Jipatie maarifa kutoka vitabu bora vilivyoandikwa na Dr Brighton shoo kuusu imani, sayansi, afya, teknolojia, asili, malezi, saikolojia na mazingira

ASILI NA UUMBAJI WA DUNIA

Asili ya ulimwengu

 ASILI NA UUMBAJI WA DUNIA

Sayari ya Dunia iko katika mwendo mkali sana wa kilomita 30 kwa kila sekunde kulizunguka Jua, yaani lisaa limoja linapoisha ni sawa na kusema Dunia inatembea umbali wa kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza mara 93. Kipindi Dunia inalizunguka Jua, nalo Jua linatembea kwa spidi kubwa ya Kilomita 250 ndani ya sekunde katika Galaxy yetu kubwa ya Nyota ‘’Milky way’’. 

Tupo katika spidi kubwa ajabu tukizunguka jua, huku tukizidi kwenda mbele. Bahati mbaya walimu wa Jiografia huwafundisha watoto kuwa sayari zinalizunguka jua kana kama Jua limetulia katikati, na sayari zinarudia mzunguko uleule, hayo ni makosa, tazama chini uhalisia halisi wa mfumo wa jua.

wote tumezaliwa tukiwa katika hii safari ya kasi kubwa sana, watu hawahisi wanatembea kama wanavyohisi wanapokuwa kwenye gari kwa sababu dunia inatembea katika spidi isiyobadilika badilika, na huu ndiyo msingi wa Fizikia ya ‘’Special relativity’’ iliyomfanya Albert Einstein kuwa Maarufu, huwezi kutofautisha mtu aliye katika sehemu iliyosimama, na anayetembea katika spidi isiyobadilika ‘’constant velocity’’. Kila jamii zina mfumo wa kuhesabu miaka, hesabu hizi huturudisha katika mwanzo kabisa mwa safari. Katika mtazamo wa kawaida kabisa, ili kitu kitembee kinahitaji Nguvu au kani ya msukumo. Ulimwengu pia una asili ya kupoteza nishati kama vile ambavyo gari lingesimama baada ya mwendo mrefu kwa kupoteza nishati ya Mafuta. au Mtu angehisi njaa na kuishiwa nguvu baada ya kupoteza Nishati ya Chakula. Ni kama Amri kuu katika Fizikia kuwa Siku zote Nishati hupungua. Sheria za mwendo za ‘’Isaac Newton -First and Second Newton’s Laws’’ na sheria kuu ya Uelekeo wa Nishati ‘’Second Thermodynamic Principle’’. Zinaturejesha katika maana kuwa, Hata Dunia isingeweza kujitembelea tu yenyewe, lazima kiwepo chanzo cha Nishati ambacho hicho kitatoa Kani ya kuisukuma iendelee kuzunguka hata hii leo. 

Dunia inazunguka kwa sababu kuna Nguvu ambayo inaizungusha katika mhimili wake. Dunia na Jua ni kama Risasi ambazo zinaendelea kutembea baada ya kulipuliwa toka kwenye Bunduki. watu wengi Duniani wasiojua elimu hii ndogo, huwa hawaelewi kwanini sayansi imejikita katika kutafuta asili ya ulimwengu. Dunia na Ulimwengu kwa Ujumla vina mwanzo. na hii ndiyo sababu ya kusema kama ulimwengu usingekuwa na mwanzo, Basi hata Jua lingekwisha zima, Kwa maana Siku zote Jua huwaka likipoteza Nishati yake, yaani Jua hupungua kila sekunde. na kama ulimwengu ungekuwa hauna mwanzo ‘’eternal’’, basi Jua lingekwisha zima, maana lingekwisha isha. Tumia kielelezo hiki kuelewa kirahisi, kama ungekuta Mshumaa unawaka, halafu mtu akakwambia Mshumaa huu upo milele yote au aseme hauna mwanzo, Basi ungemwona ni Mjinga maana ungemuuliza, kwanini haujazima mpaka leo, maana hata hapa nauona unaendelea kupungua! sasa iweje ulikwepo milele na unaendelea kuisha na bado haujaisha?

SABABU ZA MSINGI ZA KUTAMBUA KUWA ULIMWENGU UNA MWANZO 

Kwa hatua ya awali kabisa ya kujifunza asili ya ulimwengu, hizi ni sababu za msingi na nyepesi kabisa za kusema ulimwengu una mwanzo.

KUTANUKA KWA ULIMWENGU ‘’universe expansion’’

Ulimwengu unatanuka, yaani ukiachana na dunia kujizungusha katika mhimili wake, ulimwengu ambao ni mpana Zaidi, kama nitakavyouelezea hapo mbele, ni kama puto linalotanuka. kila sekunde unatanuka kwa maili nyingi sana. Sasa basi, kitu chochote ambacho kina kwenda kwa kasi kikitanuka, basi ujue kimetoka kwenye kiini au mwanzo. Hii ni kwa sababu, ili utanuke maana yake lazime uwe mwanzoni ulikonda.

Kisayansi kuna Ushahidi mkubwa sana wa kutanuka kwa ulimwengu. kwanza kupitia uwepo wa mionzi myekundu kutoka kwenye ulimwengu mbali, mionzi hii myekundu huitwa REDSHIFT.

REDSHIFT NI NINI?

Redshift ni kama ambavyo wakati wa jioni, au asubuhi, huwa unaona jua likiwa linatoa miale ya rangi nyekundu. au Gari likiwa limekupita wakati wa usiku, basi utaona kwa mbali sana rangi za mwanga wake zikionekana nyekundu njano hivi. Hii inatokana na kuwa, Mwanga tunaouona una rangi saba. au frequency za rangi saba. Rangi hizi zinatofautiana kutokana na frequency zake. Frequency ni kama nguvu ya miale, mfano, Rangi ya bluu ina nguvu au frequency yake iko juu ukilinganisha na rangi nyekundu ambayo frequency yake iko chini. kwa hiyo rangi nyekundu humaanisha kuwa, mwanga huo nguvu yake ni ndogo. Na ndiyo maana unaona rangi nyekundu wakati wa jioni na asubuhi, kipindi jua linapokuwa mbali na dunia. kisayansi Redshift humaanisha pia kuwa, kadri kitu kinavyokuwa kinaenda mbali Zaidi na wewe, basi mionzi yake inazidi kujinyoosha ‘’Stretching’’ na kuwa mirefu na hivo frequency zake kuwa katika rangi ya wekundu.

Sasa basi tukirejea katika mada kwa kutumia picha za Telescope, ‘’hizi ni kamera za kuangalia anga’’, picha zinaonesha uwepo mkubwa sana wa Redshift, ambazo hizi zinathibitisha kuwa ulimwengu unatanuka.

Zifuatazo ni picha zinazoonesha kielelezo cha hizi Redshift, na picha kutoka katika Anga ‘’Universe’’ zinazoonesha makundi mbalimbali ya nyota ‘’Galaxy’’ kama yanavyoonekana toka mbali.

MABAKI YA MIONZI YA MWANZO WA ULIMWENGU ‘’Cosmic Microwave Background’’

Miongoni mwa ugunduzi mkubwa sana mwaka 1964 uliofanywa na wanafizikia Arno allan Penzias na mwanaanga Robert Wooldrow Wilson, ni kugundua uwepo wa mionzi midogo sana katika kila sehemu katika ulimwengu, au anga ‘’cosmos’’. kiasi cha kushinda tuzo ya wanafizikia bora wa mwaka ‘’Nobel Prize’’. Kwa kawaida kama ungeangalia anga wakati wa usiku, basi ungeziona nyota na sehemu kubwa sana iliyo jaa giza ‘’empty space’’. Ulimwengu au space uko wazi ‘’empty’’, sehemu kubwa Zaidi ikiwa mithili ya kitu cheusi kisicho na miale yoyote ile ya kuing’arisha, lakini watu hawa waligundua kuwa kuna mionzi midogo sana ambayo inafanana kwa kila sehemu katika ulimwengu, tena kwa kuwa na jotoridi sawa la 2.7K (-270°C). Kumbuka anga ni la baridi sana Zaidi ya Friza ‘’Freezer’’.

Hii ina maana gani? Hii ina maana ya kuwa, hebu chukulia kielelezo hiki, kama kuna shamba lingekuwa limechomwa moto, au kuna vitu vimeungua ndani ya nyumba. Hata baada ya ule moto kuisha. Kama mtu angekuja, au pita katika mazingira yale. basi angehisi tu hata harufu ya mabaki, na hii ingempa taarifa moja kwa moja ya kuwa, kuna vitu viliungua. Kwa upande wa Cosmic Microwave Background, nayo ni namna hii hii, ulimwengu unaonesha miaka mingi sana ya nyuma, ulipitia mlipuko mkubwa sana ambao ulikuwa na joto kubwa sana. Ambalo linaonekana kuwa lilipoa baada ya muda Fulani. na baada ya kupoa, ulimwengu umekuwa hivi ulivyo leo, lakini bado kuna mabaki ya nishati joto, ile ambayo ili hali haina nguvu ya kusababisha nuru kubwa, lakini ina uwezo wa kusababisha nuru ndogo ambayo iko katika kila kona ya ulimwengu huu. na kwa mantiki hii, ulimwengu una mwanzo.

NADHARIA ZA FIZIKIA ZA ABERT EINSTEIN NA MLINGANYO WA FRIEDMAN.

Miongoni mwa mijadala mikubwa sana baadhi ya nyakati, sio kuwa ulimwengu ulitanuka, maana hilo liko wazi. Ila kuwa je ulimwengu unaendelea kutanuka? Hata mimi binafsi sina uhakika wa asilimia mia ya kuwa ulimwengu unaendelea kutanuka. au hauendelei. mwanafizikia albert Einstein aliwahi pia shindwa kutambua kama ulimwengu unatanuka. na hata kupitia mlinganyo wake ‘’equation’’, alionyesha ya kuwa ulimwengu hautanuki, lakini baadae kidogo ikaonekana kuna makosa aliyafanya na akarekebishwa na wanafizikia wengine, hasa mwanahisabati ‘’Friedman’’. Ambaye alirekebisha na kuonesha ulimwengu unaendelea kutanuka. Wazo hili hupendwa na wanafizikia wengi ya kuwa ulimwengu unatanuka, maana nao wana nadharia yao ya kuwa ulimwengu unamwanzo unaitwa ‘’Big Bang’’. 

Maajabu makubwa Zaidi ni kuwa, kadri fizikia inavyozidi kukua, imegundulika tena ya kuwa ulimwengu unatanuka tena kwa kasi kubwa Zaidi ya awali. Jambo hili ni la kufurahisha sana, hasa kwa wasomi wa sayansi wanaoijua Biblia. lakini ni la kuchanganya sana kwa wasomi wa sayansi ya asili tu. Huko mbele tutaangalia Zaidi, lakini cha muhimu hapa ni kutambua ya kuwa, ulimwengu una mwanzo.

Mlinganyo wa Kutanuka Kwa Ulimwengu

Maana ya hizo herufi. H -Hubble’s Constant, C-Speed of Light, G-Gravitation Constant, K -Curvature of Universe, ê“¥-Cosmological constant and R -Radius of universe.

HISTORIA ZOTE ZA ULIMWENGU

Katika kila jamii ya Duniani, kuna historia ya uwepo wa Muumbaji Aliyeanzisha, au kuumba ulimwengu katika wakati wa awali kabisa. na Muumbaji huyo anahitaji kuabudiwa, na pia ndiye mtatuzi wa changamoto zote za watu wake. Dunia katika kila kipindi huwa na watu wengi Zaidi wanaoamini uwepo wa Mungu, kuliko wasio amini, ijapokuwa watu hawa hutofautiana sana misingi yao ya Imani. lakini msingi mkubwa ni kuwa, ulimwengu una mwanzo. 

Historia ya sayansi pia inaonyesha, wanasayansi wa awali na mababa wakubwa Zaidi wa sayansi, waliamini katika uumbaji wa Mungu. na walijitahidi kutumia sayansi kuelewa Zaidi kuhusu uumbaji. lakini katika zama za karne ya kumi na tisa mwishoni, idadi kubwa ya wimbi la kutoamini Mungu lilipata nguvu kupitia Imani ya asili kama mungu, yaani Imani ya kuamini ijapokuwa ulimwengu una mwanzo, lakini mwanzo hakuwa Mungu. Swala la kuamini ulimwengu una mwanzo, linanguvu asilimia Zaidi ya 99% kwa mtazamo wa sayansi na Biblia. Hauwezi bishana na mtu kwamba ulimwengu hauna mwanzo, kwa maana hiyo ni mithili ya watu wazima wawili hata wakikataa kuwa hakuna kifo, na asiwepo mtu wa kuwapinga, haitabadili maana ya kuwa kifo kipo.

NAMNA ULIMWENGU ULIVYOANZA

Kwa miaka mingi sana Watoto wamekuwa hawafundishwi mwanzo wa ulimwengu wakaelewa. kwa maana nadharia wanazotumia kufundishia, ni nadharia za upande wa wasioamini Mungu. na idadi kubwa ya Watoto wanatoka katika familia zinazoamini. Tatizo la kwanza, Nadharia zenyewe hazieleweki vizuri kiasi kwamba kila siku zinafanyiwa mabadiliko, mfano, toka mwaka 1948 mpaka 2003 nadharia inayotumika ilikuwa na gunduzi zilifanywa 2, matatizo yanayotokana na kufeli kwa nadharia yalikua 7, ikabadilishwa mara 4. hapo sijaenda ndani Zaidi kwenye swala la muda, mara utaambiwa ulimwengu una miaka bilioni2 na bwana Hubble, mara utasikia ni bilioni 13.8 mwaka 2013. Kwa lugha ya kawaida ni kuwa, hata mwalimu ambaye angeelewa, asingeweza fundisha! maana anachokijua kimeshabadilishwa. halafu pia nadharia hizo zinahitaji Imani kubwa sana. maana hazileti mantiki, kama tutakavyoona hapo mbele. Kumbuka wanasayansi waliofanya mambo makubwa, hawapo katika kizazi hiki cha teknolojia.

Nitaanza kuelezea ulimwengu ulivyoanza kuumbwa, kwa kutumia nadharia za sayansi ya Biblia. na kisha nitatumia nadharia za sayansi hiyo ya wasioamini. Nafanya hivi kwa maana wao huanza na zao, na humaliza na zao tu. mithili ya hakuna kinachojulikana upande wa pili, ilihali wanajua kila kitu ila wanaficha. na hii ndiyo sababu ya mimi kuandika kitabu hiki. 

To be continued...