zilizomo na ilihali ni ndogo usiweze ione hata kwa macho. Je wajua, Gramu nne [4gm za DNA] zinaweza jaza taarifa za ulimwengu wote. yaani dunia, mpaka sayari. kwa takwimu za mwaka 2011.

Huweza fanya kazi nyingi kwa mara moja. mfano simu ingeweza tumika kwa mawasiliano, muziki, kalenda, video, saa n.k. UBONGO hivohivo upo juu kwa CPU

Huweza fanya kazi bila kuongozwa “Automatic’’

Kama ungepewa mashine bora Zaidi ya riadha. basi chui angelikua bora Zaidi. kutokana na uwezo wake wakuongoza matakwa yake

 Hutumia nishati kidogo na huweza jiongoza.

Unaweza usielewe namna wadudu kama nzi macho yao yanavyoweza kutazama kitu, wakakadiria umbali, wakahusianisha spidi na ongezeko la Saizi ya taswira kila wanapoikaribia. Wanaporuka kuelekea kitu, kadri taswira iliyo mbele yao inavyonekana kuwa kubwa, nao wanapunguza spidi automatically mpaka wanatua. Hiki ni kitu ambacho ni kigumu kweli kweli katika kukitengeneza kwa vindege visivyo na rubani ‘’drones’’ ili visigonge vitu, lakini hawa huifanya tu kirahisi. Hii teknolojia ya jicho la Inzi Huitwa pia “optic path monitoring”

Haina hatari kubwa na gharama.Hatari na gharama zote ni sifa ya teknolojia ya chini, ijapokuwa kwa mtazamo wa kawaida, ingeonekana kama kinyume. lakini hebu tafakari kama ingelikugharimu kulipia kati ya shati lako, na hewa ya oksijeni. kipi kingekuwa cha thamani na gharama kubwa? Na je wewe leo, kipi ndicho kinachoakugharimu zaidi?

Hutoa starehe kubwa Zaidi na huvutia zaidi. 

A. Hebu linganisha mivuto ya teknolojia hizi baadhi. Picha ya Sophia, miongoni mwa maroboti maarufu zaidi. Lenye uwezo wa kuchangamana na jamii


B. Picha ya binadamu. Ambaye, watu baadhi wanahisi zipo nyakati binadamu watapoteza uwezo wao. na kutawaliwa na hali bora Zaidi za mashine za Artificial Intelligence. kwa kutengenezewa nadharia sadifu ya ‘’Superman”

Ukiangalia mtazamo tu wa sura, mwonekano wa nje, n.k. utagundua tu ya kuwa, yako mengi sana ambayo yanaendelea kusadikisha ya kuwa hisabati ya ulimwengu ni kubwa sana. na binadamu kitu pekee tunachoweza fanya, ni kujaribu kuiga na kuunda, ili kujisapoti tu sisi wenyewe. lakini si kuhisi tunaweza kushindana na uumbaji wa asili. maana hizo tu picha mbili, zinaonesha ni kama mtoto wa darasa la pili, anayetaka kufanya mtihani wa chuo kikuu, akiwa na sababu zake za msingi.

Chakujifunza Hapa

Sijazungumzia vitu vingi sana. hata baadhi ya viumbe kabisa kama fangasi, bakteria, na wengineo. Ambao nao ni wa ajabu kupindukia. Mfano unakuta kiumbe mdogo kama Bakteria mdogo kabisa, ambaye hatakuonekana haonekani. lakini anaweza fanya maamuzi ya kushindana na binadamu kabisa, na akamuua.. pia sijazungumzia maarifa yanayotawala fikra zetu, ilihali hayapo katika mfumo wa moja kwa moja wa chini ya uhuru wetu wa kuchagua, ‘’subconscious and involuntary minds”. pia sijazungumzia maumbo ya kujirudia, na baadhi ya tabia za kujirudia za ulimwengu. zenye hisabati makini sana. Mfano, 

“GOLDEN RATIOS’’ angalia hii mfano

Utaikuta hata kwa mtoto alie tumboni, au mtu anapozeeka. maana nae hupinda hivyo, au kitu kinapokauka n.k. sijazungumzia teknolojia za ajabu kwa baadhi ya Wanyama. kama mdudu anayetumia Mfumo Wa Gia Kuruka, ndege wanaoona mpaka kwa kutumia mionzi ya usumaku wa dunia kama mantis shrimp anayeona kwa channel 16. viumbe wanaoweza kuunda baadhi ya tishu zao bila kutumia zile ‘’genetics’’. ujenzi wa ajabu wa viumbe wadogo. n.k

Mifumo ya gia ni mifumo inayotawala teknolojia ya binadamu. ila si kwa Wanyama, wala huyu mdudu


To be continued...