Jipatie maarifa kutoka vitabu bora vilivyoandikwa na Dr Brighton shoo kuusu imani, sayansi, afya, teknolojia, asili, malezi, saikolojia na mazingira

MSINGI WA TABIA KATIKA UBONGO WA BINADAMU

RAMANI KUU YA UBONGO WA BINADAMU

RAMANI KUU YA UBONGO WA BINADAMU

Mimi niko wapi katika ubongo

Inatambulika kuwa hisia ya Mimi katika ubongo inahusiana zaidi na namna mtu anavyofanya maamuzi. Mimi katika ubongo ni sehemu tu ya ubongo. Ni Mfumo wa ubongo unaohusiana na maamuzi yangu, hauna mamlaka ya kuongoza Kila sehemu. Hili linatambulika kwa kina zaidi katika zama hizi za sayansi kubwa ya ubongo, hasa baada ya kugundua kuwa, mfumo wa uamuzi wa mtu ‘’perception and decisions’’, unategemeana sana na uchaguzi wa umakini binafsi wa mtu. Mfano mwepesi hapa ni huu, kipindi unasoma sehemu hii, Kuna taarifa nyingi sana zinazokuzunguka, mfano, sauti za magari, ndege, makelele, miziki, wenda taarifa za njaa, maumivi madogo ya ulipokaa,n.k. lakini katika taarifa zote hizo, ubongo huamua kuzipuuzia zote na kuamua tu kuzingatia unachokisoma.

Hii ndiyo huitwa umakini, au uamuzi, yaani "attention", mifumo hii ya mtu kuweza kuamua jambo Fulani tu kati ya mengi, ndiyo inaonekana sana kuhusiana na hisia za Mimi. Lakini changamoto kubwa ya mtazamo huu ni kuwa, awali uliitwa mfumo wa utawala wa ubongo, kwa kuwa ndiyo uliokuwa unaonekana unatawala matendo ya mtu! Ulikuwa unaitwa " executive network", changamoto ni kuwa, bado sehemu kubwa ya ubongo inaonekana kutoongozwa na mfumo huu wa maamuzi na uamuzi wa mtu, mfano mzuri, ni hisia za njaa, utendaji wa viungo vya ndani kama moyo, maini, utumbo, n.k. Hivyo basi, hisia za Mimi hazimaanishi kuwa, "Mimi ndiye Kila kitu", zinamaanisha tu kuwa Mimi, ndiye nina mamlaka makubwa kabisa ya kuamua namna Mwili mzima, unajidhihirisha kwa nje na kwa ndani katika namna ya utambuzi.

Hivyo awali kabisa katika utangulizi huu, ni muhimu kila msomaji kutambua kuwa, katika ubongo zipo sehemu ambazo Mimi naonekana kupatikana zaidi! Na kisayansi Kuna ushahidi kuwa sehemu hizi unapoziharibu! Basi Ile namna mtu huwa anaonekana kitabia, kihisia, kimaamuzi, kimapenzi, kiutendaji n.k. hubadilika Moja kwa Moja! Wakati sehemu nyingine nyingi sana za ubongo ambazo Mimi naonekana kutopatokana huko, hata zikipata shida, changamoto huusiana tu na madhara ya kawaida ya viungo au tabia za kifiziolojia, mfano, shida za kuishiwa nguvu au ku "paralyze", kushindwa kupumua vizuri, athari za utendaji wa viungo vya ndani ya mwilini, kupoteza kumbukumbu Fulani, kuwa na kifafa na mitetemo ya ajabu mwilini, n.k. haya yote yanadhihirisha tu kuwa, maeneo haya ya ubongo hayahusiani Moja kwa Moja na hisia au Mimi haswa katika ubongo. Sayansi hii inawaepusha wasomi dhidi ya mitazamo Hasi ya kuwa, Mimi nipo sehemu ya mbali na ubongo aidha au nipo Kila sehemu kama uwezo wa usumaku, au nipo sehemu mbalimbali za Mwili! Sehemu ya chini tutaona uthibitisho kiundani zaidi katika ubongo, na hiyo itasaidia hata kujua changamoto zinazowapata watu wenye shida za akili, hasa waitwao "vichaa!" Katika jamii za watu.

Sehemu Za Ubongo Zinazohusiana Na Utu Wa Mtu (Personality)

Orbitalfrontal Cortex

Hii ni sehemu iliyopo ubongo wa mbele, kwa chini kidogo! Kama inavyoonekana katika picha. Neno, "orbit" lililopo katika jina lake, linatokana na namna eneo hili la ubongo lilivyo katika mzunguko wa ubongo wa mbele chini.

Eneo hili la ubongo linatambulika kuwa na kazi mahususi kabisa ya kuongoza uwezo wa kuchagua jambo lenye Hasara ndogo na Faida kubwa! Hii sehemu pia huitwa kama , ubongo wa BAJETI! Pale mtu anapokuwa ana mambo mawili makubwa yaliyo mbele yake, aidha kufanya Moja au kufanya lingine! Basi sehemu hii ndiyo huusika. Huangaika kupima uzito wa kila jambo, huangalia faida na Hasara kwa Kila kimoja, na kisha huamua Moja. Inashangaza pia namna eneo hili huchukua taarifa toka sehemu za ubongo zinazohusiana na hisia za harufu ‘’olfaction’’, miguso ‘’somatic sensation’’, sauti ‘’audition’’, vyakula ‘’gustation’’, pia huchukua taarifa toka sehemu za kumbukumbu ‘’hippocampus’’ na ‘’medial temporal lobe’’, maeneo yanayohusiana na kumbukumbu za vitu vingi sana. Na eneo hili la ‘’OFC’’ huwa halina matawi mengi ya Kwenda kusisimua misuli, kumaanisha kuwa, huusiana sana na uchanganuzi tu wa faida kwa kurejea taarifa za kitu toka mifumo yote ya ubongo, na kusaidia uamuzi kwa kushirikiana na sehemu nyingine tutakayo iona mbele kidogo.

Chukulia mfano, Pale mtu anapokuwa anapaswa kuchagua, aidha binti X au Binti Y au Binti Z, n.k, Kwa ajili ya ndoa, ubongo wake huu "OFC" , huonekana kupima tabia na namna Kila Binti hapo juu, anayeweza mpendeza zaidi huku akipima vigezo vyote, vizuri na vibaya kabla ya kufikia hitimisho. Sehemu hii ni ya muhimu sana katika kumtambua "Mimi", kwa kuwa ndiyo msingi wa utendaji wa tabia za "Mimi" pale ninapokuwa na machaguo mengi, na hapo ndipo "mimi" hutofautiana na "wewe". Msomaji anapaswa kutambua kuwa, misingi ya kwanza kabisa pia inayoweza niharibu "Mimi", na kunifanya niwe tofauti na ilivyo kawaida yangu, basi lazima ilenge katika kuathiri sehemu hii ya "orbitalfrontal cortex".

Dorsalateral Prefrontal Cortex " DLPFC"

Hii ni sehemu iliyopo ubongo wa mbele, upande wa juu na nje kama inavyoonekana katika picha. Sehemu hii huusiana na kufanya maamuzi na kufikiria. Hutawala uwezo wa mtu wa kusimamia , kuzingatia na kuongoza utendaji. Uamuzi na umakini au "Attention" ni sifa yake kubwa sana. DLPFC huonekana pia kwa sifa yake kubwa pale mtu anapokutana na changamoto, na Kisha akaamua kutafakari mbinu mpya kabisa ya kuchangamana na changamoto hiyo.

Pale daraja linapokuwa limevunjika! Na watu wanapaswa kuvuka, aidha, kwa kutengeneza daraja jipya, au kutafuta njia nyingine, na baada ya kuamua, ile Hali ya kusimamia utendaji wa maamuzi hayo, katika Hali zote hizi "dorsolateral prefrontal cortex" huonekana ikiwa imesisimka sana, kwa namna ambavyo Huwa inahusika sana. Kumbuka, Huwa ikihusiana pia na sehemu nyingine zote za ubongo, lakini yenyewe ndiyo huonekana ikiwa kiongozi mkuu.

Sehemu hii pia huusiana na sehemu ya ubongo wa kati "parietal lobe", ambayo huungana kutengeneza network inayoitwa "fronto-parietal network", hii kwa pamoja hutambulika kama mfumo wa ubongo wa kutafakari, huchangamana na sehemu kadhaa pia tutakazoziona, mfumo huu huwaka sana, mtu anapokuwa akitafakari au fikiria. DLPFC ndiyo msingi wa uwezo wa ubongo wa kujizuia, hii sehemu hushika rimoti ya mwili dhidi ya nguvu za msukumo wa kihisia. Ukisikia! ‘’Juma anaweza kujizuia sana kuliko Jose’’, hiyo kitaalamu ni sawa na kusema, ‘’DLPFC ya Juma inafanya kazi zaidi ya DLPFC ya Jose katika jambo fulani’’.

"Mimi" inaonekana kuhusiana sana na sehemu hii, na mtu anapoathiriwa katika eneo hili, kama kwa baadhi ambao wameshapata changamoto katika eneo hili, huonekana kuwa ni watu waliobadilika kabisa! Visa kadhaa huonesha kuwa, waathirika huonekana kutokuwa watu wenye uwezo wa kuzingatia, kufanya kazi, Huwa na tabia za tofauti kabisa ukilinganisha na awali kabla ya kupata tatizo, na wengi wao huonekana kuwa na hasira na tabia zingine za kushindwa kabisa kwa uwezo wa kujizuia. Hivyo hii ni sehemu ya muhimu sana katika kumtambua Mimi. Na ukitaka kumtriki "Mimi", basi mtafute hapa. Binadamu ndiye mnyama mwenye sehemu hii kubwa zaidi, na Ina matabaka sita. Hii kitaalamu inaonekana kumpatia binadamu faida ya kufanya maamuzi ya tofauti zaidi kulingana na mazingira yake, au "Highest Flexibility" ukilinganisha na wanyama wengine kuelekea chini, ambao wao, hufanya zaidi maamuzi kulingana na mazoea yaliyolenga kuongeza nafasi yao ya kuishi au "Highest Reflexive".

Ventromedial Prefrontal Cortex "VMPFC"

Hii ni sehemu ya ubongo wa mbele, iliyopo ndani chini kama inavyoonekana katika picha. Sehemu hii inatambulika kwa kazi Moja kubwa ya kusimamia mabadiliko baada ya kubadilishwa kwa maamuzi, toka sehemu ya juu na nje ya ubongo "DLPFC". Watu wenye shida katika sehemu hii, huonekana kutokuwa na uwezo au hupata wakati mgumu sana kukubaliana na mabadiliko waliyoamua kuyafuata.

Sehemu hii pia huusiana sana na mifumo ya ubongo inayohusiana sana na tathmini binafsi ndani ya mtu. Mtu anapokuwa hafanyi jambo lolote Lile, au hafanyi kazi, Anawaza kuhusu maisha yake binafsi, Huwa Kuna network inayoitwa "Default mode network" ambayo Huwa inasisimka. Na sehemu hii ya ubongo ya VMPFC ni Moja ya sehemu za network hii. Hivyo hii ni sehemu kubwa sana inayohusiana na "Mimi", hisia za kutathmini maisha binafsi ya mtu, hisia za kukubaliana na mabadiliko ya changamoto za maisha, n.k. hutengeneza msingi unaomtambulisha "Mimi". Watu kadhaa ambao huisi hisia za mimi, ni ubinafsi, Basi hujaribu kukinzana na utendaji wa sehemu hizi za ubongo. Na kama ukiathiri utendaji wa sehemu hizi, mtu hubadilika kabisa katika namna ya umimi wake.

Anterior Cingulate Cortex "ACC"

Hii ni sehemu ya ubongo iliyopo ndani kabisa ya ubongo, inayozunguka shina la ubongo linalounganisha ubongo wa upande wa kulia na kushoto "corpus callosum", sehemu hii hii kama inavyoonekana katika picha, ni sehemu inayohusiana na kazi Moja kubwa ya Kutofanya au KuruhusuMakosa.

Hii sehemu ndiyo mara zote humsisimua mtu kuongeza umakini katika kazi anazozifanya, au maamuzi anayoyafikiria kuyafanya, au tamaa zinazomsukuma, Ili asifanye Makosa. Hii sehemu ndiyo huongeza hisia za hofu ya kukosea. Kama mtu angekwazwa sana, na akataka kupigana, na Kisha akaghairi, Basi katika ubongo wake unaweza kuona "ACC" ikiwa imesisimka sana kwa namna inavyofanya kazi kubwa ya kuchakata taarifa. Hivyo, "Mimi" ambaye naweza laumiwa kwa kutoweza jizuia, na kufanya maamuzi mabaya kabisa ya kujidhalilisha au yakuniletea Hasara. Au Mimi ambaye naweza kuwa na ujasiri wa kufanya ufisadi au kufanya ukatili Bila huruma, hiyo inaweza toa kisio kuwa Mimi, naweza kuwa ni matokeo ya athari kubwa katika eneo hili pamoja na maeneo ya kulizunguka. Eneo hili huchangamana sana na eneo la pili tuliloliona likiitwa "DLPFC" ,kwa pamoja haya huongoza uwezo wa kufanya maamuzi mazuri. Kutambua eneo hili kutasaidia kuelewa namna ubinadamu wa mtu unavyoweza kuathiriwa kwa kucheza nalo.

Posterior Cingulate Cortex "PCC"

Eneo hili kama linavyoonekana katika picha ya juu, ni sehemu ya nyuma ya "cingulate cortex", imeungana kwa mbele na "ACC", sehemu hii hufahamika kwa sifa yake kubwa ya "self-awareness" au ile Hali ya "kujitambua". Eneo hili ni sehemu pia katika Ile network ya "default mode network" ambayo tuliiona inahusiana na tathmini binafsi ya mtu. Pale mtu anapojitafakari mafanikio yake, Makosa yake, Nini anatamani, ndoto zake, njia zake, n.k. hisia zote hizi za umimi, msingi wake ni eneo hili, pamoja na maeneo yake ya karibu. Eneo hili huusiana sana na hisia za furaha, motisha na maumivu kutokana na tathmini binafsi za mtu. Kumbuka hisia hizi za furaha n.k. hazitoki katika eneo hili. Isipokuwa eneo hili linahusiana Moja kwa Moja na mfumo wa hisia hizi, unaoitwa "limbic system". Huko mbeleni tutaona namna maeneo haya yanavyoweza athiriwa kwa mbinu baadhi za kisaikolojia, na kupelekea hisia tofauti kabisa na Hali ya umimi ambayo mtu angepaswa kuilinda au kuisimamia, kama utambulisho wake.

Striatum

Eneo hili ambalo lipo kwa ndani sana katikati ya maeneo ya ubongo yanayohusiana na hisia na kumbukumbu, kama inavyoonekana katika picha, huusiana na kazi Moja kubwa sana, ambayo ni kuongoza nguvu ya motisha na hisia za msukumo wa raha au karaha, kulingana na Hali yoyote Ile au kazi yoyote au hata maamuzi yoyote Yale ambayo mtu huyapitia.

Sehemu hii huusisha maeneo ya ubongo ya " Substantia nigra" na maeneo ya "ventral tegmental areas" . Maeneo haya huzalisha kemikali mbalimbali za motisha ya ubongo, hasa, Dopamine, ambayo huchochea hisia za motisha na raha, na pia huchochea kemikali zingine kama serotonin na endorphins, ambazo humfanya mtu kujisikia raha, kwa mawazo Fulani, hisia Fulani au kazi fulani au taswira Fulani. Pia huusiana na maeneo mengine ya kuzunguka eneo hilohilo yanayoitwa ‘’nucleus accumbens’’, ambayo nayo huusiana na uzalishaji wa kemikali za dopamine za motisha. Nguvu ya Mimi kupenda kutenda sana maswala Fulani zaidi ya mengine, Inatokana na msisimko ambao Mimi naupata zaidi ukilinganisha na wengine. Hivyo basi kama ukiathiri utendaji katika eneo hili, basi unaweza pata mtu ambaye anaweza kuwa na msisimko au kutokuwa na msisimko kabisa na baadhi ya vitu, na itakuwa ndiyo utambulisho wake.

Eneo hili linasifa Moja kubwa sana pia, eneo hili huwa ndiyo kitovu Cha utendaji wa dawa zote za kulevya, pombe, sigara na Kila bidhaa ya uraibu hata na tabia za uraibu. Hivyo unaweza mbadilisha mtu, vipaumbele vyake na hata utu wake, kama utakuwa na uwezo wa kucheza na hili eneo. Na mbeleni tutaona triki za kisaikolojia zinavyofanikiwa sana kwa kuweza kucheza na hili eneo. Picha chini inaonesha mishale ambayo ndiyo inatoa uelekeo mkuu wa uzalishaji wa homoni za dopamine za motisha ya utendaji wa ubongo. Unaweza ona namna mishale yote chanzo chake ni sehemu ya ndani kabisa, ambayo ndiyo tuliyoiona inayoitwa striatum.

Limbic System Hasa "AMYGDALA"

Huu ni mfumo wa hisia, kama unavyoonekana katika picha. Mfumo huu huusiana sana na maeneo mengine ambayo tumekwisha yaona, ikiwemo "cingulate cortex", lakini pia huusiana na sehemu ya ubongo inayohusiana na utendaji wa mifumo ya Mwili isiho ya hiari, inayoitwa "hypothalamus". Mfumo huu Huwa na sehemu iliyo ndiyo kiini kikubwa sana Cha utendaji wake, inayoitwa "amygdala".



Yaweza onekana kama picha ngumu kueleweka, lakini hoja ya msingi ni kujua eneo lake ilipo na maeneo yake ya msingi sana ya kuyafahamu ambayo nitayaelezea.

Amygdala huusiana na hisia za hasira, utulivu na hisia zingine ambazo unaweza ziweka katika makundi hayo makubwa mawili. Uharaka wa mtu kupata hasira na kupambana au kutulia, pia huusiana na hisia hizi katika sehemu hii. Kumbukumbu zinazohusiana na maumivu ya matendo yaliyowahi muumiza mtu Huchakatwa katika eneo hili pamoja na eneo lingine linaloitwa "hippocampus" ambalo linapakana nalo maeneo haya. Kama ukiniuliza jambo Gani ninalo lipenda zaidi, au linalonipa raha zaidi, au ninalolitamani zaidi, basi kama litakuwa ni kwenda Mbinguni, Basi taarifa kuhusiana na mbingu, huzungushwa katika kumbukumbu na pia katika huu mfumo. Hii ni kusema tu utambulisho wa umimi kulingana na mapenzi yangu, umejikita katika utendaji wa maeneo haya. Mbele kidogo tutaona namna maeneo haya yanavyoweza kuathiriwa na kuleta shida kuhusu ubinadamu wa mtu.

Insula Cortex

Hii ni sehemu iliyo ndani pia karibia na makutano ya ubongo wa pembeni "temporal lobe" na wa kati parietal lobe, kama inavyoonekana katika picha.

Eneo hili huusiana na hisia zote za umimi zinazotokana na taarifa za mifumo yangu binafsi ya Mwili. Chakula ni kitamu sana, najisikia raha katika Mwili wangu, harufu hii ni nzuri, moyo wangu umetulia, Najisikia kichefuchefu, n.k. hisia hizi kuhusu umimi, hujenga msingi wa utu wangu, mapenzi yangu, machukizo yangu, n.k. Athari katika maeneo haya, huusiana na Hali ya kutotulia kabisa ndani ya mtu. Pale unapomwona tu mtu na Kisha ukajikuta "umesisimka", Aidha kwa kumpenda au kughadhabika. Hizi huitwa "visceral markers". Hufanana na nyingine za nje, mfano, unapomwelekeza mtu, mpaka akatikisa kichwa, Hizi huitwa "somatic markers". kwa zile za ndani huusiana sana na sehemu hii "insula". Wakati zile za nje au somatic huusiana na "parietal lobe" au ubongo wa juu kati. Mimi ni matokeo ya ninachojisikia. Pale mtu anapojinyonga ni matokeo ya maeneo mengi ya ubongo yanayokuwa yameathiriwa kabisa, ukijumuisha na hili.


RAMANI YA ENEO LA UBONGO KWA UJUMLA UNAPOWEZA KUMPATA MTU (MIMI)

Shoo-Hypothesis.

Kwanza ukirejea maendeleo ya mfumo mzima wa fahamu, mpaka ubongo unapokamilika. Utagundua kuwa mfumo wa fahamu unaendelea katika namna kama ya treni linalotengenezwa kuanzia kwenye mabehewa, halafu linamaliziwa kwa kutengenezwa kichwa chake. Baada tu ya kichwa chake kukamilika, kinaanza kuongoza treni lote tena. Hoja hapa ni kuwa, kichwa cha treni hakiundi mabehewa, hakiwezi kutawala kila mfumo wa behewa, lakini chenyewe ndicho kinaamua treni litaenda au haliendi. Ijapokuwa hakiwezi kuamua pia mfumo wa umeme wa kila behewa ambalo lina mfumo wake wa kujitegemea, Lakini ndicho kinatengeneza maana nzima ya mfumo na mitambo ya treni.

Pia kama ilivyo katika mifumo ya nchi, makao makuu ndiyo huwa yameendelea zaidi ya maeneo yoyote yale, hueshimiwa kama kitovu, lakini haimaanishi bila makao makuu, hakuna tena Maisha katika falme Fulani. Ubongo Pia una eneo ambalo ndilo makao makuu. Eneo hili ambalo makao makuu, ndipo ‘’Mimi’’ napatikana. Ijapokuwa watu wengi hutambua kuwa, sehemu hizi ndizo za ‘’Prefrontal cortex’’, ni kweli, lakini siyo peke yake. Ni maeneo yote kama nitakavyoonesha katika ramani ya chini.

Picha hii inaonesha mfumo mzima wa maendeleo ya ubongo, tazama sehemu ya mbele ya ubongo.


Ukitazama katika hizi picha unaweza pata kielelezo kizuri cha kuelewa maana ya eneo ‘’Mimi’’ anapatikana, hii ndiyo makao makuu kabisa ya mfumo wa Ubongo. Mfumo wa uti wa mgongo huongoza utendaji wa sehemu mbalimbali za mwili, za nje na viungo vya ndani. na hupanda hata kufikia sehemu za juu za uti wa mgongo, ambapo hukutana na ubongo wa nyuma chini, medulla na pons, ambazo nazo huongoza zaidi mifumo ya mwili isiyo ya hiari, kadri unavyopanda unakutana na sehemu ya kati ya ubongo ‘’mid-brain’’, ambapo inahusiana na kuchakata sasa, taarifa zinazohusiana zaidi na mazingira yanayotoka nje ya mwili. Hapo ndipo unaanza kukutana pia na sehemu za ubongo zinazohusiana na namna mtu anavyotafsiri mazingira yote ya ndani ya mwili, na pia nje ya mwili.

Watu wengi husahau kuwa, hata maeneo ya ubongo ambayo huusiana sana na kuongoza matendo yasiyo ya hiari, maeneo haya yanapopata shida, hupelekea mfumo mzima wa ubongo wa juu, kutafuta namna ya kuyatatua matatizo hayo. Mfano ni huu, ijapokuwa, hatuna uwezo wa kutawala utendaji wa moyo kwa hiari yetu, lakini inapopatikana shida, huwa tunajua kuwa kuna shida katika mfumo wa damu au moyo, na huwa tunatengeneza dawa na mitambo ya kutatua tatizo hilo. Hivyo bado unarejea katika hitimisho kuwa, sehemu niliyopo ‘’Mimi’’, ndiyo sehemu iliyo makao makuu ya Ubongo. Mfumo wa ubongo au fahamu kwa ujumla unaanza kuumbwa ukiwa bado hauna fahamu, na unapopata fahamu, unakuwa kama mtu aliyelelewa na kufundishwa mpaka akawa na maarifa ya hali ya juu kabisa. Hivyo katika namna zote hizi mbili ‘’logic’’ inaonesha kuwa lazima kuwepo mfumo wenye nguvu zaidi nyuma, na ndiyo maana kusoma sayansi ya ubongo bila kumtambua Muumbaji haiwezekani kiufasaha zaidi, maana utashindwa kujua maswali ya kwanini? ingawa utasifiwa kwa kujua ‘’kivipi?’’