IMANI ZA UCHAWI, MAZINGAOMBWE NA MASHARAIKI YA MBALI
IMANI ZA UCHAWI, MAZINGAOMBWE NA MASHARAIKI YA MBALI
01/4
Mipaka Na Udhaifu Katika Uwezo Wa Fiziolojia Ya Ubongo
Ubongo ambao unatambulika kwa ubora na uwezo mkubwa sana wa kufanya kazi na kugundua vitu vigumu, taaluma kubwa, na teknolojia za ajabu kuwahi kutokea, Bado una mipaka ya utendaji wake, na pia una udhaifu kadhaa katika utendaji wake. Kila kitu kinachofanywa duniani na mwanadamu ni matunda ya ubongo. Hata elimu ya kuujua Ubongo, bado ni kazi ya Ubongo wenyewe. Ubongo ndiyo mtambo ulio ‘’complex’’ kuliko kitu chochote katika ulimwengu tulichowahi kiona kama Binadamu, na mfumo uliounda ubongo na ulimwengu wake, ndiyo mfumo ulio complex zaidi ya mfumo wowote ulimwenguni.
Pamoja na ubora wake, ubongo huwa na udhaifu kadhaa. Na katika huu udhaifu, ndipo shida zote za namna zote duniani huanzia. Hata unaposikia, mtambo wa nyuklia umeripuka, ujue ubongo wa wataalamu kadhaa ulifeli hisabati kadhaa. Ukisikia ugonjwa Fulani hautibiki, Ujue ubongo wa wataalamu kadhaa umefeli biolojia fulani. Lakini kubwa zaidi katika kitabu hiki, ni namna ambavyo ubongo unapofeli kuzijua sanaa Fulani, na kuziita Giza.
Nguvu Za Giza
Si ajabu neno ‘’Nguvu za Giza’’ kutumika kumaanisha Ushirikina, ambao unaonekana hautambuliki. Ni sahihi kabisa katika sayansi inapotambulika kuwa kitu kinaonekana matokeo yake, ila hakitambuliki, kupewa jina la ‘’Giza’’. Vipo vitu vingi katika fizikia ya mfumo wa ulimwengu ‘’cosmology’’ ,vinavyoitwa vitu giza au ‘’Dark matters’’. Ikitokea Nguvu zinaonekana zikisukuma, lakini haijulikani zinatokea wapi, au zikoje zikoje, Basi huitwa Nguvu giza au ‘’Dark Energy’’. na hizi nguvu ni asilimia 73% ya nguvu zinazoonekana kuusukuma ulimwengu, ikiwemo na mfumo wetu wa jua, lakini bado hazifahamiki. Kwa hiyo hata neno Nguvu za Giza katika Biolojia, kutumika kumaanisha nguvu zenye matokeo katika biolojia za watu, lakini hazifahamiki, ni sawa kabisa. Ijapokuwa wanabiolojia kadhaa wanaliogopa neno hili la kisayansi.
Unaona neno ‘’Dark Energy’’ kumaanisha Nguvu za Giza katika ‘’Physics’’ ya ‘’Cosmology’’. wanabiolojia tumekuwa nyuma sana kufatilia sayansi kadhaa kisa tu hazihusishi matumizi ya hospitali, ilihali wagonjwa wengi zaidi wanaamini ‘’nguvu hizi’’, na hata baadhi ya wataalamu. Lengo kubwa siyo kuamini Nguvu za Giza, lengo ni kujua wapi zinapopata Nguvu, na kujua namna ya kuwasaidia wahanga wa hizi nguvu, ambazo ni sanaa za miaka mingi sana.
Mipaka Na Udhaifu Wa Fiziolojia Ya Uwezo Wa Ubongo
Mfumo Wa Kuona Na Umakini
Tunapaswa kuamini tunachokiona, lakini hatupaswi kuamini kwa asilimia 100%, hii ni kwa kuwa, mfumo wa kutazama huwa una mapungufu kadhaa, ambayo yanatengeneza njia ya kuweza kutrikiwa kiakili kwa kushindwa kutengeneza uhalisia halisi. Rejea hoja zifuatazo kutazama baadhi ya mipaka ya fiziolojia hii muhimu. Utambuzi ni wa Taswira Iliyopo katika Ubongo, siyo iliyopo nje. Ijapokuwa baada ya mwanga kukifikia kitu, na kuakisiwa kwa uelekeo wa jicho, kupita katika mboni za macho, hata kufika katika seli za kuona, taswira huenda kukamilika kuundwa katika Ubongo, sehemu ya nyuma ya ubongo ‘’occipital lobe’’. Tafsiri ya taswira hii, huusisha sehemu kadhaa za ubongo ambazo taarifa zile za kuona huwa zimepita maeneo hayo, ambazo ni sehemu za ubongo wa kati na pembeni, na ubongo wa mbele huusika kutengeneza maamuzi kuhusiana na taswira hiyo. Lakini, bado taswira huwa ni matokeo yanayotegemea zaidi ubongo wenyewe, kuliko hata kilichopo pale.
Mfano wa kwanza, Mtu yuleyule mimi naweza mwona tofauti na wewe unavyomwona. Hiyo siyo kwasababu mwanga wa jua umetofautiana katika namna ya kutufikishia taarifa, La hasha; Ni namna ambavyo sisi, ubongo wetu huiboresha na kuichakata taarifa ile kwa uchochezi wetu binafsi. Inaweza boreshwa kwa mvuto zaidi, au kwa ubaya zaidi.
Mfano wa Pili, mtu anapokuwa amelala, huwa anaota ndoto. Ndoto huwa zinakuja baada ya mtu kumaliza mzunguko wa hatua nne za kwanza za usingizi, ambazo huwa hazihusishi mizunguko ya jicho, au huitwa pia ‘’non-rapid eye movement sleep’’ kifupi ‘’Non-REM Sleep’’. Hatua hizi zinapoisha, baada ya dakika takribani Tisini hivi, mtu huingia katika hatua ya usingizi ambayo ndiyo huwa inaambatana na ndoto. Hatua hii huitwa ‘’REM-Sleep’’ kwa kuwa hapa, Jicho huwa linazunguka kama vile mtu yupo macho. Na pia mtu ubongo wake huwa ukiwa umesisimka ‘’active’’ kama ubongo wa mtu aliyekuwa hajalala. hoja ni kuwa, Mtu anayeota, huwa anaona. Lakini swali ni Je, ni kweli anaona vilivyopo pale? Kama Jipu ni Hapana. basi sio kila unachokiona kipo pale.
Mfano wa tatu, Wavuta bangi, madawa ya kulevya, magonjwa yaliyofikia hatua za kuathiri Ubongo, Ugonjwa unaoitwa ‘’schizophrenia’’, wagonjwa wake huwa vichaa, Ugonjwa wa kifafa hasa hatua kubwa au unatokana na shida za ubongo wa kati, Mara karibia zote, watu hawa huwa wanaona taswira za ajabu sana. Mara nyingi watu hawa huwa wanaona taswira ambazo, watu kwa kawaida huwa hawazioni. Na kitaalamu taswira hizi huitwa ‘’hallucinations’’, swali pekee ni kuwa, je taswira hizi kweli zipo? Uhalisia ni Hapana. Hoja ni kuwa, kinachoonekana mara zote huwa kilichopo katika Ubongo, na sio kilichopo pale.
Mfano wa nne, tazama picha hii chini na kisha utajibu swali moja jepesi sana.
Katika picha hii kitu cha kwanza ambacho ulikiona ni nini?
Kitu cha kwanza ambacho umekiona katika hii taswira ni matokeo yaliyotegemea zaidi kipaumbele, ambacho kimetolewa zaidi na ubongo wako, na sio uhalisia. Kuna wengine watakuwa wamemwona Bata, lakini kuna wengine watakuwa wamemwona Sungura. Na kama mtu atakuwa hajawahi mwona mmojawapo, yaani Sungura au Bata, basi Picha hii itakuwa ni ya mnyama mmojawapo tu wa aliyewahi mwona. Hizi zote zinathibitisha kuwa, asilimia kubwa zaidi ya tunachokiona, kipo katika Ubongo.
Mfano wa tano, tazama nje kama kuna Jua. Kadiria ukubwa wake wa uhalisia. Kuna uwezekano mkubwa sana kuwa makadirio yako sio ya kweli. Hivyo ndivyo inavyokuwa mara zote, Ubongo hutengeneza makadirio ya unavyoviona kulingana na taarifa unazozijua wenyewe, na sio lazima ziwe za ukweli. Watu wanaotazamwa usiku kwa mara ya kwanza, huwa kiuhalisia na mionekano tofauti kidogo na mwonekano wao ambao ungeonekana katika mwanga mkubwa. lakini mara zote, ubongo huchukulia taswira zao kama ni kamili kabisa. Ubongo huwa haukubali kuwa hauoni kama unaweza kiona kitu. Ukiambiwa na mtoto mdogo sana, kuwa ‘’kuna mtu mkubwa kwelikweli’’, kiukweli, huyo mtu anaweza kuwa mtoto mwenzake tu aliyemzidi urefu kwa tofauti ndogo sana.
Mfano wa sita, Mara nyingi Ubongo hukadiria kwa kufananisha mionekano, kana kama ina rangi kamili au sura nyororo, wakati uhalisia huwa sio nyororo wala kamili. Ukitazama shati jeupe katika mazingira ya kawaida, huwa linaonekana jeupe bila hata madoa, labda yawepo makubwa sana. Na huwa hivyo pia kwa rangi zingine na sura za vitu ‘’surfaces’’. Hii inatokana na udhaifu wa Ubongo, wa kushindwa kujua tofauti za mipaka inapokuwa midogo midogo sana. Huwa kuna msemo unasema, ‘’hakuna Ngozi isiyo na vinundu vinundu’’, sema tu huwa vidogo sana, na macho huchukulia tu kama ni nyororo.
Macho Huwa Hayaoni muda mwingi na yanaficha. Jicho huzunguka mizunguko mitatu kila baada ya sekunde Moja. Na kila linapozunguka katika mzunguko mmoja, huwa halioni kwa 1/10 ya sekunde au unaweza sema, huwa kwa kila mzunguko halioni kwa muda wa 100milliseconds. Sasa basi, kwa siku binadamu huwa anazungusha jicho lake mara 150,000. Na kwa mantiki hiyo binadamu kwa kila siku huwa anakuwa Kipofu, au Haoni kwa masaa manne ‘’4’’. Cha ajabu Katika nyakati zote hizi binadamu huwa haisi kama huwa haoni, hata wewe ni shahidi, tangu uanze kusoma sura hii, umegundua kama kuna wakati huwa hauoni? Kama jibu ni Hapana, basi Jicho lako limekudanganya.
Katika msingi huu hoja ni kuwa, miongoni mwa triki kubwa sana za Ubongo, zinachochewa na sifa yake yenyewe ya kujazia magepu sehemu ambazo huamini kuwa umeona, na kumbe haujaona. Ubongo huwa unatengeneza mategemeo yake ya namna ambavyo unategemea taswira itaendelea kuonekana. Hii tabia ya ubongo lengo lake ni kusaidia kutafakari jambo katika namna endelevu, bila kubanwa na vituo. Kumbukumbu za unavyozidi kutazama,‘’intermediate memories’’, ndizo hujazia magepu haya’’.
Mfano wa kwanza, kama unamwangalia mtu na ghafla kikapita kitu mbele yake. Wewe utaendelea kumwona katika mwonekano wake uleule kamili. hata kama kile kitu kuna wakati kilifanya mwonekano wake usionekane kamili kiuhalisia.
Mfano wa Pili. kama mtu atakuwa akikarusha kampira juu kwa mkono, na kisha akikadaka tena kwa mkono. Na akawa akifanya hivi mfululizo, na mtu mmoja akawa akimfatilia kwa kukatazama ka mpira kanavyoenda juu na chini. Ikitokea huyu mtu katika mfululizo wa kitendo hiki, ghafla akamshtua mtazamaji wake katika wakati wa kurusha, kwa kusema, ‘’Tazama kamepotea juu’’ huku akiwa ameigiza kama kukarusha, na uhalisia amekabana mkononi mwake, basi mtazamaji atashtuka, Kwa kuwa ataamini kweli hakajarudi, kamepotea. Kiuhalisia lakini ni kuwa, Ubongo umetengeneza kumbukumbu ya mfululizo wa utendaji, ambazo zimekinzana na uhalisia, na hivyo, huyu Mtu alipodanganya hoja yake ikapata Nguvu, ikisapotiwa na uongo wa Ubongo unaotokana na mazoea ya kukadiria matokeo hata kabla ya kitendo, katika matukio ya mfululizo.
Macho Hayawezi kuchakata Spidi kubwa za Vitu ‘’high Processing rate’’. Mfano vitu kumi na tano vinapopita ndani ya sekunde moja mbele ya Jicho, lazima vitasababisha jicho lishindwe kuchakata hiyo taarifa. Na matokeo yake, jicho lazima litatoa tafsiri isiyo sahihi. Na ndiyo maana hata watu wengi hawajui kuwa, video zote ni picha tu zinazopita katika spidi kubwa, na Ubongo unazikusanya kama tukio linalofanyika kwa mfululizo. Udhaifu huu wa Ubongo hutumiwa sana na watu wa triki baadhi, huweza kufanya mizunguko mikubwa na ndani yake wakifanya mizunguko midogo, na matokeo yake Ubongo hushindwa kutengeneza uhalisia na kutengeneza taswira ya uongo. Na wakati mwingine, kitu ambacho ni kigumu kabisa, kama mtu atakitembeza kwa umakini na polepole kimfuatano wa mzunguko au mtembeo wa kitu Fulani, kinaweza onekana kama nachenyewe ni laini kama kamba, kumbe ni kitu kigumu kabisa.
Mfano mtu akiwa ameshika karata kwa vidole mkononi mwake, na akawa akiipandisha na kuishusha kwa spidi, na ghafla kwa vidole vyake vingine akaizungusha kuelekea kwa nyuma ya mkono wake, kama wanavyofanya wasanii wa triki za karata. Basi watu watakao kuwa wakitazama, watashangaa kwa hamaki, kwa kuwa wataona ni kama muujiza kupotea, na kumbe ni macho yao tu yalishindwa kuchakata spidi nyingine kwa uelekeo mwingine, kwa kuwa zilikuwa ni taarifa za fastafasta katika uelekeo tofauti.
Ubongo hauwezi kuzingatia taarifa nyingi kwa wakati ‘’multi-tasking’’. Yawezekana hii ndiyo mbinu kubwa zaidi kwa wanamazingaombwe wa mbinu za kawaida, au wale wa kamali. Watu hawa huwa wanashughuli nyingi sana za kuteka akili za watazamaji wao kwa wakati mfupi, na mara nyingi, shughuli hizi huwa haziingiliani. Na kwa kawaida, ili mtu awe na sifa za kuweza kuwa msanii wa sanaa hii, lazima awe mtu wa tabia za uongeaji sana, mwana komedi sana, mtu mwenye vituko vingi asiyetabirika, Na hata wengi wanaotumia usanii katika wizi, huwa na mafanikio katika msingi huu. Hawa watu mara zote humfanya mtu azingatie jambo Fulani kwa umakini mkubwa kabisa, huteka kabisa umakini wa mtu. Na kisha, kadri mtu anavyokuwa ameanza kuzoelea matokeo ya umakini wake, humuingizia ajenda ambayo itamtoa katika ufatiliaji wake, na anaporudi katika ufatiliaji wake wa kwanza, huwa amepitwa na baadhi ya taarifa, kipindi, anapojaribu kutafakari, msanii wake ili hali akijua alichokifanya, hushtuka kana kama na yeye hajui lililotokea, na kadri mtazamaji anahamaki, msanii anaongeza zaidi kumfanyia triki kwa kuongeza sitofahamu.
Kwanini Hufanikiwa Hapa, Hutumia Mbinu Ya Uelekeo wa Upofu wa Jicho ‘’Blindspot’’. Hii mbinu inashangaza sana. Na hakuna mtu anaweza iepuka kama atakutana nayo. Iko hivi, unaposoma neno lolote lile katika sura hii, uelekeo wa macho yako na umakini ni moja kwa moja katika neno husika. Ndani ya ubongo wako unajiambia kuwa, unatazama kila eneo linalokuzunguka lililo mbele ya uono wako. Ni kweli unaona, lakini uhalisia ni kuwa, kuna maeneo yako mbele kabisa ya uono wako, lakini maeneo hayo huyaoni. Hii ni kwa kuwa, kuna sehemu ndani ya jicho inaitwa ‘’Blindspot’’, hiyo sehemu hakuna seli za kuhisi taswira, kitalaamu ni eneo ambalo neva ya Jicho inapita ‘’optic nerve’’.
Katika eneo hili, taswira zote zinazofika huzioni. Lakini Ubongo kama kawaida yake huzijaza kana kama unaona kila kitu. Sasa basi, mfano mtu akijua uelekeo wa eneo hilo mbele yako, anaweza badilisha kitu, au ongeza kitu, au ondoa kitu. Na kisha akakwambia, hebu tazama kitu Fulani kimetokea, au badilika, au ongezeka, Lazima mtazamaji atashtuka sana. Na kushtuka huku kunatokana na kuwa, alihisi kuwa anatazama kabisa, lakini kumbe hakuwa kiuhalisia akiona. Mtu anaweza chukua kitu ambacho wewe unaamini kabisa anakiweka katika uelekeo Fulani, lakini akiweza kucheza na uelekeo sahihi wa ‘’blindspot’’ yako kiuhalisia, basi kamwe hutaweza kugundua kuwa, Pamoja na kuwa ulikuwa ukishuhudia akifanya kitendo Fulani, lakini mwenzako alibadilisha bila wewe kujua. Na mtindo huu, hutumika sana katika sanaa za kawaida za mazingaombwe ya vitu, na hata kamali na wizi pia. Picha chini inayoonesha mfano wa namna eneo hili linavyoweza kumtriki mtu, na kumshtusha mtu kwa kitu ambacho hakikuwepo kiuhalisia.
Namna Nyingine kubwa hapa, ni tabia za kuongeza mzigo wa taarifa katika ubongo, wasanii huwa na tabia za kumchekesha mtu, kumkatiza mtu ufuatiliaji wake, kumtikisa mtu, na mara zingine hata huamuru baadhi ya vitendo kwa watazamaji wao, ili kuwafanya wawe wafutiliaji endelevu, hulenga kuwasisimua kirahisi zaidi. Kadiri ubongo unavyokuwa na mambo mengi ya kufuatilia, huwa na ufanisi mdogo na mdogo zaidi. Iliihali ubongo bado huonesha kana kwamba haujazidiwa. Hii ndiyo sababu utakuta, mtu hata umkataze asitumie simu wakati wa kuendesha chombo cha usafiri, bado atakukatalia akiamini bado anaweza mudu yote, lakini ukweli ni kuwa, asilimia kubwa sana ya ajali husababishwa na mitindo hii.
Wakati mmoja nikiwa napita maeneo Fulani yenye msongamano wa watu, nikakuta kijana mmoja akijigonga kwangu na kunitikisa kwa kusema ‘’tembea vizuri kaka’’, kipindi akiwa anazungumza, ndipo kwa neema ya Mungu tu nikagundua, mwenzake mmoja akikaribia kumaliza kuvuta kabisa simu yangu kwa kutaka kuniibia. Hii ni mbinu ya ‘’multi-tasking’’, kitendo cha kunitikisa, kuniongelesha kwa kunikemea, maswali binafsi ya kwanini afanye vile? Taarifa zote hizi, zilipunguza nguvu ya mfumo wangu wa hisia za miguso, kuweza kujua kuwa simu yangu kuna mtu anaelekea kutaka kukamilisha kuiiba. Ndivyo ilivyo pia kwa sanaa hizi, taarifa nyingi ambazo watu hawa huzichochea, ukiongeza na triki zingine kama za juu, basi mtu hujikuta akiwa tayari ni mhanga wa moja kwa moja wa utapeli wa kifikra.
Kutabirika kwa Vipaumbele vya mfumo wa Umakini ‘’Attention’’. Wasanii wengi wa wasanaa za ‘’magic’’ husema kuwa, ni rahisi sana kumtriki mtu timamu sana, ukilinganisha na watu wasio timamu. Hii ni kwa kuwa, kuna mambo ambayo Ubongo uliotimamu unapokutana nayo tu lazima utajikuta umeyazingatia. Mfano, kama atatengeneza mazingira ambayo ni kama yana hatarisha uhai hivi, au yanaweza tengeneza aibu kubwa hivi, Ubongo huwahi kuhemka hata kabla ya matokeo, ili kuongeza umakini, kwalengo la kuwahi kuzuia. Lakini kwa mwigizaji, hii huwa ni faida sana, hufanya vitu vyakushtukiza ambavyo ubongo huwa na hamaki kubwa sana. Mfano mtu ambaye angeigiza kwa kufanya kama anavunja shingo yake vile, na kisha akaweka sauti ya kitu kinachovunjika kwa sauti kama ya mfupa.
Ubongo wa watazamaji lazima utashtuka sana, kwa kuwa utaamini kuwa yawezekana unaweza vunjika kweli, na baada ya kugundua kuwa ni usanii tu, basi huishia kuburudika, lakini sio kuwa unapenda, La hasha. Ni kwasababu tu za kisaikolojia nitakazozielezea pia. Kama mtu atachukua kitu kama chupa ya glass, akakivunja na kikawa kikisagika kwa sauti za glass, na kikaonekana kama glass, na akaanza kula hizo glass. Aisee, ubongo wa watazamaji lazima utawaka kwa msisimko mkubwa, Ubongo utakuwa ukivuta picha ndiyo wenyewe unayofanya matendo yale ‘’rejea mfumo wa mirror neuron system’’ sehemu zilizopita. Pia kuna michezo ya kuigiza uigizaji na umwagaji damu kama uhalisia, hizi triki huwa sana kwa filamu, ubongo husisimka sana kwa kweli, msingi ni uleule.
Mwanamazingaombwe kila anachokifanya kama utakuwa unamwangalia, lazima utaingia katika mtego wake. Hii ni kwa kuwa, vitu vyote ambavyo atakuwa akivifanya, anajua lazima kwa ubongo timamu utavifuatilia, na yeye huwa na mafanikio zaidi kwa kutumia mbinu zingine. Katika mpira wa miguu inapopatikana penalty, watazamaji wote huwa wanaangalia eneo lile lile, hilo hata kwa watazamaji wa filamu, kama tulivyoona katika Vol02, kitendo cha wote kuangalia sehemu moja Kinamaanisha kuwa, uwezo wa umakini ‘’attention’’ unatabirika. Kipindi kikundi cha vijana wa kiume wa rika Fulani wanapokaa kwa Pamoja, Na ghafla akapita binti mmoja aliyevaa katika namna ya kuonesha maumbile yake, Vijana wengi watakaomwangalia binti huyu, watamwangalia maeneo ya kufanana na katika vipindi vya kufanana. Hii ni kawaida kabisa, umakini unatabirika sana, na ni muhimu watu kuwa makini sana. Tazama picha
Katika picha uliyoitazama, unaweza gundua kuwa muda mwingi sana umetumia katika kuzichunguza sura za hao watu, kuliko kuangalia taarifa zingine. Huu ni mfano wa hoja ya kuwa mfumo wa umakini ‘’attention’’ unatabirika.
Udhaifu Wa Ubongo Katika Kumbukumbu ‘’Working Memory’’
Mbinu hii ni pana sana, na katika hatua hii ya kwanza, huwa inatumika pia katika triki za mazingaombwe ya kawaida. Hapa kinachotokea ni hiki, ubongo huwa una aina tatu za kumbukumbu, kuna zile za muda mfupi sana ‘’intermediate memories’’, kuna zile za muda mfupi ‘’short-term memories’’, na kuna zile za muda mrefu ‘’long-term memories’’. Hapa triki huwa ni hii, katika mzunguko wa kumbukumbu, Ubongo huwa na kiasi maalumu cha taarifa za kuzizingatia kwa kila baada ya muda, kama utampatia mtu idadi kubwa zaidi, Basi huyo mtu hataweza kukumbuka. Mara nyingi kwa namba hazipaswi kuzidi saba, Zaidi ya hapa mtu atasahau. majina yanaweza kuwa matatu tu, Sura labda moja tu kwa wakati, n.k.
Hasa Kwenye Karata, Unapompatia mtu taarifa nyingi kuliko uwezo wake wa kuzingatia, Madhara yake huwa, mtu husahau. Na sasa basi, kama mtu huyu atasahau, kisha ukampitishia namna za taarifa zinazofanania na alizokwisha ziona, huyu mtu kumbukumbu ya kufanania itakuja, ‘’kwasababu ya tabia ya ubongo inayoitwa Priming’’ lakini utakapombadilishia, lazima atashangaa sana kwa mshtuko. Hii sanaa hutumika sana kwa wanamazingaombwe wanaotumia Karata. Hawa jamaa hushika karata, huwa wanazungumza huku wanakuonesha wakizichanga, zile karata zao huwa tayari na mipangilio ya hesabu zao, pia huwa kuna karata baadhi wanazigeuza kuwapa alama za vituo. Na hata wanapomuambia mtu achague yeyote ile, na wao wataijua, huwa wanajua kuwa kwa kipindi chote cha mchezo, umakini wa mtu, na uwezo wake mdogo wa kumbukumbu, hataweza kuzingatia baadhi ya usanii wao. kumbuka hizi ni mbinu rahisi sana za magic katika hatua ya kawaida kabisa.
Kutumia Lugha ya Alama na Sauti kumpoteza mtu ‘’Mis-direction’’. Hizi pia katika hatua ya kwanza huwa na nguvu sana kwa wasanii wa hatua za awali. Kipindi wasanii hawa wanapokuwa wakifanya sanaa zao hupenda sana kutumia sauti za vidole kumfanya mtazamaji kuangalia kilichopo pale, huku wao wakitumia udhaifu huo wa kuteka umakini kubadilisha baadhi ya vitu kwa wakati huohuo, pia wanaposhika vitu mikononi mwao, hutengeneza miondoko hewani ambayo watazamaji huwa wakiifatilia kwa vichwa vyao, wakijua au bila kujua. hii tayari pia ni faida kwao kutengeneza sanaa ya uongo kwa kutumia tabia zao kadhaa tulizokwisha ziona.
Mfumo Wa Kusikia
Sauti hutumiwa na wasanii wa triki za ‘’magic’’ kama zinavyotumika ala za muziki au mapigo ya muziki katika nyimbo. Tayari mapigo hueleza hatua iliyofikia ya muziki, na hueleza kuwa sauti ya mwimbaji inapaswa ipande au ishuke, ianze au iache, n.k. wasanii wa ‘’magic’’ hupenda sana kuchukua umakini wa watazamaji wao kwa kutimia sauti, kama tulivyoona katika sehemu zilizopita. Lakini kikubwa hapa ni kuwa, Sauti Hujua Hisia Zilipo. Kila binadamu ni mhanga wa sauti ambazo zinaweza kuwa zina ujumbe wa hisia za furaha, ‘’kumbuka zile biti za miziki ya Chrismass, au Birthday-Songs’’, kuna biti za kutembea kijeshi, ‘’zile zinazopigwa jeshini, ukizisikia tu unaguswa kutembea kikakamavu’’, kuna biti za nyimbo za huzuni hasa za misibani, kuna biti za hisia za mapenzi, n.k. lakini hapa hawa watu huwa na biti au ala zao maalumu kabisa.
Hutumia biti za kutisha. hizi ni biti ambazo huuambia ubongo kuwa, kuna kitu hatari kinaenda kutokea. kumbuka zile biti katika filamu, zinazoonesha kuwa ‘’Jini’’ anaenda kutokea, au kitu kibaya kinaenda kutokea. Hizi biti sio kuwa ni biti tayari zinazofahamika na Ubongo, Hapana, hizi biti huwa na siri moja, huwa zikipigwa zikiongeza Frequency za sauti zake. zinapoanza biti moja na jingine hupishana kwa kitambo kikubwa, lakini muda unavyoenda, muda wa kupishana hupungua, na sauti huongezeka. Ubongo unapohisi sauti hizi, hutiwa tashwishwi kwa asili. mtu anaweza jiuliza zaidi, kwanini Ubongo uogope hizi biti? Jibu ni kuwa, kwanza asili yenyewe tu haina sauti za muundo huu, hivyo huwa zikiushtua ubongo. pili Ubongo hutengeneza makadirio kulingana na mtindo wa sauti unayoisikia, rejea kielelezo cha ‘’predictive coding model’’ nilichoelezea hata kwenye sayansi ya ubongo Vol 02, ambapo ubongo unaposikia tu biti, hulikadiria kwa namna ya mapigo yake, na kwa kuwa hili biti linaenda likiongeza sauti na kupunguza upishano au ‘’interval’’, ubongo tayari hutambua kuwa kuna tukio kubwa linaenda kutokea karibuni. Pia mabiti ambayo hukosa baadhi ya mawimbi ya asili katika sauti, unaweza yaita ‘’Suspended na augmented chords’’, hutengeneza hisia za kutisha na hamaki.
Swali la Muhimu watu wa ‘’Magic’’ huwezaje kutumia ala hizi. Hawa watu mara zote hutumia Ngoma, Na ala zingine nyingi. Nilipokuwa mdogo kijijini kwetu, nilikuwa nikisia sana usiku maeneo ya karibu, wakipiga ngoma zilizoitwa, ‘’ngoma za mashetani’’. Mtaa wetu ulizungukwa na waganga watatu, Sikuwahi elewa ngoma hizi. Maana hazikuwa na utaratibu wa sauti za kawaida za muziki, lakini nilipokuja kusoma haswa, ndipo nilipogundua mbinu hii ya muziki wa mabiti ambayo, huwa hayaeleweki kirahisi, lakini huwa yanauweka ubongo katika mazingira tatanishi. Unaweza rejea sehemu ya Muziki katika Vol 02 kuelewa namna mapigo haya ya Ngoma, ambazo hupigwa kwa mabiti mengi ‘’polyrhythms’’ namna hutengeneza sitofahamu, na hisia za mshtuko ‘’syncopation’’. Ambapo kwa mtazamaji humpa burudani, lakini kwa mhanga humpa wasiwasi.
Hutumia maneno yasiyoeleweka au fahamika. Mbinu hii hutumiwa sana na waganga wa kienyeji, na pia hata wasanii wengine wa magic. Mbinu hii hulenga katika kubumbuwaza ubongo zaidi katika sehemu za ubongo wa pembeni; zinazohusiana na kuelewa lugha na maneno, kama ulivyochanganywa ubongo wa mbele na kati, kwa usanii wa mfumo wa kuona na umakini. Ubongo hauwezi kukumbuka maneno yasiyoeleweka ni lugha gani? Au Nyimbo zisizojulikana ni za namna gani? Kushindwa huku kwa utengenezaji wa kumbukumbu, huzuia kabisa uwezo wa kutafakari katika sehemu ya mbele ya ubongo. Nakumbuka Biblia inasema kuwa, ikiwa mmoja atanena kwa lugha, lazima afasiriwe na mwenzake, La sivyo, watu hawa watakuwa wapumbavu. Hiyo ni ’’ 1Kor14’’ , neno ‘’Upumbavu’’ katika Biblia hutumika kama neno la kisaikolojia linalomaanisha sifa nyingi sana. Na miongoni ni hizi zinazochochewa na huyu msanii, kwa kuwa, unaposikia maneno ya ajabu usiyoyaelewa, Ubongo huwa unakuwa ukisisimka sana kwa kutaka kujua, je yanahusu nini? Yananihusu mimi? Vipi kama ni mipango hatari? Maswali haya ndiyo huwafukuza watu waliokaribu na vikundi vinavyoongea lugha wasizozielewa mara zote. Kitendo cha kukaa kuzisikiliza, tayari ubongo wa waasikilizaji, huchochewa kuwa na hamaki ambayo, hushindwa kugundua triki kubwa zaidi tutakazoziangalia mbeleni.
Hutumia Frequency za sauti za Kukazia, Kuunguruma, Kutishia na Kushtuka shtuka. Hakuna asiyejua mbinu hii ya kuongea inayotumiwa sana na waganga wa kienyeji. Saikolojia zote za mitindo ya kuongea kwa kuunguruma au kukaza sauti, Zinamsingi mmoja tu wa Kutishia, huku zikilazimisha malengo yake. Simba anapo unguruma, hutishia na hukazia dhumuni lake. Watu hawa hutumia hizi ‘’frequency’’ kwa lengo kubwa moja, kuongeza msisimko wa sehemu ya ndani ya ubongo, katika ule mfumo wa ‘’limbic system’’, kuongeza hisia za hofu na woga, na mara zote, Hofu na Woga vinapozidi, Ubongo wa mbele hupungua kabisa ufanisi. Hisia mara zote hukinzana na uwezo wa kufikiri. wengi ni mashahidi kwa hili, kwa namna ambavyo wanapokuwa na mihemko mikubwa ya hisia, hufanya mengi sana wasiyoyategemea. Kuna sehemu katika ubongo inaitwa ‘’locus cerelus’’, hii huzalisha kemikali zinazoitwa ‘’norepinephrine’’ , hizi husisimua mfumo mzima wa Hofu, na hapa mtu, huwa anahema juu juu, mapigo huongezeka, jasho humtoka, n.k. sehemu hii huchochewa na mfumo wa hisia ‘’limbic system’’, ambayo huwa ikichochewa kwa sauti hizi za kuunguruma, kumbuka lengo hasa, ni kuua sehemu za mbele za ubongo, mbeleni nitaonesha kiundani zaidi na triki hatari zaidi.
Hutumia Sauti za asili yaani wadudu, za ndege ndege, Bundi, na Utulivu. Ubongo ukisikia sauti Fulani tu za wadudu, hujua kuwa upo katika mazingira hatarishi sana, au ya porini sana. Hii ni kwa kuwa, wadudu hawa na ndegendege huwezi wasikia kwenye makazi mengi ya watu. Kumbuka Ubongo umezoeshwa kutambua sehemu yasipo makazi ya watu, ni sehemu hatari. Hivyo kwa namna yoyote Ubongo lazima utaongeza hofu, na kama ilivyokuwa kwa sehemu ya juu, hofu huathiri kabisa uwezo wa akili. Kwa upande wa sauti za Bundi, mara nyingi hapa triki huwa haijalenga fiziolojia, huwa imelenga zaidi saikolojia kama tutakavyoangalia mbeleni kidogo.
Sauti nyingi za Juu za Kucheka. Magicians wote huelewa nguvu za hii mbinu ya sauti za juu za kucheka. Mara nyingi wahanga wa wasanii hawa wanapokuwa wakiwa na Hofu kubwa sana, Sauti ya Kicheko, huongeza maradufu hisia za hofu. Hii ni kwasababu kubwa sana ya kisaikolojia, siku zote Ubongo unapokuwa unahofu, huwa unaficha hisia zake, ubongo haupendi kuonekana kuwa unaogopa. Sasa basi, kitendo cha kuchekwa, kinamaanisha kuwa, Ubongo unachokificha, tayari kinaonekana. Na hapa sasa, mtu hupata hisia za kujidharau, mashaka huongezeka , na hii humfanya kuwa muwazi zaidi kuzisema hisia zake na hata siri zake. mbinu hii inafanana na mbinu ile Unapoonesha kuigiza hisia za mtu ambaye hajazionesha, unajaribu kumtengenzea hisia za udhaifu zaidi, ni kama mtoto anayeanguka na kisha ukamcheka, uchungu wake huongezeka marazaidi ukilinganisha na asipoonekana.
Mfumo Wa Harufu
Katika sanaa za mazingaombwe, harufu huwa hazina triki nyingi zaidi ya moja tu ya matumizi ya poda ‘’powder’’, ambazo hizi zinapotumika huongeza uzubaifu ‘’altered consciousness’’. Kuna poda au powder nyingi sana ambazo huchochea hisia za taswira feki, kitaalamu pia huitwa ‘’hallucinatory drugs or powders’’. Mara nyingi hizi hutumiwa na waganga wa kienyeji na vikundi vya washirikina, wao hujipulizia hizi poda au vumbi, Na nyingi ya hizi vumbi hupelekea hali za kuona, kwa Kiswahili cha kisasa ‘’mawenge mawenge’’, au sitofahamu, nilieleza katika sehemu inayoitwa ‘’striatum’’ katika ubongo kuwa, dawa zote hulenga sehemu zile, na madhara yake huwa ni kuharibu uchakataji wa taswira, na mtu huwa na msisimko wa taarifa yoyote ya taswira anayoiona, na pia huwa na tafsiri feki zaidi mara nyingi.
Mara nyingine dawa hizi huwa wakizipaka usoni kama mapoda ‘’powders’’ za rangi rangi. Na mara nyingine huzipulizia kama Ubani. Inashangaza sana kuwa wengi hutumia sana Ubani. Na huamini kuwa, huwa zinakaribisha mapepo, Kumbe wanasahau, Ubani una kemikali hizi ‘’hallucinatory powders’’ ambazo zinaweza kutengeneza taswira feki kichwani. Sasa hapo ndipo utaelewa nguvu ya fiziolojia inapoungana na saikolojia. Ubani huweza Kuua Mbu. Si kweli kuwa huwaua mbu, Huwalevya mbu. mbu hupoteza fahamu na kuanguka. Na ndivyo ilivyo kwa mfumo wa fahamu, huwa umelevywa, na huwa kama mtu aliyetumia madawa ya kulevya, huona vitu visivyopo.
To be continued..






Join the conversation