Wanavyologa Wachawi ‘’Magical Causality
Wanavyologa Wachawi ‘’Magical Causality’’
Hili huwa ni miongoni mwa maswali makubwa sana ambayo watu hutamani kujua kuhusiana na soshiolojia, ya elimu za kichawi. Wachawi wanawezaje katika ulimwengu wao uliojikita zaidi kiroho, Kuwa Na uwezo wa kuathiri watu na vitu katika hali za kimwili. Lakini sayansi hiyo zaidi nitaielezea mbeleni tutakapoanza kuangalia kisayansi zaidi uchawi. Katika sehemu hii ya soshiolojia mtu anapaswa kutambua kuwa, wachawi hutengenezea hali za kibinadamu kwa vitu vinavyowazunguka. Hii ni sawa na kusema, anaweza kumchukua mdoli, na kisha kumwita kwa jina la mtu Fulani, na kumlaani huyo mtu. Hiki kitendo cha kutumia watu kwa vitu huitwa ‘’Personification’’.
Kumbuka pia kuwa wachawi, kwa asili huwa na msingi wa falsafa inayoitwa ‘’Animism’’. Hii falsafa hujikita katika kuamini kuwa kila kitu kina hisia au sifa za kibinadamu. Au pia unaweza kusema kuwa, huamini kuwa kila kitu kinaweza kuwa kama kibinadamu. Kwa mantiki hii, maelezo ya juu ni mfananisho tu wa mtu na kitu. Kuelewa zaidi hili, hebu tuangalie sheria za msingi za utendaji wa kichawi.
Sheria za Utendaji wa Kichawi ‘’Laws of Sympathy and Magic’’
Kazi kubwa iliyofanywa kuanzia na mtaalamu E.B.Tylor, na wengineo, waligundua sheria za utendaji wa namna zote za kichawi, sheria zinazoitwa ‘’laws of sympathy’’. sheria hizi huwa na namna kuu tatu, ambazo zote ni sheria za utendaji wa kichawi.
Sheria za Migusano (Laws of Contagity).
Sheria hizi husema kuwa, vitu vilivyogusana, vitaendelea kuwa na matokeo ya kugusana kwa muda wote. Hizi sheria huwa na maana hii, kama mtu atashika kitu Fulani, mfano ameshika chupa ya soda. Baada ya kumaliza kunywa ile chupa akaitupa, Basi mchawi akiichukua ile chupa, Anaweza kumfikia huyu mtu aliyekuwa akiitumia. Msingi ni kuwa, kama aliishika mara ya kwanza, basi nafsi yake bado itaendelea kuhusiana na hii chupa. Na watu hawa, wanapochukua nywele za mtu, nyayo zake, nguo zake, n.k. hulenga utendaji kupitia sheria hii.
Neno ‘’contagion’’, unaweza pia liita kama ‘’contact’’, kwa hiyo kwa wachawi, migusano huwa haiishi baada ya vitu kuachana. Na pia nafsi ya mtu huendelea kuwepo kwa vitu alivyovigusa. Msomi wa kawaida hawezi kuelewa kwanini mwanasayansi wa anga ‘’Gregg barden’’ katika vitabu vyake anahamasisha tafiti ya ‘’DNA-Phantom effect’’ kuonesha kuwa, DNA huendelea kuwa na matokeo katika chembechembe za mwanga zinazoitwa ‘’photons’’, zilizopo kila mahali kwenye mwanga. ‘’ Huyu bwana nadharia yake inapendwa sana na wafuasi wa sanaa za mashariki. Ambazo ndani yake kuna misingi ya Imani hizi za kichawi, au ‘’laws of contagity’’.
Sheria za mifanano (Laws of Similarity).
Sheria hizi hulenga kuwa, vitu vinavyofanana, huleta matokeo ya kufanana. Mfano mzuri ni kuwa, kama ambavyo ukame huambatana na joto, basi unaweza kuroga mvua isinyeshe kwa kutumia moto. Mchawi anaweza kutumia maji kutengeneza mazingira ya mvua. Hii sheria pia hutumiwa kwa waganga. Kama mtu angehitaji mtoto kwa mchawi au mganga, basi mganga angempatia Tunda alile kama kielelezo cha mtoto. Kama mtu angehitaji chochote kile Angepewa kitu chenye kufanania ajenda yake. Hii ni sheria ya pili ya uchawi.
Sheria za ukinzani (Laws of Opposition).
Hizi sheria hufanana na sheria za mfanano au ‘’laws of similarity’’. tofauti pekee ni kuwa, huku mchawi anaweza kutumia kitu kuelekeza upinzani wake dhidi ya matakwa yake. Mchawi angeweza kutumia kisu, kuelekeza ukinzani wake dhidi ya uhai. Mchawi angeweza kuelekeza matumizi ya kupasua nazi, Kumaanisha kupasua kitu Fulani katika uhai wa mwingine. Hii ni sheria kuu ya tatu ya utendaji wa kichawi.
Vigezo vya sheria hizi. Ili sheria hizi zifanye kazi, lazima kigezo cha kwanza kitimie, ambacho ni kutumia vitu, kumaanisha watu. Hivyo, maombi yote ‘’prayers’’ na ibada za wachawi, ambazo huelekea kuomba mahitaji yao, hutimizwa kwa namna hii.
Part 2
Mapepo na Majini.
Tumeshaona namna wachawi hufananisha vitu Namna ambavyo huvilaani au kuvinenea. Lakini kiundani zaidi, nini hasa hutokea, soshiolojia huamini ni kupitia matumizi ya yale mapepo ‘’spirits’’, ambayo mchawi huwa akiyamiliki. Haya mapepo ambayo mchawi huyatumia katika dhumuni lake, hutambulika pia kwa nukuu zingine kama ‘’majini’’. na majini hasa huwa ni mapepo yaliyohuru ‘’free spirits’’. haya pia hutambuliwa kwa matokeo ambayo huwa wakiyasababisha. Mapepo haya huru, huwa na majina kadha wa kadha kutokana na matatizo wanayoyasababisha, yapo yanayotambulika kwa kusababisha Homa, kuna ya kifo, kuna ya kuharisha, kuna ya kila aina ya matatizo. Mapepo haya huwa na majina yao ambayo waganga na wachawi huwa wakiyatamka sana, kuwaita waje kuwaomba matakwa yao. Na huwa wakiyaita kwa majina ya Watoto wa kifalme au wafalme, huwaita ‘’prince’’ na ‘’princess’’ wa maeneo mbalimbali. Na baada ya kuwaita, huwasiliana nao katika namna ya kialama, na pia namna za kuwehuka kwa kuwa na pepo kichwani ‘’possesed’’. hapo huwaomba shida zao, na kuwatuma kwa vielelezo vile vya sheria kuu za utendaji wa kichawi.
Uelekezaji wa Mawazo kwa Mchawi. Hili ni lengo ambalo mchawi hufundishwa namna ya kulikamilisha kupitia ibada zake. Kuna aina mbili za mitindo ya ibada, kuna zinazohusisha lugha ‘’verbal’’ na zisizotumia sana lugha ‘’non-verbal’’. Wanaotumia lugha Mfano mzuri kabisa ni ‘’Spell’’, ambazo mchawi baada ya kuandaa mchanganyo wake, au formula, Huanza kunenea sasa ili kutengeneza au kuelekeza Mawazo yake katika kuchukuliwa au kuzungumza na mapepo. Mara nyingi huambatana pia na nyimbo ambazo hupigwa kiutaalamu kabisa. Kwa upande wa uchawi usio wa maneno ‘’non-verbal’’, hawa hutumia sana alama. Hawa hutumia sana vielelezo vya kimatendo, hutengeneza maumbile mbalimbali kumaanisha mawasiliano na miungu yao. Hucheza wakati kadhaa. Na mara nyingi hawa pia huusisha tamaduni za kichawi kama za meditation za mashariki. hata hivyo huwa zikichangamana kwa kiwango kadhaa. Katika uchawi wa matumizi ya maneno, pia huwa kuna wakati wakitumia kidogo alama. na hivyo hivyo, kwa wanaotumia alama, hutumia pia na lugha. Sheria zao zote hufanana katika utendaji, na pia huusisha matendo ya namna za kufanana ya kiibada, kama vile utoaji wa kafara. Ambazo mara nyingi sana wanasoshiolojia wamenukuu kuwa zamani, zilikuwa zikihusiana sana na utoaji wa kafara za Watoto. zote msingi wake huanzia katika Imani ya kuamini uchawi na sheria zake.
Sayansi Ya Sanaa Za Uchawi, Mazingaombwe Na Meditation
Utangulizi
Katika sura iliyopita tumetazama misingi ya sanaa za kichawi. Hasa zaidi katika namna wachawi walivyo, namna wanavyofanya uchawi wao, Sheria kuu zinazoongoza matendo yao, Na tumetazama upana wa elimu za soshiolojia za uchawi na sanaa zake zote za kufanania. Katika sehemu hii, mtazamo unabadilika kidogo. Huku tunaangalia sayansi ya ndani kabisa ya misingi inayoendesha utendaji wa kichawi. Sehemu hii inalenga zaidi kuonesha namna uchawi unavyoweza kuwa na nguvu sana katika akili za watu. Na hasa katika nyakati hizi.
Pamoja na kuwa uchambuzi wa mada hii unahusisha sana sayansi. Lakini lengo hasa kubwa ni kutazama kiini cha nguvu za uchawi katika Maisha ya watu. pia sehemu hii inahusisha makisio bora kabisa ya kisayansi ‘’most probable hypothesis’’, kuelezea maeneo ambayo yana viwango vya utata kwa wengi wa wataalamu. Katika sehemu ifuatayo tutaangalia sehemu za msingi kabisa za kuzizingatia katika kujifunza misingi ya utendaji wa sanaa za kichawi, mazingaombwe, uganga na mbinu zote za namna hii ya kishirikina.
Uchawi Na Ubongo
Msingi mkubwa kabisa wa sanaa zote za uchawi ni ubongo. Uchawi ijapokuwa kwa wengi huonekana kama vile ni sanaa inayohusiana na matokeo ya moja kwa moja ya fizikia ya utendaji wa vitu kwa nje, Lakini uhalisia wa sanaa zote za uchawi umejikita zaidi katika utendaji katika ubongo wa mchawi, na wanaomzunguka. Unaweza kulielewa hili vizuri kwa kuzingatia baadhi ya vitu. Ushawahi ona Daraja au jengo limewahi jengwa kwa muujiza wa kichawi? Umeshawahi ona gari au Barabara imetengenezwa kwa uchawi? Lakini wengi huamini kwa uchawi watu huumwa! Watu hufa! Kuna miaka karibia elfu nne imepita tangia nukuu zianze kunukuliwa katika maktaba za dunia. Na hata maktaba kubwa kama ya Alexandria ilipochomwa na warumi, na kupoteza maelfu ya vitabu vya historia. Bado dunia haikuwahi pungukiwa rekodi za historia. Na katika historia zote hizo, hakuna hata moja inayoonesha kuwa kuna utafiti umewahi fanywa, wa kumtazama mchawi akipita katika ukuta au nyumba iliyofungwa mlango, tena bila kuharibu hata kidogo, na akatoka vizuri kabisa, asichukue hata senti ndogo ijapokuwa naye anashida ya pesa. Hakuna tafiti yoyote ile. Hata leo ambapo tuna wanasayansi maelfu wachawi, na tena hutumia uchawi wao wanapohitajika kuonesha mbinu za kichawi ‘’magic’’, huwa wanaweza triki za ubongo, ila sio fizikia ya vitu.
Mtazamo Mpana. Mjadala wa sanaa za kichawi huwa ni mgumu sana katika viwanja vya fizikia. Kubadilisha kilogramu 67 tu za uzito kuwa nishati inayoweza pita popote, Hupelekea mlipuko wa nishati sawa na yale mabomu ya nyuklia yaliyopigwa na marekani kuelekea japani miji ya Hiroshima na Nagasaki. Hivyo kuamini mchawi huwa anasafiri na kilo zake za uzito 50 au 60 za uzito akibadilika na kuwa mithili ya nishati, kama filamu nyingi zinavyodanganya wengi kuwa mchawi anaweza safiri na mwili wake akaenda popote, Huo ni uongo, na ni matokeo ya kutojua hasa namna uchawi wenyewe ulivyo kama tulivyoona katika sura iliyopita.
Mchawi kupaa kama ambavyo wengi wa wachawi huona, au huonekana, au huigiza, au huigizwa, au huaminiwa kuwa hupaa hewani, yote haya ni matokeo katika ubongo, na sio katika fizikia ya ulimwengu. Hii ni rahisi sana kueleweka. Unaweza kumkataa baba yako, ila huwezi kukataa kuwa yeye ndiye baba yako. Kwa kuwa, hauna namna ya kupingana na DNA zake ndani yako. Kushindana na ukweli huu, itabidi ujiumbe tena upya, ujiue kwanza, halafu utafute sheria zako, aidha DNA, cells, n.k. unaweza kataa kuwa Mungu hayupo, sawa. Ila huwezi kataa kuwa sote tunafata sheria zake za asili. Sheria za Gravity, sheria za fiziolojia, Sheria za chemisty, sheria za jiografia, N.k. hii hoja inalenga kuonesha kuwa, Mchawi kama binadamu hawezi kushindana na sheria za Mungu wake, zinazomzuia kupaa, Mpaka Mungu wake mwenyewe atakapomuamuru.
Ukiumba gari unaweza libadili likawa ndege. Elia kupaa mbinguni iliwezekana kwa mapenzi ya Mungu mwenyewe, Yesu kupaa iliwezekana kwa kuwa yeye ndiye aliyeumba sheria za gravity. Kumbuka mwanafunzi wa kawaida anaweza asielewe kuwa, sheria zote za asili ni tabia tu za ulimwengu. Na sio mikataba. Spidi ya mwanga wa jua inaweza badilika, lakini hakuna anayejua kwanini haibadiliki, mfano mzuri, nguvu ambayo ungetumia mwezini kupaa, ni ndogo gawanya kwa sita ya ambayo ungetumia duniani. Hivyo ni ujinga kuamini kuwa Mungu sio muumbaji. Ila ni ujinga zaidi kuamini kuwa mchawi anapaa. Hii ni kwa kuwa yeye ni matokeo ya uumbaji, na tena anapingana na muumbaji. Triki Za Uchawi Katika Ubongo. wachawi huwa wakifuata baadhi ya vitu ambavyo, huwafanya kuwa na uzoefu wote ambao huwa wanakuwa nao kipindi kizima wanapokuwa katika shuguli zao. Triki hizi tunazigawanya tena katika makundi makuu mawili, triki za kifiziolojia na triki za kisaikolojia.
Kiini Cha Fiziolojia Ya Uchawi Shoo Hypothesis
Kiini cha fiziolojia ya uchawi ni kutenganisha, mfumo wa utambuzi na hisia binafsi za umimi wa ubongo, na mfumo wa ubongo wa kupokea na kuchakata taarifa za nje na za ndani. Yaani, Ubongo huwa na sehemu kuu mbili unaweza zigawanya katika kazi. Kuna Sehemu kubwa zaidi ya ubongo, nazungumzia sehemu zote za nyuma, sehemu za pembeni, sehemu kubwa ya kati, sehemu nyingi za ndani, na mfumo wote wa uti wa mgongo.
Sehemu hizi zote huusiana na kazi za kuchakata taarifa zilizoufikia ubongo, toka mazingira ya nje, kama vile taswira, sauti za vitu, harufu, kumbukumbu, lakini pia taarifa za ndani, kama uwepo wa maji, uwepo wa chakula au sukari, mzunguko wa damu, mapigo ya moyo, utendaji wa mapafu, viungo vya mwili kama miguu, mikono, n.k. kumbuka hata katika picha ya mwonekano wa nje wa ubongo, utaona sehemu kubwa kabisa ya ubongo, huitwa ‘’association cortex’’, au sehemu ambazo zinahusiana na kutafakari taarifa kwa kuhusianisha na taarifa zingine, mfano, ninapomuona mdogo wangu, kupitia mwonekano wake, huja taarifa kuhusiana pia na harufu yake, maneno yake, sauti yake, hisia zake, n.k. hivyo sehemu hii yote kubwa ya ubongo, huusiana zaidi na taarifa za mazingira ya ndani ya mtu na nje yake.
Na ya pili, ambayo ni Sehemu ndogo iliyobakia ya ubongo, ambayo hii sehemu nimekwisha ionesha kama ndiyo sehemu ambayo mfumo mzima sasa wa utambuzi, uamuzi binafsi, tabia, na kila kitu kinachohusiana na utambulisho binafsi sasa wa mtu, ndiyo hupatikana. Sehemu hii ni kasehemu ka mbele kalikoungana na sehemu kadhaa za ndani, tazama picha chini.
Katika hii picha, lengo ni kutambua kuwa, mfumo wa utambuzi, uamuzi na hisia binafsi za umimi, ni kama asilimia 25% tu ya mfumo wote wa fahamu. kutambua hili ni muhimu sana, kwasababu linaonesha namna ambavyo sehemu kubwa ya ubongo, huusika zaidi na uchakataji wa taarifa za kuhusiana na mtu binafsi. na sehemu hii ndogo, ndiyo huwa baba wa mwili wote, yeye ndiye anabajeti nzima ya familia. Uchawi hulenga kutenganisha sehemu hizi mbili, na kufanya sehemu ya makao makuu kutokuwa na mzigo wa taarifa za sehemu zingine za ubongo. yaani kama Treni litenganishwe na mabehewa. Au kama baba anayesaliti familia yake, nakuwa na mzigo mwepesi sana, na anaweza akawa ni mtu mwenye anasa sana. Lakini ukweli ni kuwa, huwa hadumu. Msingi wote wa sanaa hizi umejikita katika kutenganisha mfumo wa ubongo unaohusiana na hisia binafsi na motisha za mtu, dhidi ya mfumo wote wa ubongo unaohusiana na uchakataji wa taarifa za nje na ndani ya mwili.
Lengo Kuu La Kiini Cha Fiziolojia Ya Uchawi
Lengo kubwa la kutenganisha mifumo hii miwili ni dogo sana. Kuondoa uhalisia wa tafsiri za ubongo wa mtu. Nakumbuka Biblia inavyosema ‘’shetani ni mwongo, na baba wa huo uongo’’, kweli hii triki ni ya kisayansi sana. Yaani unapotenganisha kichwa cha Fuso na trela lake, halafu unamwambia dereva, piga mwendo leo gari lina spidi sana, tutakuwa wakwanza kufika, sisi ndio mabingwa, Hiki ndicho kielelezo cha kinachotokea hapa katika ubongo.
Maisha yamejawa na stress, za ndani ya mwili, na nje ya mwili. Taarifa za kuumiza mara zote ni nyingi zaidi ya taarifa za kufurahisha. Maumivu yote msingi wake ni taarifa hizi, za ndani ya mwili, na taarifa za nje ya mwili. Kama ambavyo mwasisi wa dini ya Buddha, bwana Siddhart alivyowahi kuandika, ‘’matatizo katika Maisha ni kama matawi, na mizizi ndizo tamaa, uking’oa mizizi, basi hakuna matatizo’’. msingi wa falsafa hii moja kwa moja unafanania na hii sheria, kama mtu atachukulia tamaa kama kila taarifa isiyompendeza baada ya kushindwa kuimudu. Kila mtu anatamani Maisha mazuri, hivyo, kukataa tamaa mbaya, hakupaswi kuwa kupitia kukata kila mfumo wa kutamani. maana kuna tamaa ni za muhimu kwa Maisha. je ni vyema mwanaume kutomtamani mkewe, Je ni vema mwanafunzi kutotamani kufaulu.
Wachawi huwa na mbinu ya kutenganisha huu mfumo wa fahamu, toka sehemu ambayo ungepaswa kupata fahamu. Msomaji unaona maandishi ya hiki kitabu, kwa kuwa kuna taarifa zimetoka katika sehemu za ubongo wa nyuma, zikipita sehemu za kati na pembeni kuchakata kwa Pamoja maana ya haya maneno, na mwishowe sehemu ya mbele inayohusiana sasa na wewe, ndiyo imetengeneza logic au kuelewa kiundani na kukubali msingi wa maneno haya. Sasa basi ikiwa tutacheza na huu mfumo, maana yake ni kuwa, unaweza kuwa unaangalia, Lakini hauoni. Unaweza kuwa unasikia, lakini hausikilizi. Na kibaya zaidi ni kuwa, sehemu ya ubongo ya kutengeneza maana binafsi za Maisha, iko huru ikiwa inaelea elea kwa kukosa mfumo wake wa kupata taarifa. Na hapa ndipo shida inapoanzia.
Kitaalamu kuna maneno mengi sana yanayoelezea hii hali ya sehemu za ubongo wa mbele na ndani, mfumo wa utambuzi na uamuzi, kuwa ukielea elea bila kujishikilia na mfumo wa kupokea taarifa, wengine hutumia neno ‘’altered states of consciousness’’. Mtu anapokuwa katika hii hali, huwa anakuwa katika hatari kubwa sana ya kuwa na taarifa zisizo sahihi ‘’Delusions’’, katika teknolojia ya Ubongo, wanaamini kuwa, karibuni wataweza kuwa na namna za hata kumuingizia mtu katika hali hii, kumbukumbu za uongo ‘’false memories’’, maana hii ni kama ule mfano wa awali, kichwa cha trela kilicho huru, ni rahisi sana kukipachikia trela lingine lisilo lake. Wachawi kabla hatujaangalia kuwa huwa wanafanyaje baada ya kufikia hatua hii, ni muhimu kuelewa namna ambavyo hujichochea zaidi, ili hali hii iwe na matokeo makubwa.
To be continued...







Join the conversation