Jipatie maarifa kutoka vitabu bora vilivyoandikwa na Dr Brighton shoo kuusu imani, sayansi, afya, teknolojia, asili, malezi, saikolojia na mazingira

KWANINI SIPENDI SUKARI

 SUKARI ZA MIWA NA SODA ‘’fructose’’

Kama kuna sukari inayotumika zaidi ya uhitaji wake ndani ya miili ya watu, basi ni sukari ya muwa ‘’cane sugar’’. Sukari hii hutumika sana kutokana na tabia yake ya utamu mkubwa sana, inapofika katika ulimi. Watu wengi huitumia sana sukari hii katika utengenezaji wa juisi, biskuti, keki, chai, huichanganya kwenye maziwa, huiweka kwenye bidhaa nyingi sana za kisasa. Matumizi yake huwa makubwa sana kutokana na tabia yake ya utamu.

Lakini swali la msingi huja, je, inahitajika katika mwili katika namna inavyotumika? Au inatumika tu kwa kuwa ni tamu, na watu husukumwa kuitumia zaidi?

Kwa wataalamu wa afya wote jibu litakuwa ni hoja ya pili. Watu huitumia sana sukari kwa kuwa huwa na msisimko mkubwa katika ubongo, wa utamu. Na hivyo watu huvutwa kutumia zaidi bidhaa yenye sukari hii, na hiyo tayari ni sababu ya msingi sana katika soko, maana kadri unavyoitumia sukari hii katika bidhaa zako, tayari unawavuta watumiaji wengi zaidi.

Marazote kabla ya kuchambua hoja yoyote kisayansi, ni muhimu kutambua asili inasema nini kuhusu jambo hilo. Kwa upande wa asili, kuna kiwango kidogo sana cha sukari hii. mtu anayekula muwa mita moja, analingana na mtu anayetumia kijiko kimoja tu cha chai cha sukari. Bidhaa mbalimbali, kama soda kadha wa kadha, huwa na wastani wa sukari zenye vijiko karibia vijiko 10. Na hivyo mnywaji wa chupa moja tu wa bidhaa hizi, huwa sawa na mtu ambaye angekula muwa mita kumi, jambo ambalo lisingewezekana.

Asili huonyesha kuwa ipo kinyume na matumizi makubwa ya bidhaa hizi zenye sukari nyingi, maana asili haina vitu vyenye sukari nyingi sana kwa kiasi hiki, na tena, kwa kiwango cha sukari iliyopeke yake bila muunganiko na chembechembe zingine, kama ilivyo kwa bidhaa kama asali, au matunda ya tende, ambayo huwa na balansi nzuri sana ya sukari.

Nini madhara ya sukari hii ‘’Fructose’’

Huitajika kidogo sana katika mwili, na mwili huweza kumudu kiwango chake kidogo kama kilivyo katika matunda bila kuleta madhara. Lakini kiwango kikubwa kupita kiasi cha sukari hizi kama kinavyotumika katika bidhaa hizi za kibiashara, huwa na madhara katika namna zifuatazo.

Kwanza ni muhimu kutambua kuwa, hizi ‘’fructose’’ hutumika kwa kuwa ni tamu sana, ni tamu mara nyingi sana zaidi ya Glucose. Na ndiyo maana watu huwa hawatengenezi keki, biskuti, au soda, au maandazi na kisha wakaweka Glucose! Hii ni kwa kuwa, glucose sio tamu sana, na pia, Glucose haina uraibu ‘’addiction’’, mtu hawezi akakwambia kuwa kila akiona muhogo, au muhindi, anachanganyikiwa! Hii ni kwa kuwa, glucose huwa haina uraibu.

Glucose katika ubongo huenda katika sehemu inayoitwa ‘’Basal ganglia’’, ambayo huusiana na matumizi ya misuli, na miondoko, na hivyo mtu anavyoitumia, huwa na nishati ambayo husisimua sana ufanyaji kazi. Lakini mtu anapotumia ‘’fructose’’, mfano iliyopo katika keki, hii huenda katika sehemu ya ubongo inayoitwa ‘’nucleus accumbens’’, au ‘’ventral striatum’’, na huko huchochea kuzalisha homoni za msisimko zinazoitwa ‘’dopamine’’, ambazo huchochea sana hamu ya kula na kula zaidi ‘’sweet craving’’, na sehemu hii ndiyo hata madawa ya uraibu mengi sana huenda kama ‘’nicotine’’, na ‘’heroin’’, na hii ndiyo sababu watumiaji wa bidhaa hizi za sukari, huwa ni vigumu sana kuacha kuzitumia bidhaa hizi.

Fructose inapoingia katika mwili, huenda katika eneo moja tu, katika ini. Tofauti kabisa na ‘’glucose’’, ambayo huenda katika seli zote za mwili. Na hii ni ishara ya kwanza kabisa ya kuwa, chembechembe hizi za ‘’fructose’’ ambazo mdomoni zilionekana kuwa ni tamu, mwili huziona ni kama ‘’Sumu’’, na ndiyo maana baadhi husema, chembechembe za fructose na ‘’ethanol’’ zilizopo katika pombe, ndizo chembechembe pekee ambazo mwili huwa na uwezo kidogo sana ‘’limited’’, wa kuzichakata, ni kama tuziite ‘’vestigial products’’, yaani tunao uwezo kidogo sana wa kuzichakata.

Sasa basi, kiwango kikubwa sana cha ‘’fructose’’ kama mnywaji anavyoitumia katika bidhaa hizi, hubadilishwa yote katika ini na kutengeneza mafuta. Mafuta haya hujaa katika ini, na huitwa hii hali ‘’fatty liver’’, na hii huwekwa katika kundi kitaalamu linaloitwa ‘’Non-alcoholic fatty liver’’, yaani, mtu hanywi pombe, lakini ini lake limejaa mafuta, maana pombe ndiyo huchochea zaidi ini kujaa mafuta, na kunenepa. Na ini kunenepa kwa mafuta, ndiyo msingi wa matatizo yote ya kufeli kwa mifumo ya utendaji ya miili ya watu, au ‘’metabolic syndromes’’.

Kadri mnywaji anavyozidi kutumia bidhaa hizi, ndivyo mafuta mengi zaidi yanavyojaa katika ini lake, na katika mishipa yake ya damu. Mafuta yanavyozidi kujaa katika mishipa ya damu, huvunjwa na seli za kinga zinazoitwa ‘’macrophages’’, ambao kadri wanavyoyavunja mafuta, huyapelekea kuunda mabaki au ‘’plaques’’, ambazo hujishikisha katika ukuta wa damu, na kuupelekea mshipa wa damu kuwa na tundu dogo la kupitisha damu, hii tayari huchochea zaidi matatizo ya presha, na shida za moyo. Huwa pia kitaalamu inaitwa ‘’atherosclerosis’’. 

Sababu hii tayari inaweza kujibu kwanini mara zote kuanzia miaka hii ya usasa, kuanzia miaka ya 2000, matatizo ya moyo ‘’cardiovascular problems’’, ndiyo yanaongoza zaidi kuua watu, matatizo kama ‘’ischemic heart disease, stroke, na hata kisukari ambacho nacho kinauhusiano na shida za sukari hizi’’

Fructose ni maarufu sana kwa kuua mashine kadhaa za seli za nishati ‘’enzymes of mitochondria’’, mfano, huua enzymes wanaoitwa ‘’CTP1, .......’’, enzymes hawa wanaumuhimu sana katika utendaji wa sehemu hizi za seli zinazohusiana na uzalishaji wa nishati. Na hivyo sasa, kuharibu ‘’mitochondria’’, hupelekea mwili dhaifu ambao hauwezi kuchakata nishati vizuri, na hata huchochea vifo vya seli kwa kushindwa kujiendesha kisawasawa.

Fructose inapoingia katika seli za ini, hutumia zaidi nishati ya mwili katika kuvunjwa vunjwa, kuliko hata yenyewe kuzalisha nishati. Fructose hupelekea ATP nyingi sana za mwili kutumika katika kuivunja yenyewe, ili kuibadilisha kimetaboliki ije kupelekea kuzalishwa kwa chembechembe zinazoitwa ‘’acetyl-coA’’, ambazo huchochea zaidi kuundwa kwa mafuta katika chaneli inayoitwa ‘’de-novo synthesis’’. Sasa basi, kitendo hiki hupelekea kujaa kwa kiwango kikubwa sana cha chembechembe zinazoitwa ‘’AMP’’, ambazo huvunjwa zaidi na kupelekea chembechembe zingine zinazoitwa ‘’IMP’’, hizi sasa hubadilika zaidi na kuunda chumvichumvi za ‘’uric acids’’.

Hizi chumvichumvi za ‘’uric acids’’ hujaa kwenye sehemu za maungio ya mifupa ‘’joints’’, na hupelekea matatizo ya viungo ambayo kitaalamu huitwa ‘’gouts’’. Lakini pia, hizi chumvichumvi hupelekea matatizo makubwa sana ya figo, hii ni kutokana na tabia yake ya Kwenda kujikusanya katika mishipa midogo ya figo, inayofanya kazi ya kuchuja damu. Na chumvichumvi hizi kadri zinapozidi kujaa, huunda mithili ya vijiwe vidogo vinavyoitwa ‘’kidney stones’’, hizi hata bila ya kupelekea tatizo la moja kwa moja, hupelekea kuanza kufeli kwa kazi za figo, za kusafisha damu.

Ulaji wa bidhaa hizi zenye viwango vikubwa sana vya sukari, za ‘’fructose’’, kama ilivyo kwenye soda, keki, biskuti, juisi za viwandani, n.k. huambatana na kiwango kidogo sana cha kambakamba zilizomo katika vyakula, hasa vya wanga vya asili ‘’Fibers’’.

Hili ni tatizo kubwa sana kuliko wengi wanavyoweza kulitambua, kitendo cha kupungukiwa kambakamba hizi, au ‘’fibers’’, hupelekea bakteria wazuri waliomo tumboni, kukosa chakula. Hii ni kwa kuwa, wao huwa wakila hizi kambakamba, na wanapozikosa, huanza kula uteute unaoukinga utumbo ‘’mucus’’, kwa kuwa ule uteute huwa una protini zinazoitwa ‘’mucin’’, na kadri wanavyozidi kuula ule uteute, utumbo hizidi kubakia wazi, na fructose hunukuliwa na wataalamu wengi sana kuambatana na kuruhusu utumbo kupitisha vitu kutoka katika utumbo, na kuingia katika damu moja kwa moja ‘’leaky gut’’, na kupelekea mchafuko wa damu.

Kadri vimelea wanavyozidi kuushambulia uteute wa utumbo, wanaufanya kuwa hatarini sana na vichubuaji kama ‘’free radicals’’, au ‘’acidifiers’’, na hawa na wengine wote wanavyozidi kuuchubua utumbo, huufanya utumbo kuvimba, uvimbe mdogo sugu ‘’chronic inflammation’’, na huu uvimbe huzuia utumbo kuweza kufyonza vizuri virutubisho, huchochea kukua kwa saratani, kama tutakavyoona mbeleni namna saratani ya utumbo wa Colon ambavyo hutokea.

Kambakamba ‘’fibres’’ husaidia sana katika kubalansi umeng’enyaji wa vyakula vya wanga, hizi huifanya wanga Kwenda kukamilisha umeng’enywaji wake katika utumbo mdogo, chini kabisa katika utumbo. Lakini vyakula hivi vyenye sukari hukosa hizi kambakamba, maana hata ukiziweka, haziwezi kufanya kazi kama ilivyo katika vyakula vya asili.

Madhara yake ni kuwa, mtumiaji wa bidhaa hizi, kama tu ilivyo kwa mlaji wa ugali wa sembe, baada tu ya kula, wanga huvunjwa haraka sana, maana iko huru tu inaelea ‘’free’’, na baada ya kuvunjwa kwa haraka sana, hupelekea kujaa sana kwa kiwango kikubwa sana cha chembechembe za sukari za mwisho kabisa, yaani, ‘’glucose, na fructose’’, pale tu vyakula vinapokuwepo katika utumbo baada ya tumbo ‘’duodenum’’, na madhara yake ni kuwa, sukari hizi zote huenda moja kwa moja katika damu na kisha ini, kupitia chaneli ya damu inayoitwa ‘’portal circulation’’, na sukari hizi zote hubadilishwa na kuunda mafuta.

Mafuta yanayoundwa hujazana sana katika utumbo, huwa yanaitwa ‘’visceral fats’’, hupelekea kitambi ‘’obesity’’, na huchochea sana Kisukari aina ya pili ‘’Diabetes mellitus-type 2’’. Hii ni kwa kuwa, mafuta haya hupelekea kujaa kwa aina za chembechembe zake za mafuta zinazoitwa ‘’fatty acids’’, hizi chembechembe huingia katika seli, na huzuia mashine kadhaa za seli ‘’enzymes’’, kama ‘’ hexokinase 6, na Phosphofructokinase’’, ambao hawa wote, huzuia chembechembe za Glucose zisiingie ndani ya seli katika mlango wa glucose wa kuingia ndani ya seli, unaoitwa ‘’Glut4’’, hii inamaanisha kuwa homoni ya insulin tayari haiwezi kufanya kazi, na ndiyo maana watu hawa hupata shida za kisukari. Mbeleni tutaangalia kiundani zaidi namna watu hawa hupata kisukari.

Kumbuka changamoto hizi katika bidhaa hizi, huwa hazipo peke yake, huambatana na changamoto nyingine nyingi sana. Hii ni kutokana na kuwa, huwa bidhaa hizi hazina sukari peke yake, huwa pia na viwango vikubwa sana vya viongezwa vingine. ambavyo navyo, huwa na madhara kama tutakavyoviona kiundani kwa sehemu za mbele.

Kwa asili kiwango kidogo cha fructose ambazo huwepo katika matunda, hubebwa na fibres bila kupelekea madhara makubwa katika ini, na katika ubongo. kiwango kidogo katika ini hubadilishwa kimetabolikia bila kuleta changamoto yoyote ile, na kiwango kingine ambacho hushuka mpaka katika utumbo, humeng’enywa na bakteria wazuri na kuzalisha chembechembe nzuri kabisa za afya, zinazoitwa ‘’short chain fatty acids’’. Hizi huwa na manufaa katika ubongo, na katika mwili. Kiwango kidogo ambacho huenda katika ubongo, husisimua ulaji kiasi wa matunda, ili kupata virutubisho kama vitamini, madini, maji, protini, n.k. lakini matunda kwa asili pia huwa na kambakamba nyingi sana ‘’fibers’’, ambazo huifanya isiwe na changamoto kama ilivyo kwa bidhaa za kisasa.



Watumiaji wengi wa bidhaa hizi za sukari, na ambao huwapatia na Watoto wao pia, huwa na hatari sana za kushambuliwa na magonjwa ya vimelea, hasa virusi. Hii ni kwa kuwa, kiwango kikubwa cha sukari hizi, huambatana na kiwango kikubwa cha presha kama tulivyokwisha kuona katika sehemu zilizopita, hii huwa na matokeo yafuatayo.

Hupelekea figo kusisimua mfumo wake wa kupambana na ongezeko la presha ya damu, unaoitwa ‘’rennin-angiotensin-aldosterone-adh system’’ huu mfumo hupelekea mapafu kuzalisha enzymes zinazoitwa ‘’angiotensin converting enzyme, hii hupelekea sensa nyingi sana za seli zake kuwa wazi, au huitwa ‘’ace-2 receptors’’, hizi sensa sasa ndizo ambazo virusi hujishikisha. Kwa hiyo watumiaji wa bidhaa hizi, huwa na sensa nyingi zaidi za kuwakaribisha virusi kuwashambulia. Lakini pia kiwango kikubwa cha sukari hizi, huchochea vimelea kuzaliana, kwa kupata vyakula vingi, na kuwa na mfumo dhaifu wa damu wa kusafirisha seli za kinga.