Jipatie maarifa kutoka vitabu bora vilivyoandikwa na Dr Brighton shoo kuusu imani, sayansi, afya, teknolojia, asili, malezi, saikolojia na mazingira

SAIKOLOJIA YA TABIA

Saikolojia ya tabia

SAIKOLOJIA KWA MTAZAMO WA SHOO-HYPOTHESIS

Maswali ya msingi sana yanapaswa kuwa; kwanini uwe na tabia hiyo uliyonayo? Je ipi ni tabia inayofaa? Je tabia ni matokeo ya kutengenezwa na kudumu au ya kutengenezwa na kubadilika? Na kwanini kuwe na tofauti za kitabia? Majibu ya maswali haya yote hauwezi kuyapata kwa kuitazama saikolojia kama sayansi. Saikolojia inatazama tabia kwa nje. kuitumia saikolojia kujua sababu za tabia ni kama kumpaka dawa mgonjwa kwenye ngozi kwa ugonjwa uliopo tumboni. Wanasaikolojia wengi zama hizi wanajikita kujifunza Zaidi Ubongo, mfano mzuri ni ‘’Neuropsychology’’, ambapo wataalamu hawa wanahusianisha tabia, na utendaji wa ubongo, bila usomi wa mtindo huu, huwa ni ngumu sana kuweza kuzitambua kiundani sababu za tabia kwa asilimia kubwa.

                                        MSINGI WA TABIA

Tabia ni kama kazi ya kifaa. Fikiria hili, kazi ya kisu ni nini? Je! kisu kazi yake ni kukata ili kusaidia au kukata ili kuua au kuumiza? Kazi ya kisu ni kukata. Kukata ili kuumiza, au ili kusaidia ni matokeo ya mkataji mwenyewe. Hivi ndivyo ilivyo tabia. Tabia ni msukumo wa utendaji wa mwili wa mtu au fiziolojia. Hebu vuta taswira ya hili, vijana wa kiume wengi wanapokuwa katika Balehe huwaza mapenzi kwa kiwango cha juu sana, lakini mawazo haya na msukumo huu wa kupenda mapenzi, ni matokeo ya ongezeko la kama mara tatu ya uzalishwaji wa homoni ya mhemko wa mapenzi ya Testostetone kwa vijana hawa, mpaka kufikia 1200ng/dl. Sasa basi, kama mtu atajiuliza kuhusu tabia, kuwa kwanini vijana wengi sana wa kiume wanapobalehe huwa na tabia ya kupenda sana mapenzi au huwa na tabia za viburi? Je! itakuwa sawa kujibu pasipo kuzingatia mabadiliko haya ya kihomoni? Bila shaka hapana. Swali la msingi linarudi tena, kwanini vijana hawa wanawaza sana mapenzi kutokana na mabadiliko ya kihomoni?

Jibu pekee ni kuwa sasa mfumo wao wa kimwili unawakomaza kuwa wanaume ambao wanaweza kukidhi majukumu yao makuu mawili, yaani kuweza kujitegemea kimahitaji. Hili ndilo linawafanya kutopenda kuendeshwa kwa kuwa wanaanza kuishi kama wanaoweza kujitegemea. Wote wanaotaka kuwaendesha kama viumbe dhaifu lazima watawahisi wana viburi. Jukumu la pili la mawazo haya ya mapenzi ni kuwasukuma kwenda kufanya mapenzi, ili ubongo uthibitishe kuwa mfumo wake wa uzazi unaweza kufanya kazi ya kuzalisha kama ulivyoanza kuutengenezwa toka wiki ya sita tumboni. Kazi hizi zote zinaongozwa na homoni ya Testosterone. Homoni hii ndiyo inaongoza kukua kwa misuli kama vijana hawa wanavyoonekana. hili huwaongezea kujiamini kuwa wanaweza kujipambania, na kupambana. Homoni hii inaongoza uotaji wa nywele kwenye mwili, inaongoza tabia za ukali na uzingatiaji, na inapozidi huzisisimua sana tezi za mafuta ‘’sebaceous glands’’ katika ngozi, na kuchochea sana chunusi.

Kielelezo hiki kina maana kubwa sana, marazote tabia yeyote ile huwa na sababu. Na sababu ya tabia yeyote ile huwa ni kuutetea mwili kuwa katika sehemu salama Zaidi. Hakuna tabia mbaya hata moja, maana tabia zote huongozwa na Ubongo, na hasa mfumo wa kihomoni. Unaweza kuligundua hili kwa kujifunza Zaidi wanyama, inapotokea mnyama Fulani anatabia ya ajabu, huwa ni rahisi sana kumgundua, hii ni kwa kuwa kama ambavyo tunafanana sana kihomoni, wote huwa tunafanana sana kitabia.

Jambo ambalo watu wengi sana wanachanganya, ni neno Tabia mbaya. Hakuna tabia mbaya, neno jema la kulitumia ni shida ya kitabia. Mtu aliyelewa hupaswi kusema anatabia ya kuimbaimba, au kuropoka, hiyo ni shida ya kitabia. Mtu mwenye hasira kali sana, hupaswi kusema ana tabia ya ukali, unapaswa kusema ana shida ya kitabia. Ndivyo ilivyo kwa mtu Mwenye kutojali wengine au mbinafsi, bado tabia za kujali wengine zinahitaji ubora wa mfumo wa Oxytocin na homoni nyingine na mifumo mingine ya ubongo. Watu wenye shida katika mifumo hii huwa na shida sana za ubinafsi. Katika jamii ya leo kuna orodha ya tabia nyingi sana ambazo zinaonekana ni tabia mbaya, lakini kiuhalisia, zote ni shida tu za kitabia. Na nyingi ni rahisi sana kuzitengeneza kama tutakavyoona katika sehemu za mbele za kitabu hiki.

Tabia zote za binadamu zinalenga kumfanya kuweza kukidhi mahitaji yake ya msingi kwa Amani na kuendeleza uhusiano mzuri na jamii yake. Richard Dawkins katika kitabu chake cha ‘’Selfish gene’’ aliandika watu huishi vizuri katika jamii, kwa kuwa wanawekeza mema kwa wakati ujao ikitokea watapata changamoto. Lakini si kweli, watu hawawi wema kwa kuwa ni wabinafsi wanaowekeza kwa kuwasaidia wengine, watu hutendeana wema kwa kuwa wana asili ya uhusiano wa kijamii, wa kindugu na wakiakili ndani yao. Ubongo una mfumo wa kuhisi kuunganishwa na wengine unaoitwa ‘’Mirror neuron system’’. Mfumo huu husisimka watu wanapokuwa na mahusiano ya kijamii. Kwa mfano, Watu wanaokuwa pamoja, bongo zao huonesha kuendana sana mpaka katika mawimbi yaUbongo na Moyo. Asilimia kubwa ya vitu wanavyovipenda watu ni vitu vinavyofanywa na wengine, iwe ni muziki, michezo, uandishi, n.k. hakuna faraja ya binadamu kwa kuweza kukidhi mahitaji yake ya kuishi kwa asilimia 100% akiwa peke yake. Kila mtu anajua faraja ya jina lake kutajwa kwa heshima. hata kama utakuwa na mali, uwezo, na nguvu ya kijamii; vitakuwa na mvuto mkubwa Zaidi kama tu jamii itakuheshimu.

Tabia zilizopo kama kupenda Kuimba, ni kwa kuwa binadamu wanapenda kusikiliza muziki. Muziki unaleta faraja. Tabia ya kupenda kuzungumza, ni kwa kuwa binadamu wanapenda kushiriki taarifa kwa kujifunza, kujikumbusha, na kuburudika. Tabia za kupenda kupika; ni kwa kuwa binadamu wanapenda kula, ili waishi. Tabia za kupenda mapenzi, ni kwa kuwa binadamu wanapenda kuzaa, ili kuendeleza maisha. Inapotokea kuna tabia ya Ulafi, uchoyo, Wivu, n.k. hapo tayari kuna changamoto, na tabia hizi zote tutaziangalia kwa undani Zaidi kiini na sababu zake katika sayansi ya kina ya ubongo. Swali la kwanza; tabia ni nini, tabia ni kazi ya mwili kukidhi mahitaji yake makuu.

Kwanini una tabia uliyo nayo?

Kutokana na mitazamo ya kisaikolojia, inaonekana kuwa kuna tabia mbalimbali za kisaikolojia. Kutokana na Mtazamo Niliouona na kuuita ‘’Space-Time and Behavior”, Binadamu wamefanana katika upande wa Mazingira ‘’Space (S) ‘’, na wametofautiana kwa upande wa Muda ”Time (T)’’. Katika mtazamo huu nimeweza kugundua yafuatayo;

Mazingira ‘’Space’’; Katika mazingira ambayo watu wote wapo pamoja. Watu wote hufanana kitabia. Hii ni kumaanisha, katika wakati huu watu huenenda kwa kufuata utaratibu uleule uliopo, kila mmoja huishi kwa kuzingatia mipaka yake na ya mwenzake. Na hapa ndipo inapoonekana mtu mmoja haendani na wengine, huonekana na changamoto. Mfano, kujipenda Zaidi yeye peke yake ‘’Narcissism’’, au kushindwa kujizuia kufikiria jambo linalomumiza ‘’obsessive compulsive disorder’’. Kuna kushindwa kuguswa na changamoto za wengine. Mfano, Psychopath- hawa hawawezi kuhisi madhaifu ya wengine, hata kama wanayaelewa. kuna Socialpath- hawa wanaweza kuhisi lakini hawajipi nafasi hiyo.

Zipo changamoto nyingi sana ambazo unaweza kuzigundua kwa watu mnapokuwa pamoja, na hii yote ni kutokana na kuwa, kiuhalisia tumefanana sana tabia kuliko tulivyotofautiana katika kigezo cha mazingira au space.

Muda “Time’’; hapa sasa watu huwa tunatofautiana. Katika kigezo hiki watu huwa tunaangukia makundi makubwa matatu, ambayo yanafanania kabisa mtazamo wa awali kabisa wa Plato, unaoitwa ‘’Tripartite theory’’. Katika mtazamo huu, watu wapo katika makundi makuu matatu.

Viongozi na Watafiti ( Watazamaji wa Mbele)

Hawa ni aina ya watu ambao wao hutazamia kesho Zaidi ya kijamii. Watu hawa hutazama Zaidi madhaifu yaliyopo, yaliyokuwepo, na yanayoendelea. Watu hawa huyakosoa sana, na huiwazia kesho iliyobora Zaidi. Mara nyingi watu waliopo katika kundi hili huwa ni watu wasomi wa kina sana, ni watu ambao huwa na uwezo wa kuunganisha sana dot, mimi huwa napenda kutumia neno ‘’Integrative minds’’. Hawa ni watu ambao katika makundi ya awali ya kisaikolojia ungeweza kuwakuta wakiwa na sifa kama za Kutopenda sana kujamiiana au ‘Introverts’ na baadhi wachache extroverts, intuitive, perceivers, thinkers’’ au hata Melancholy.

Nikiongezea sana kwa kazi ya Plato, watu hawa ni watu ambao kiasili hupendelea sana kuwa wapweke kijamii au kifikra, hii ni ishara ya kuwa, watu hawa wanauwezo mkubwa sana wa kujizuia, ni watu ambao wanafikiria kwa kina sana kiasi kwamba kwao kila neno lina maana. Muda mwingi vichwa vyao huwa vina kazi ya kufikiria hata wanapozungumza, taarifa zao huwa ni nzito kwa wastani kwa jamii, na huwa hawaeleweki, faraja yao kubwa huwa ni ubongo wao. Si kweli kuwa watu hawa sio wa kijamii, hapana. Watu hawa huwa kijamii sana, ila katika akili zao. Wao huendelea kuifikiria jamii pindi wengine wamelala. Huwezi kusema mtu kama Albert Einstein hakuwa mtu wa jamii; ili hali aliweza kupitia kazi nyingi sana za watu hata kuja kufanya kazi yake. Kundi hili la watu ambao baadhi huisi kwamba huwa lina motisha ndogo ya kuwa na wengine. Uwenda kutokana na kiwango kidogo cha sensa za Dopamine ‘’DR4’’. Ukweli ni kwamba kundi hili lina motisha kubwa Zaidi ya kuwa na jamii, lakini isiyo katika hali za kidhaifu. Uwezo mkubwa wa kujizuia, ambao wataalamu kadhaa huisi, ni kutokana na kemikali nyingi za kujizuia ‘’GABA”, na kemikali za utulivu wa kiakili ‘’Serotonin’’, huchochea sana msukumo wao wa kutotumia kabisa hisia katika utafiti wao.

Je wewe upo hapa? Unaweza kulijua hili sio kwa kujipima namna unazungumza katika jamii, hapana. Hata introverts huzungumza pia kama Extroverts. Mtu hupimwa kama introverts kwa aina ya mazungumzo yake Zaidi, kuliko muda anaotumia kuzungumza. Introverts na watu walio katika kundi hili hupenda sana kuzungumza mazungumzo yanayohusiana na Kesho ya jamii, na sio leo ya jamii, wala kuhusiana na ishu za kijamii zinazoendelea. Watu hawa hupinga sana mifumo mibaya iliyopo; hata kama ni msanii, utamgundua kwa asili ya hoja zake. Haimaanishi utakuwa bora sana kwa kuwa katika kundi hili, kundi hili lina watu ambao asili imewabalansi kuwa na jukumu la kuonyesha njia ya kesho. Kama ambavyo kuna balansi ya jinsia ya kiume na kike, ndivyo ilivyo balansi ya watu wa kundi hili, na makundi mengine. Watu kadhaa hufatilia kama kuna sababu za kijenetikia za makundi haya au sababu za kimazingira za makundi haya au kama mtu anaweza kubadili asili toka makundi haya. Kutumia jenetikia kuelezea tabia ni mtazamo dhaifu usio na nguvu kabisa, tena hauwezi hata kuelezea jinsia kwa nyakati kadhaa. Binadamu ni Zaidi ya vinasaba vinavyopokea maelekezo navyo toka mifumo mikuu. Huwezi kubadili asili ya ufanyaji kazi wa mwili wako, tabia ni matokeo ya mwili.

Kumbuka, watu wengi huchanganya watu wasiojiamini kuzungumza, wabinafsi na wachoyo, na watu wenye asili ya ukimya unaotokana na kutumia muda mwingi kufikiria. Na ndiyo maana kipimo kizuri cha kumjua mtu anayefikiria ni maneno atakayoyatoa baada ya kufikiria. Na kama ni Introvert au intuitive na hana uwezo mzuri wa kufikiria, bado utamgundua kwa asili ya mada na hoja anazozipendelea. Kumbuka asili huwa hairuhusu uwepo wa watu wengi sana katika kundi hili, kwa kuwa watu hawa; huwa hawafanyi sana kazi, hivyo asili inatambua uwepo wa watu wengi katika kundi hili, unaweza athiri balansi nzuri ya nishati, hivyo mara nyingi watu hawa huwa sio wengi sana.

Walinzi na Watunzaji ( Watazamaji wa Nyuma)

Kundi hili la watu linahusisha watu wenye asili ya kutazama nyuma jamii ilipotoka. Watu hawa mara zote kwao kumbukumbu za zamani huzunguka vichwani mwao. Kundi hili huusisha watu wengi kwa wastani pia, lakini sio wengi sana, kwa kuwa bado kundi hili huwa sio la wafanya kazi wengi sana. Kundi hili huwa lina watu kama wasanii, huwa lina watu wa kupenda kufuatilia utendaji sawa wa haki, sheria na maadili. Huwa ni watu wenye asili ya ulinzi. Watu wengi katika kundi hili huwa wakizingatia sana mienendo ya kijamii na mawasiliano ya jamii.

Katika makundi ya saikolojia watu wengi wa kundi hili utawakuta katika zile sifa hasa za ‘’Sensing, Feeling, Judging, na Extroverts, Sanguine, Phlegmatic’’. Watu hawa huwa pia ni wabunifu sana, huwa na uwezo mkubwa sana wa kumbukumbu, huwa ni watu ambao hupenda sana kuona utaratibu ukifuatwa. Asili inatambua uwepo wa watu hawa huilinda jamii kutorejea katika matatizo ambayo yalikwishakuwepo na yakatatuliwa, na hayapo au yanataka kuanza kujitokeza tena. Kama umeshawahi kukutana na mtu ambaye anahisi ana wito wa kutangaza Amani au kuhubiri upendo, mara nyingi watu hawa huwa wanakuwa katika kundi hili. Watu ambao wanaweza kutunga nyimbo ambazo zinalenga kutatua changamoto zilizopo katika jamii, zikiwapa watu moyo au kuwagusa. kama utawafanyia utafiti katika ubongo wao, utagundua ni watu ambao wana kiwango kikubwa sana cha homoni hasa za uzazi. Mfano, homoni kama Vasopressin na testosterone kwa wanaume, hasa hapa unaweza kugundua kwa Wanajeshi, ambao hukereka sana wanapoona haki zinazofahamika zikivunjwa, utaona Oxytocin nyingi kwa watu ambao wanaweza kuhisi changamoto za kijamii na kuguswa nazo.

Unaweza kuwepo katika kundi hili? Unaweza kujijua kwa namna unaumia unapoona unavunjwa utaratibu mwema uliokuwa unafahamika. Tofauti ya kundi hili na lililopita, kipindi kundi lile wapo radhi kuona damu ikimwagika kutokana na ujinga unaofanyika, kundi hili hawapo tayari kuona damu ikimwagiza kama ilivyowahi kumwagika.

Watenda kazi na Walezi (Watazamaji wa sasa)

Hili ndilo kundi kuu, ambalo naweza sema lina wanaume wa kazi. Kundi hili ni la watu ambao unaweza waita ‘’Smart people’’, hawa katika makundi mengine ya kisaikolojia unaweza zungumzia makundi kama ya ‘’Perceivers, Choleric, lakini wanaweza kuwa Extroverts au introverts’’. Kundi hili linahusisha watu ambao wana msukumo mkubwa sana wa ubongo. Wana Dopamine za kutosha. Watu hawa hawana muda wa kuifikiria jamii, wao wanafikiria Ubongo wao. Watu hawa wanajali Zaidi malengo yao, na wengi wa watu hawa, ndiyo huwa viongozi wakubwa sana, wafanyabiashara wakubwa, huwa wanamichezo wakubwa sana, kila wanachokifanya mara nyingi hufanikiwa sana.

Kundi hili lina wanasayansi wengi sana, na hapa ndipo ninapojazia Zaidi kuhusiana na mtazamo huu wa kale wa plato, ambaye aliandika akiwa hajui kabisa kuhusiana na ubongo, lakini bado alikuwa sahihi kuliko wanasaikolojia wengi wa karne ya 21. Kundi hili huwa lina watu ambao huwa hawafikirii katika namna kama ya wale wa kwanza yaani ‘’integrative thinking’’, kundi hili huwa lina ‘’Deep thinking’’, yaani, watu hawa huwa wanafikiria moja kwa moja dhumuni kuu la kazi yake mpaka anapata jibu. Mfano, kama kungetokea daraja lililovunjika, na ikaonekana hakuna namna ya kuliunga, mtu mmoja wa kundi hili angelifikiria hilo daraja katika namna ya moja kwa moja, ya kiutendaji, hata akagundua nini hasa ni chanzo cha tatizo, na angelipata suluhisho la moja kwa moja. Watu wa kundi hili wengi huwa ni wakandarasi wakubwa, ambao hufanya maajabu makubwa sana kama Nikola Tesla, maranyingi fikra zao huwapa majibu hata bila kujua sababu, au nadharia za mafanikio yao. Tofauti na Integrative thinkers wa kundi la kwanza, ambao kwao huweza kufikiria sana hata kujua huyu amewezaje, lakini pindi huyu bwana anawaza, hakuna anayejua hata yeye mwenyewe.

Kundi hili huwa na watu wengi Zaidi, hili ndilo kundi ambalo linailisha Dunia. Sina nukuu rasmi lakini miongoni mwa wanaharakati Che Guevara aliwahi kusema, kundi hili ndilo Mama wa Ulimwengu. Hawa ndiyo wakulima wakubwa Zaidi wanaoilisha dunia, hawa ndiyo wafanyabiashara wakubwa Zaidi wanaosambaza bidhaa duniani, na hawa ndiyo viongozi wajasiriamali kama Donald Trump. Kumbuka sifa ya ‘’Perceiving’’ katika kundi hili, huwafanya watu hawa kuendana na mazingira yeyote yale, watu hawa ni kama maji, na hivyo huwa wajasiriamali wakubwa, na hawa ndiyo akina Elon Musk, watu ambao wana utajiri wa kuzidi Mapato ya Nchi zote za Afrika Mashariki zikiungana. Kundi hili huwa na uadui sana na kundi lilelile la kwanza, kwa kuwa kundi hili huwa likiitawala dunia mara zote, na watu wake huwa wana nguvu lakini hawana hisia za asili za kuiwazia jamii kama makundi yaliyopita, hawa kwao Nguvu ndilo jambo la msingi Zaidi.

Je wewe upo hapa? Unaweza kujigundua kama upo katika kundi hili kwa kujiangalia namna una nishati na nguvu ya kupambania malengo yako, bila kukata tamaa. Watu wengi walio katika makundi haya, hata burudani kwao huwa ni biashara.

Kwanini Kuna Tofauti ya Tabia?

Kujua kwanini kuna tofauti ya kitabia, namna pekee iliyobora kabisa ya kuielewa pamoja na mitazamo yote iliyopita, ni kielelezo cha Shoo-Hypothesis.

Namna nyepesi kabisa ya kuelewa shoo hypothesis ni kutazama kila kitu kama mawimbi ya muziki, katika neno la kifizikia jepesi Zaidi kuvutiwa taswira basi ni ‘’Quantum Music’’. Ladha ya Muziki ni namna kuna mawimbi yanayoenda Chini, kipindi mengine yanaenda Juu. Muziki ndiyo namna bora Zaidi ya kuyaelewa maisha, maana katika kiwango cha chini kabisa cha kila kitu, kuna muziki. Muziki ni mawimbi, unaposema Ubongo, umeundwa na tishu, ambazo zimeundwa na seli, ambazo zimeundwa na chembechembe zinazoitwa ‘’Organelles’’, zilizoundwa na kemikali kama Protini, chembechembe za nyuklia, mafuta, sukari, na maji. Ambazo zimeumbwa na elementi kama kaboni, oksijeni, nitrojeni, phosphorus, na hydrojeni. Zilizoundwa na chembechembe za elektroni, protoni, na neutron. Ambazo zinaundwa na chembechembe ndogo Zaidi zinazoaminika kuwa ni Fermions kama Quarks, Leptons, na kushikiliwa na mithili ya mawimbi ya Gluon, kukiwa na chembechembe zisizo na uzito kama Photons, na Bosons.

Katika namna ya mwisho kabisa ya kila kitu, basi tu mawimbi tu. Sisi hatuna tofauti na upepo unaovuma, upekee wetu ni namna tumekuwa ni mawimbi yaliyotulia na kutengeneza uzito. Tunapaswa kuelewa hilo ili tuweze kujua kwanini tuna tabia tulizonazo. Jamii ina watu waliojuu wakiwa na nguvu, kwa kiwango sawa na idadi ya watu waliochini wakiwa na udhaifu. Asili imeliruhusu hili ili walio juu watoe nguvu zao kuwainua waliochini, na walio chini wanapopanda juu, basi wanakutana katikati, na hapo ndipo mithili ya muziki wa asili unapochezwa.

Kila kitu katika asili kipo katika mzunguko wa kutoa, na kupokea, na kutunza balansi. Hii ni kama kusema, wakati wa siku dunia inapokea joto, mimea inatengeneza chakula, inatoa oksijeni, na wakati huohuo, wakati wa usiku dunia inapoteza joto, na ndiyo maana hali huwa ya baridi, mimea nayo hutoa chakula chake na makazi kwa wanyama, mimea hupokea kaboni dioksaidi toka kwa wanyama. Kipimo cha kutoa na kupokea nishati mara zote huwa sawa kama sheria ya fizikia inavyosema, muda wa giza na mwanga hufanana sana hasa maeneo ya Equator yenye uhai Zaidi. Dunia pamoja na kusapoti hivi uhai, ipo katika balansi na jua, na mwezi, na hata sayari nyingine. Idadi ya wanyama mwituni wanaokula nyama, na wanaokula nyasi, wakati wote hujitahidi kubalansi. Huu mfanano wa asili ‘’Symmetry’’ ndiyo ulimfanya mwanamama mwanahisabati ‘’Emmy Noether’’ kusemwa ‘’Genius’’ aliyeiokoa Fizikia mpya ya General Relativity.

Unapoona una tabia yeyote ile au uwezo wowote ule; ujue kuna wenye upungufu wa huo uwezo ulio nao. Unapoona una udhaifu wowote ule au uhitaji; ujue kuna wenye nguvu wa kuweza kukuinua katika udhaifu wako. Asili inaruhusu tofauti hizi ili kuwakutanisha viumbe katika uhusiano wa kutoa na kupokea. Asili inafanya hivyo kwa kuwa kutoa na kupokea ndiyo uhusiano pekee ambao unatengeneza hisia za furaha. Kupitia Shoo Hypothesis ndipo utakapogundua kuwa jambo pekee ambalo linaweza kutengeneza faraja, au raha, ni yale mabadiliko, mithili ya muziki kipindi kuna kitendo cha kutoa na kupokea. Mwanamke hujisikia raha sana anapomwagiwa au anapopokea mbegu na mwanaume, na mwanaume hujsikia raha sana anapotoa mbegu kwa mwanamke. Ndivyo ilivyo pia, mtoto hujisikia raha sana anapopatiwa zawadi na mzazi, na mzazi hujisikia raha sana anapotoa zawadi kwa mtoto. Hakuna hisia nzuri kama wanayoipata watu wanaobembea kwenye Kamba, msingi wa hisia hii ni namna watu wanapoteza nishati wanapopanda, na wanapoongeza nishati wanaposhuka, huwa ni mabadiliko ya Potential na Kinetic Energy. Watu hufurahia sana pia wanapoogelea mtoni, kadri mtu anavyoinuliwa na maji, anapoteza hisia za uzito na kujisikia raha sana. Hivyo ndivyo ilivyo siri za tabia. Watu wengi wenye vipawa vya muziki, huwa hawajui tu namnanyimbo zao huwa na faraja kubwa sana kwa wasikilizaji wao wanaopitia nyakati ngumu, uhusiano huu ni msingi wa Shoo hypothesis.

Je unaweza tumia tabia yako sawa na Shoo hypothesis? Katika Biblia liliwahi ulizwa swali kwa Yesu kuwa, kwanini kuna walemavu, na vilema, je kuna dhambi iliyowahi fanyika? Hili ni sawa na swali la je kila udhaifu una sababu za kijenetikia, au uzembe wa kiafya uliowahi fanyika? Lakini Jibu la Yesu lilikuwa ni ili Mapenzi yatimizwe. Hakuna ambaye huweza kulielewa hili kirahisi bila kulifikiria katika namna hii. Asili imeruhusu udhaifu ili Upendo uonekane. Waddington ni miongoni mwa watu walioonyesha huwezi kutabiri hata utengenezwaji wa sifa ndogo kabisa katika jenetikia. Hii ni kusema, hatuwezi kabisa kutengeneza sifa zetu, kila kitu ni matokeo ya asili zetu, hatupaswi kuwa wabinafsi, maana kwa kila kiwango kidogo cha ubinafsi anachokiongeza mtu, anaongeza kiwango kikubwa cha stress. Stress ndiyo muuaji wa kila janga. Stress ni ubinafsi, na asili hutumia stress kuwaua wote wasioenenda sawa na shoo hypothesis.

***********-------**********---------*********----**