SAYANSI YA HATUA KUU TATU ZA TAMAA #11
TAMAA
Sehemu hii tutaangalia hatua
kuu tatu za tamaa, na maana ya tamaa. Uchambuzi umejikita sana toka kwa
majaribu matatu ya Yesu. Msomaji usichanganyikiwe kwa kuanza na jaribu la
kwanza, kisha la tatu, na mwisho la pili. Hatua ya pili na ya tatu ya tamaa
inafanania sana, na namna nyepesi zaidi ya kuelezea ilikuwa kupitia mtindo
uliotumika, lakini hoja ya msingi unaweza ipata baada ya kusoma.
HATUA KUU TATU ZA TAMAA
kama kuna jambo lenye Nguvu
kubwa sana katika motisha ya kiumbe yeyote yule anayeitwa hai, basi ni tamaa.
Kuna wakati hata neno tamaa hutumika kumaanisha motisha! Yaani, utendaji wowote
ule wa kiumbe, huisiwa kuwa ni matokeo ya msukumo mkubwa sana wa tamaa ya huyo
kiumbe juu ya jambo hilo.
Kuna mkanganyiko mkubwa sana,
juu ya maana ya neno ‘’Tamaa’’ katika mantiki ya tamaa katika uasi, au tamaa
katika wema. Lakini hata hivyo, tofauti ya mtu anayemtamani mke wa Jirani yake awe
mkewe, na mtu anayetamani kuwa na mke kama wa Jirani yake. Imejengwa katika
kiini cha tamaa kwamba, wa kwanza, anatamani kitu ‘’ambacho ni mke wa Jirani
yake’’. wakati wa pili, anatamani hali ya kitu. ambacho ni ‘’tabia za nje au za
ndani za mke wa Jirani yake’’.
Jambo ambalo ni baya sana
kuhusu tamaa kutokana na amri ya kumi ya Mungu. kutoka kitabu cha Kutoka sura
ya 20. limejengwa zaidi katika mtazamo wa kwanza, wa kutamani kitu, kuliko
kutamani hali ya kitu. Hii ni kwa kuwa, hakuna vitu viwili duniani vinavyoweza
kufanana katika kila kitu, kwa asilimia zote 100%. Kutamani kuwa na kitu
ambacho siyo chako, lazima kutakupelekea kutaka kukichukua! Ambapo huo ndiyo
mwendelezo wa maovu mengine, kama wizi, uuaji na hata uzinifu kama ubakaji.
Mtazamo wa pili wa tamaa juu
ya hali ya kitu, huwa na changamoto ndogo kidogo. kwa kuwa, hali ya kitu
inaweza tengenezwa bila uhitaji wa kitu husika. Na hii ni kutokana na kuwa,
hali nyingi za vitu hufanana na huwa hazitegemei kitu husika. Mfano, tabia ya
ucheshi, furaha, usafi, nidhamu, n.k. zinaweza letwa na kitu chochote kile. Ni
kama vile namna ambavyo redio zote zinaweza tangaza taarifa ileile, hata kwa
sauti ileile, lakini hakuna redio mbili duniani zilizofanana kwa asilimia 100%,
hata kama zimetoka kiwanda kimoja! Kadri utakavyozichunguza kiundani zaidi,
utagundua kuna utofauti, hata kama ni katika viwango vya chembechembe za atomu.
Shida ya mtazamo wa pili,
imejengwa zaidi katika saikolojia ya mwenye tamaa. yaani, ni rahisi mtu
kutamani mjumuisho wa tabia au hali Fulani za kitu, kwa kuhusianisha na kitu
husika. mfano, mtu anatamani ucheshi, usafi, nidhamu au sifa yoyote ya mke wa
Jirani yake, kama inavyotoka kwa mke wa Jirani yake moja kwa moja. Hii
inadhihirisha kuwa, kiundani zaidi, huyu mtu bado ametamani kitu, namna
kinavyojidhirisha. Ni sawa kabisa na mtazamo wa kwanza, ila tu hapa, haijawa
kwa moja kwa moja.
TAMAA SIO MALENGO
Wengi huchanganya tamaa na
malengo. lakini hii huwa ni changamoto tu ya uelewa wa maana ya tamaa. Tamaa
lazima ihusishe dhamiri ya kutaka kuwa na kitu au hali ya kufanania na jambo la
nje na mtu binafsi. Ili isemwe ni tamaa, lazima mtu atake kuwa na kitu
anachokitaka, au hali anayoitaka, ambayo ni matokeo ya anachokiona kuwa ndicho
bora zaidi. Wengi hawajui kuwa, huwezi tamani bila kuona. Lazima uone, utake,
ndipo isemwe kuwa umetamani.
Ukija kwa malengo, Malengo
huwa hayatoki nje. Huwa ni msukumo wa maono ya ndani. Na kama yakitokana na
mtazamo wa nje, basi nayo huwa ni tamaa. Huwa napenda kusema, malengo ambayo
yanahusisha sana mipango, ni matokeo ya kutazama mazingira yako, kuyatafakari,
na kutengeneza taswira ya kuwa unataka kutengeneza nini. Mfano, nalenga au
nafikiria kujenga saloon ya nywele maana nimeona kuna wateja wengi sana eneo
hili, na ninaweza thibitisha kwa kuona hata Jirani yangu naye mwenye saloon,
hushindwa kumudu idadi kubwa sana ya wateja wa nywele. Ninapovuta taswira sasa
kuwa nimeshaijenga ilihali nipo katika mipango ya kuijenga, basi nakuwa nahamu
ya kuikamilisha. upande wa tamaa huwa kinyume kabisa, yenyewe huanza kwa kuona
saloon ya mwenzangu ikiwa na mafanikio mpaka kuzidiwa, na kisha hutoka huko
kuja kwenye mipango ya mimi kufikiria hilo kama fursa kwangu.’’
Tamaa huenda kinyume na
malengo, tamaa haina mipaka ya kuikamilisha, ila malengo yana mipaka. Nina
mipaka ya malengo ya namna yangu ya kuoa, lakini sina mipaka ya namna yangu ya
kutamani kuoa. Malengo yana kikomo kwa kuwa hutumia sana sehemu za mbele za ubongo,
katika mfumo wa ubongo unaoitwa ‘’CEN’’ au ‘’central executive network’’,
wakati tamaa hazina mipaka, na hutumia sana sehemu kadhaa za ndani na nyuma
katika ubongo, hutumia mfumo wa ubongo unaoitwa ‘’DMN’’ au ‘’default mode
network’’, mtu anayetamani anaweza zini hata akitembea, anaweza kuua ili
kukamilisha au kuiba, anaweza pia akatumia njia sahihi ila bado asiwe na nia
njema, kiufupi tamaa haitoki moja kwa moja sehemu za kufikiria katika Ubongo.
Changamoto: kuna
watu maranyingi husema, nimemwona Mwalimu mmoja anafundisha vizuri sana, na
mimi nimetamani kuwa kama yeye, Je, hiyo nayo ni tamaa mbaya?
Jibu: kwa mujibu wa Ubongo,
kama umetamani namna alivyo Mwalimu, nafasi ya ualimu, au kipawa cha ualimu,
namna ya kufundisha, kusaidia watu maarifa, hapo umetamani Hali. Na hilo halina
shida. Na kisaikolojia hapo umetamani kwa kuwa hiyo hali ipo ndani yako,
umesukumwa kuelekea asili yako. Ni kwamba umekosa neno la kutumia, umetumia
tamani, badala ya kuvutiwa.
Upande wa pili kama umetamani
nafasi ya Mwalimu huyo, umetamani wewe ndiyo ungekuwa katika nafasi yake,
umetamani wewe ndiyo ungekuwa unasikilizwa. Wewe una dhambi ya tamaa, na
inakuhatarishia afya yako ya Ubongo, na hautakuwa Mwalimu mzuri, maana huna mipaka,
na hautatenda kwa upendo, utatenda kwa ubinafsi au kwa kutaka sifa.
Kabla hatujaangalia kiini cha
sura hii, juu ya hatua kuu tatu za tamaa. Ni lazima tutambue kuwa, tamaa ndiye
adui mkubwa zaidi wa mtu. Kama kuna kila uovu ambao mtu anaweza kuutenda kwa
kutaka au kutotaka. Ambao hata yeye mwenyewe huweza kukiri kuwa hakutamani
kutenda hivyo, basi sababu ya huo uovu ni tamaa. Tamaa humlazimisha mtu kutenda
kwa kutaka, au kutotaka.
Katika mtazamo mpana zaidi
ambao sitataka kuuzungumzia zaidi katika sehemu hii, ni kuwa, hata sayansi ya
Ubongo huonyesha kuwa tamaa haina msingi katika sehemu za mbele za ubongo, au
sehemu za msingi wa akili na utambuzi wa mtu. Msukumo wa tamaa ni mpana sana,
kifalsafa zaidi, tamaa tutaiona kuwa imelenga parefu sana, zaidi ya malengo
binafsi ya mtu. Na ndiyo maana, kama kila tamaa ya mtu ingetimia, basi
tusingekuwa na Mungu mmoja leo hii duniani.
Kadri mtu anavyojifunza zaidi
kuhusu tamaa, ndivyo anavyogundua zaidi kuwa, kwanini hata Suleimani alifikisha
wanawake elfu wakumridhisha tu, au Nebukadneza alitaka kuabudiwa kama Mungu.
Leo hii vijana hutamani umaarufu, utajiri, heshima, mamlaka, kupendwa, n.k.
lakini hayo siyo malengo ya wengi wao! Unaweza gundua kuwa, wengi huwa na
melengo katika fani zao, elimu zao, vipaji vyao, n.k. ajabu ni kuwa, tamaa huwa
kubwa zaidi ya malengo.
tamaa huathiri hata uwezo wa
malengo binafsi ya mtu. Maana, mtu hutazama malengo yake, na tamaa yake
humwambia kuwa, hapo ulipo bado ni dhaifu sana. Ni kama stori ya kweli ya
Lusifa, ambapo, lengo kubwa la kipaji
chake cha uimbaji bora, lilimezwa na tamaa kubwa zaidi hata ya lengo lake,
tamaa ya kuwa Mungu. Naweza tamani kuwa mwalimu bora, na nikawa nikitembea katika
lengo langu la kuwa mwalimu bora, lakini tamaa yaweza ua lengo hili, na kuibua
hisia ya kutaka kuwa bora zaidi ya mwalimu yeyote yule anayenizunguka, au
aliyewahi kuwepo. Na hapo ndipo tatizo huanza, maana hata kwa kusemwa kuwa bora
zaidi ya wote, tamaa hupanda ngazi, ya kutaka kuwa sio tu mwalimu bora zaidi ya
wote, bali hata kuwa bora zaidi ya wenye taaluma wote.
Unaweza thibitisha hili kwa
namna ambavyo, watu walio katika ngazi bora zaidi, bado hukosa raha kwa
kutoridhika na hali zao. Mfano, Malaika mkubwa zaidi Lusifa bado hakuridhika na
nafasi yake, au mbunge, au Waziri Fulani, Pamoja na heshima ya nafasi yake,
lakini bado hajaridhia. Na hata akiwa raisi, bado utaona hisia za kutoridhika
zikiendelea kumrarua.
NAMNA TAMAA INAVYOKUUA
Unapokuwa kijana wa kiume wa
miaka 7, huwezi elewa sababu ya kaka yako wa miaka 16 kutumia hela yake yote ya
chakula kumnunulia zawadi mpenzi wake, na yeye kushinda njaa akitafuta tu
kumridhisha mpenzi wake. Ukweli ni kuwa, alipobalehe, uhalisia wa ubongo wake
ulibadilika, akapanda ngazi katika tamaa za mapenzi hatua moja zaidi ya mdogo
wake. Na sasa ubongo wake una uhalisia mpya kabisa wa anavyovipenda, hii
kitaalamu huitwa ‘’neuroplasticity’’.
Ndivyo pia ilivyo kwa tamaa,
unapoanza ngazi za chini, unaweza usielewe kwanini kuna watu wanatamani hata
waitwe Mungu, lakini kuwa makini tu usiwatukane, maana Ubongo wao umefunguka
zaidi ya wa kwako, na wanaona uhalisia tofauti na uhalisia unaouona. Na wewe
ukijaaliwa kukua, utaelewa wanachokiona. Sehemu hii tunaenda kuangalia ngazi
kuu tatu za tamaa, huku Lusifa akiwa kielelezo cha mgonjwa mkubwa, na wa kwanza
kabisa wa tamaa.
HATUA NA AINA KUU TATU ZA
TAMAA
1.Uhakika
Wa Kuishi na Chakula
Kila anayeamka na kuendelea
kupumua, ni nguvu ya chakula alichokwisha kula. Binadamu huishi kwa mkate.
Inahitaji akili kubwa sana kutambua kuwa, binadamu anaweza kuishi bila mkate,
na kama sivyo! Shetani asingemjaribu Yesu kwa kumwambia ‘’badili jiwe hilo kuwa
mkate!’’ sayansi ya Ubongo huonesha kuwa, katika mahitaji yote ya msingi ya
mwili, Ubongo huonesha kipaumbele zaidi cha motisha kwa chakula, hasa chenye
kuupa mwili nishati, kama sukari. Wanasayansi wasiolijua hili, huisi labda
mapenzi ndiyo huwa na kipaumbele zaidi, kama inavyoonekana kwa namna ambavyo
huzalisha msisimko mkubwa sana katika ubongo, lakini hawa husahau kuwa, kama
mwili usingekuwa na chakula wala mapenzi, na kuwa mhanga wa vyote mpaka mwisho,
kamwe usingechagua mapenzi mbele ya chakula. Mapenzi huwa ni baada ya chakula
katika ubongo. hivyo hitaji kubwa zaidi la asili katika ubongo ni chakula. Na
sababu ni kuwa, binadamu huishi kwa mkate.
Msingi Wa Tamaa
Unaweza jiuliza, iwapi tamaa
hapo juu. Tamaa huanzia hapa. Kwa kuwa binadamu huishi kwa chakula. Na kadri unavyoweza
kuwa na uhakika wa kula, ndivyo unakuwa na uhakika wa kuishi. Binadamu hutamani
sana kuwa na uhakika wa kuishi, kwa kuwa na uhakika wa chakula.
Sasa udhaifu ni kuwa, mwili
huweza kula chakula kwa kiasi maalumu tu, tena chakula cha siku moja tu. Huwezi
kula chakula cha leo na kesho, na kwa hivyo, kila siku kunapokucha, binadamu
hupaswa kuwaza atakula nini, Au ataishi vipi kwa lugha nyingine. Swali hili
huwa halipendwi kabisa na Ubongo, mtu kwa asili hutamani kuwa na uhakika wa
kuishi au kula, na hivyo hitimisho pekee, huwa ni kutamani kujilimbikizia ghala.
Ambapo kwa zamani za uandishi wa Injili, mfano wa Yesu humzungumzia Tajiri
mpumbavu, aliyejijazia ghala, na kisha akahisi sasa, atafurahi kwa kuwa na
uhakika wa kuishi. Kwasasa hivi watu hujilimbikizia mali au fedha katika
mabenki, wakijitengenezea furaha kwa uhakika wa Maisha.
Unaweza jiuliza kwanini asiyemsomi
au aliyemsomi, Tajiri au masikini, mwenye mamlaka au mtumwa, wote hutafuta sana
Pesa. ijapokuwa hutofautiana kidogo katika matumizi, lakini wote hushea aina
kuu ya utumiaji, kwa chakula. Masikini hutafuta hela ya kukidhi hitaji kuu
zaidi, wakati Tajiri huongeza wigo zaidi wa mahitaji.
Maana Pana Ya Jaribu La Kwanza La Yesu
Jaribu la kwanza lilikuwa
linamaanisha kuwa, kila mwanadamu hujaribiwa katika namna ambavyo ana tamaa ya
kutaka uhakika wa kuishi. Mfumo wa Maisha kwa asili, huwa hautoi uhakika wa
kuishi, na ndiyo maana kila mtu hupaswa kula kila siku, na siyo kula chakula
cha miaka Hamsini kwa mara moja, na kuwa na uhakika wa kuishi, hata kama
utatokea ukame wa chakula.
Jaribu hili ni jaribu la hatua
ya kwanza ya tamaa. Yesu anafundisha kuwa, ‘’Maisha ni zaidi Chakula, na Mwili
zaidi ya mavazi’’. Pia anasema ‘’Msiwaze mtakula nini au mtavaa nini’’ pia
anasema ‘’Msiiwazie kesho, kesho itajiwazia yenyewe’’ na Jibu lake kwa jaribu
lilikuwa ‘’Binadamu hataishi kwa mkate tu’’ Jibu hili ni la kisayansi sana,
Binadamu alipoanza kuumbwa, hakuumbwa mwili na kisha akapewa chakula, na kisha
akaanza kuishi, la hasha! Alipoumbwa mwili, alipuliziwa pumzi ya uhai, na kisha
akaanza kuishi.
Hivyo nguvu ya kwanza kabisa
ya uhai ni pumzi ya Mungu. Na baada ya Kuishi, Mungu akampatia binadamu Chakula
kama chanzo endelevu cha uhai ‘’secondary source’’. Kama mtu angeufananisha
mwili na Gari, basi Chakula ni kama Petroli. Katika wakati na jamii yangu kwa
sasa, lita moja ya petroli inayouzwa 3,203/=Tshs, inaweza lisukuma gari la gharama ya Milioni
250/=Tshs, kwa umbali Fulani, kama
kifanyavyo chakula kusukuma uhai wa mwili kwa siku kadhaa. italeta mantiki gani
mtu mwenye gari hili kutokuwa na raha, kwa kukosa uhakika wa petroli? Au hata
kulishusha kabisa thamani yake?
Lakini kama kuna ujinga mkubwa
sana, ni kuamini kuwa gari linatembea kwasababu kubwa zaidi ya Petroli. Na
kusahau kuwa, Ufundi uliogharimu maarifa na nishati nyingi sana, ndiyo sababu
kubwa. Mpaka hapa tunaweza kugundua kuwa, Shetani hakuwa mpumbavu sana wa
kutolijua hili, hata kumjaribu yesu. Ila alimjaribu kwa kuwa, alihisi naye
anaweza kuwa na tamaa kama aliyonaye yeye.
Maisha Ya Tamaa Katika Hatua Ya Kwanza
Hatua hii huchukua asilimia
karibia 80% kwa makadirio yangu ya rafu, ya watu wote. Asilimia kubwa sana yetu
ni watu wa matabaka ya chini na kati ‘’poor & middle class’’. Na katika
matabaka haya, upatikanaji wa mahitaji ya msingi kabisa, ya kuishi, ni
changamoto kubwa sana. Hili huwafanya watu kuwa ni watu wa kuwaza sana, ni
namna gani wanaweza kupata fedha za kukidhi mahitaji haya. Hasa pale hali
inapokuwa ni ngumu, au dhiki, kama ‘’Yesu alipokuwa na njaa kwa kufunga siku
40’’. Tamaa kubwa kabisa katika hatua hii huwa, nikipata kazi! Nikipata hela!
Nikivuna sana awamu hii! n.k. hisia za mtindo huu mara nyingi hujaribiwa kuhisi
kuwa, kwa kukosa mahitaji hayo, basi hakuna Maisha tena. Na hapo Shetani huwavuna wengi kama Samaki,
kwa kujifanya kuwa yeye ndiye mwenye kutoa uhakika wa Maisha. kitu ambacho si
kweli.
Lengo kubwa la Yesu ni
kuturudisha nyuma kuwa, hakuna haja ya kutamani uhakika wa Maisha. binadamu
anapaswa kujali zaidi majukumu yake, au kazi zake, na kukubaliana na kikomo cha
utendaji wake, kesho ni fumbo. Kwa kuwa na lita nyingi za petroli hakumaanishi
kuwa ndiyo uhakika wa kufika safari, Yesu alihitimisha mfano wake wa Tajiri
mpumbavu kwa kusema, ‘’Mungu akasema leo hii naichukua nafsi yako’’. Hivyo
wengi wa wanaokimbilia uhakika wa Maisha, kwa kutamani kujimbikizia mali,
hujikuta tu wakiishia pabaya. Ni vema kuwa na kiasi, kuridhika na leo, na
kuamini kuwa thamani ya Maisha ni kubwa kuliko chakula, kwa kuwa mwanzo wa uhai
haukuwa chakula, bali neno la Bwana wetu Yesu Kristo.
2. Tamaa Ya Kutawala Asili na Ulimwengu
Akili hubadilika ghafla sana
baada ya kuhisi tayari sasa nina uhakika wa kuishi kwa chakula. Binadamu huanza
kutamani sasa kuwa kichwa, na kuwafanya wengine mkia. Wasomi baadhi hutafsiri
vibaya sana ahadi ya Mungu ya ‘’ntakufanya kuwa kichwa na sio mkia!’’ Wao
huonyesha kuwa, wanaobarikiwa huwa kichwa, au nambari moja, au viongozi, na wasiobarikiwa huwa mkia, au wa mwisho au
watumwa, Hapana, Kila mtu anaweza kuwa kichwa kama alivyo na kichwa,
kutobarikiwa hulenga zaidi kutoweza kutumia kichwa, na kuwa mkia, au kutoongoza
akili yako, bila shaka kuongozwa.
Yesu alipojaribiwa na Shetani
kuwa, ‘’ Kama Ukinisujudia ntakupatia milki na falme zote za ulimwengu. Shetani
alilenga hatua ya pili ya hisia za tamaa. Wengi huwa hawajui kwanini watu
hutamani sana kuwa wafalme, maboss,
managers, machifu, viongozi, wenye ubora zaidi, nambari moja, hajawahi tokea,
n.k. Falsafa ya sayansi inatusaidia sana kuelewa hili, kadri mtu anavyokuwa wa
upekee sana, ndivyo thamani yake huongezeka zaidi, ndivyo watu wengi humhitaji
zaidi kutokana na upekee wake, ndivyo huwa na mapokeo makubwa zaidi toka kwa
watu, na ndivyo utajiri wake huongezeka zaidi. Kadri utajiri wake unavyozidi
kuongezeka, ndivyo uhakika wake wa kuishi unavyoongezeka.
Kama ukimchukua kijana
anayetamani kuwa Tajiri sana, na kisha ukawa ukimuuliza baadhi ya maswali
kuhusu sababu ya tamaa yake, Utagundua kuwa, anatamani kuwa Tajiri sana kwa
kuwa, kwa kuwa Tajiri sana atapata mengi ya mahitaji anayoyatamani, hatatumia
nguvu kubwa kupata mahitaji yake au tamaa zake, atakuwa na uwezo mkubwa wa
kujilinda dhidi ya hatari za Maisha.
wengi ambao huisi watu hupenda
kuwa maarufu au wakubwa sana kihadhi kwa kupenda sifa toka kwa watu, huwa
hawajui kuwa kupenda sifa hulenga sana uhakika wa usalama binafsi wa mtu,
kimwili na kiakili. Kama atasifiwa na wengi, maana yake, uwezo wake wengi wameuona
hauna wa kulinganisha naye ‘’yaani, upekee wake ni wa juu sana’’, pili
wanaokusifia wanakuhakikishia kuwa wanakupenda, hivyo hawatakubali uanguke.
Hizi zote zinalenga tu kumhakikishia zaidi mtu uhakika wa kuishi, kwa kujiona
ya kuwa, hayuko peke yake, au yuna nguvu nyingi.
Kwa kutamani umaarufu mkubwa
na mamlaka, watu wote hukutana juu. Ni kama kila mtu huongozwa kutamani sifa
hizo, na hivyo, anayewahi kufika huwa na wafuasi wengi wanaotamani kuvutwa
mkono. na kwakuwa kwa umaarufu na
mamlaka ni rahisi kupata marafiki wengi, wapenzi wazuri, wataalamu
wakukusapoti, wasanii wa kukuburudisha. Kila aina ya kileo cha uraibu wa akili
hupatikana juu. Mambo haya humfanya aliyejuu kuwa na nguvu kubwa sana, na hapa
sasa ndipo kiini cha tamaa huzidi kukomaa.
Yesu alitoa somo kubwa sana ya
kuwa, anayepaswa kusujudiwa ni Mungu tu, na sio mwenye nafasi yoyote ile ya
juu. Alimaanisha kuwa, kwa kuwa na mamlaka na umaarufu juu ya watu,
hakumaanishi kuwa thamani ya mtu huongezeka. Kwa kuwa sifa zote za Ukubwa ni za
Mungu peke yake.
Uhalisia Zaidi Wa Hatua ya Pili ya Tamaa
Lusifa alishindwa kuelewa kuwa
‘’hata uwe na vitu vyote, kama huna Upendo, wewe si kitu’’. Msingi wa Ulimwengu
ni Upendo, maana Mungu ni pendo. Mungu aliumba kila kitu kutoka hakuna kitu
‘’nothing’’. Biblia inaandika katika ‘’1Kor13 kuwa, hata ukiweza kusema kwa
lugha za Malaika, kama huna upendo si kitu wewe. Hata ukiwa na maarifa ya
kuelewa siri zote za mbinguni na duniani, kama huna upendo, si kitu wewe. Hata
ukitoa mali zako zote na uwape masikini kama huna upendo, si kitu wewe. Hata
ukitoa mwili wako ukachomwa moto kama huna upendo, si kitu wewe’’. Hizi zote
zilikuwa ni sifa za lusifa, na ndiyo maana alimwambia hata Yesu, ntakupa kila
kitu, ukinisujudia. Ajenda ya muhimu ni kuwa, Dhumuni kama sio Utukufu kwa
Mungu, aliyechimbuko la Upendo, basi yote ni ubatili.
Jamii imejaa watu wenye tamaa
za kuwa juu ya wengine, msingi huu wa tamaa Lusifa huujenga tangia binadamu
wanapokuwa wadogo. Hii ni kupitia kuwazoeleshea ushindani katika taasisi za
elimu, kupitia michezo wanayoifanya, kupitia filamu, sinema, na hata magemu
wanayoyacheza. Haya yote huwachochea sana kuingia katika falsafa za kutamani
kutawala wenzao, na sio tu kuwa na tamaa ya kufanikiwa. Binadamu wengi
hawaridhiki kwa hali zao njema, bali huridhika kwa matokeo yao baada ya
kujilinganisha na wenzao. Huu ni upumbavu mkubwa sana, haimaanishi kuwa kama
umepata 30, na wanaokufuata wamepata 5, basi wewe umefaulu kama kipimo cha
ufaulu ni 50. Hii ni sawa na kusema, ujihesabie haki kwa kutofanya sana uzinifu
kama wanavyofanya jamii inayokuzunguka! Vipimo vya ukweli havilinganishwi na
mtazamo wa jamii ‘’relative standards’’, hulinganishwa na vipimo vya haki
‘’absolute standards’’.
Kadri watu wanavyoshindana,
ndivyo wanavyotazamia zaidi kuwa juu ya wenzao. Wengi wao sio watu wakutazama
na kuona, bali hutazama na kulinganisha. Sio watu wa kusikiliza, bali husikia
na kulinganisha. Idadi kubwa ya watu katika hatua hii ya tamaa, hushindwa
kunufaika na ubora wa hali zao zisizolinganishwa.
Lengo La Lusifa
Lengo la Lusifa katika hatua
hii, ni kuwatengenezea uhalisia feki wengi wa mateka wake. Mtu aliye na utajiri
mkubwa sana lakini hana mamlaka huishi kama mtu asiye na kitu kabisa kwasababu
tu ya kujilinganisha na aliyejuu kabisa zaidi yake. Vivyo hivyo mtu aliye na
afya huishi kama vile asiye na afya kabisa kwa kujilinganisha na aliye na afya
na mamlaka zaidi yake. Kiufupi lusifa analenga jamii isiyo na shukurani kwa
hali walizonazo. Na matokeo yake ni kupata watu wasio na shukurani kabisa kwa
hali walizonazo, ziwe za juu, ama za chini.
Wahanga Wa Tamaa Hatua Ya Pili
Viongozi wengi sana katika
taasisi za umma, binafsi, na za kidini, wasomi wengi sana na vijana walio
katika hatua za mafanikio, na wengineo wengi. Hawa wote hutekwa na lusifa
kirahisi sana kutamani kuwa juu ya wengine. Na ilihali wakipambana sana kuwa
juu ya wengine, hujikuta wakiingia katika wimbi la uraibu wa kutamani tamaa ya
lusifa ya kuwa juu, na hapo ndipo msingi wa matatizo mengine yote.
3. Tamaa Ya Kuishi Milele
Hii ni aina ya tatu ya tamaa,
ni aina ya tamaa ambayo hulenga kiwango cha mwisho cha tamaa ya mwanadamu.
Yaani, mwanadamu alianza kutamani kuwa na uhakika wa Maisha, kisha akatamani
kuwa na heshima na sifa juu ya wenzake, na sasa, mwanadamu huyu anatamani
kuendeleza hali yake hii ya tamaa ya kuwa juu ya wenzake milele.
Na hapa ndipo utakuta wafalme
wakijiita Mungu, hapa utakuta waheshimiwa wakubwa wakitaka upendeleo wa huduma
bora zaidi za afya. Hapa ndipo utakuta matajiri wakubwa zaidi wakitaka kuwekeza
katika miradi, au sayansi zitakazo wawezesha kuishi milele. Hali ya kuishi
milele ni tamaa ya hatua ya mwisho ya tamaa, hali yoyote ile ya umilele, ni ya
Mungu tu.
Viongozi wengi wakubwa
hutamani uhakika wa ulinzi toka kwa idadi kubwa ya walinzi wenye taaluma kubwa
kabisa. Siyo kana kama huwa hatarini
sana katika nafasi zao, ila ni kuwa huitaji usalama sana kutokana na nafasi
zao. Wapo viongozi wengi wakubwa walioamua kuishi Maisha ya kawaida sana, hasa
baada ya kuziona nafasi zao ni za kawaida sana. Na mara nyingi viongozi hawa
huwa wachache sana kwa idadi, na huwa na Maisha ya kutojiinua kwa nafasi zao,
kama wastani wa viongozi wengi.
Maana Ya Jaribu la pili la Yesu
Biblia inaandika, ‘’Kisha
ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu,
akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa,
Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu
wako katika jiwe.
Jaribu hili linafanania kabisa
hoja ya hatua ya tatu ya tamaa, ijapokuwa ni jaribu la pili. Jaribu hili
linaonyesha ni kwa namna gani Binadamu huwa tunajaribiwa kwa tamaa ya kuwa na
uangalizi wa Kiungu katika Maisha yetu ‘’divine intervention’’, hii ni kama
namna ya kutamani kuwa na muunganiko na uwezo wa kiroho, uhakika wa asilimia
100%. Kiufupi tunarejea palepale katika kutamani kuishi milele.
Watu kadhaa hutamani hata
kuambiwa kuwa wataenda sehemu Fulani baada ya Kufa. Lusifa anajua Kiburi cha
mwanadamu yeyote yule huisha anapoeleka katika kufa. Na hutamani sana
kumhakikishia kuwa hatakufa, aidha atabadilika kuwa kiumbe mwingine, au ataenda
sehemu bora zaidi.
Watu Hutamani Kuwa kama Mungu
Katika hatua hii ya tamaa,
ambayo inafungamana sana na hatua ya pili, iliyo katika jaribu la tatu. Watu
wengi sana hutamani na kujaribu Kutenda kama Mungu. Watu hujiona wakiwa na
uwezo wa kubadili majira na nyakati. Hujiona wakiwa na uwezo wa kuathiri Maisha
ya viumbe wenzao. Hujiona wakiwa na uwezo wa kufanya lolote lile. Kiburi hiki
huwasukuma sana kujiona kana kama wao si watu wa kawaida.
Hatua za wengi wa watu katika
tamaa kiwango cha mwisho, huelekea kutawala kabisa wenzao. Wengi wao hutumia au
hata kutengeneza dhiki nyingi sana kwa wanaowazunguka, na kutengeneza namna za
suluhisho ambazo zitawafanya wanaowazunguka kuendelea kuwasujudia, na wao
wakijilimbikizia nguvu juu yao.
Hutumia Sana Utajiri kama Silaha
Mara nyingi watu katika hatua
ya mwisho ya tamaa. Hujikuta sana wakiegemea katika matumizi ya mali zao
kutumia vikundi vya watu wa usalama kupambana na maadui zao. Kwao binadamu wa
usalama huwa kama Malaika. Mara nyingi watu hawa huwachukia sana maadui zao,
kwa kuwa wao huwa kama Mungu, na kisha maadui zao huwa kama wenye dhambi, na
mshahara bora zaidi kwao huwa ni kifo.
Katika kizazi hiki watu hawa
hutumia sana teknolojia za kisasa sana ili kuweza kujilinda, kwa kuwa na
taarifa za kila kinachoendelea duniani kote. Watu hawa hutumia sana teknolojia
katika namna mbili za kiuungu wao, yaani, kujilinda, na kujitukuza.
Sababu za Kupenda kuwa kama Mungu
Kusujudiwa huchochea kiini cha
tamaa ya binadamu mpaka mwisho. Chuki zote, wivu wote, fitina zote, hasira
zote, kiini chake ni kutamani kusujudiwa. Yaani, kuwa bora kuliko wote. Kama
kuna mtu unamchukia mpaka mwisho, akija kukusujudia, maana yake yupo mbele zako
akiwa chini mpaka mwisho, tayari kwa lolote utakalo. Ubongo wa binadamu
hutamani sana hii hali ya kiungu, na wadhaifu wote huiota kama alivyo Lusifa
mwenyewe aliyetamani kusujudiwa mpaka na Mungu wake.
Mungu pekee ndiye anaweza kufanya lolote, mwanadamu mpumbavu hutamani kuwa kama Mungu, kwa kiburi cha utajiri hujidanganya kuwa anaweza Kutenda yote. Na hili hutokana na kuwa, mali nyingi huathiri afya ya ubongo, maana utajiri uliokithiri ni matokeo ya ubinafsi. Watu wenye akili nyingi hujali sana jamii zao, na hapo ndipo ulipo msingi wa ugunduzi na maarifa. Jamii yangu inateseka sana, na mimi kama nina akili, nitazitumia kuwasaidia, matajiri wengi huona dhiki za watu kama fursa, na kuzitumia kuwa juu yao, watu wa mtindo huu kamwe hawawezi kuwa na akili bora kabisa.
MATAWI YA TAMAA KISAYANSI
Yafuatayo ni matawi ya tamaa
ambayo watu wengi sana hushikwa nayo kwa kuwa hushindwa kuelewa tamaa kiundani
kabisa. Sehemu hii nitaelezea kiufupi msingi wa ubongo katika kuangukia katika
mitego hii ya tamaa.
IBADA YA SANAMU & UCHAWI ‘’idolatry & witchcraft’’
Sitaelezea sana sehemu hii,
kwa kuwa nimeandika kitabu kinachohusu sayansi ya ubongo inavyohusiana na
mazingaombwe, uchawi, na miujiza. Katika kitabu cha Q6 msomaji atajifunza
sehemu za msingi za ubongo katika sura mbili za kwanza, kabla ya kuelewa nini
hutokea katika ‘’magic’’.
Kwanini ibada ya sanamu &
uchawi na tamaa?
Kwasababu mitindo hii yote
huusiana na kutumia na kuchochea sana sehemu za hisia, na sehemu za taswira
‘’imaginations’’, kupitia mfumo wa ubongo wa ‘’Default mode network’’, kadri
mtu anavyojifunza uchawi, au anavyofanya ibada za sanamu, anajifunza kuvutia
taswira kitu kilichombele yake, huku akielekea katika kuunda uhalisia tofauti
na uliombele yake. Yaani, mtu anaona sanamu ya ng’ombe, ila anavuta taswira ya
kutazamia mungu wake, hivyo hivyo kwa aina zote za wachawi, aidha kwa wale wa
‘’spell’’, ambao hunenea kitu huku akitegemea kutengeneza uhalisia wa kweli,
wachawi hufundishwa kuvutia vitu taswira, hii huitwa ‘’visualization’’, na
waabudu sanamu huingia katika kundi la wachawi la wasiotumia maneno,
‘’non-verbal rites’’, hawa hutumia sana ‘’Alama’’ au ‘’symbolism’’, nao hufanya
pia ‘’meditation’’, hizi zote kwa Pamoja hukinzana na sehemu za ubongo
zinazohusiana na uhalisia wa taarifa zilizopo mbele.
Madhara yake ni kuwa, mtu
huingia katika uhalisia feki wa taarifa, kwa kuwa ubongo wake sasa kama ambavyo
huonekana kwa namna unavyoathiri sehemu zake za ubongo zinazohusiana na
utambuzi wa taarifa halisi ‘’parietal connectivity’’, huanza kupata taswira
toka vyanzo visivyo na uhalisia. Kitaalamu ni mithili ya ‘’hallucinations’’,
lakini kiuhalisia ni roho za kipepo ndizo huwa zikiwakamata watu hawa, na
kuwaunganisha katika ulimwengu ambao wao huuona wa kiroho, kiufupi haya yote ni
matatizo ya kiakili.
Tamaa imeingiaje?
Wengi wa wachawi hutamani sana
kufikia hali za juu sana kihali zao za kiroho, hata kimwili. Wengi wao hupenda
ulinzi na heshima. Wengi wao hutamani uwezo wa kuwadhuru maadui zao. Wengi wao
hawapendi wawepo wenye mafanikio kuwazidi, au wenye kuwapinga. Waabudu sanamu
pia hutamani sana ukaribu wao na miungu yao kiasi cha kutaka muitikio wa moja
kwa moja kwa kuwa karibu zaidi na miungu yao. Na haya yote yamejengwa katika
misingi ya tamaa, hata kumuasi Mungu wa kweli.
UADUI NA UGOMVI ‘’hatred & variance’’
Kwa utafiti mdogo sana
unaoweza kuufanya, utagundua wengi wa watu hawagombani kutokana na kuwa
hawawezi kukaa Pamoja na kutatua tofauti zao. Maana panapotokea mgogoro wowote
ule, huwa kuna pande mbili ambazo watu hupishana, lakini ukweli ni kuwa,
hakujawahi kuwa na kweli mbili. Na ukweli haujawahi jificha, kama watu wataamua
kukaa Pamoja na kujadili pande zote kiundani kabisa, ukweli huonekana na watu
hufanya maamuzi yaliyo sahihi.
Kwanini sasa Ugomvi na uadui?
Mara nyingi mmoja au wote huwa
na tamaa. Marazote mmoja kwa tamaa zake za kutamani kuwa na mamlaka juu ya
jambo linalogombaniwa, hupuuzia kabisa ukweli kuhusu upande wa pili. Uadui ni
hisia za ndani za chuki. Lakini Ugomvi huwa ni matokeo yanayoonekana ya uadui.
Watu hugombana kwa kuwa mwenye
ukweli huamua kuushikilia, na asiye na ukweli hutaka kutimiza matakwa yake. Ili
hali wakigombana, wote sasa huwa wapumbavu. Maana baada tu ya uadui kuanza kama
ugomvi, sehemu za hisia za wote wapinzani huwaka mpaka juu, na kama ilivyo
kawaida hisia zinapoinuka, basi sehemu za akili za ubongo hushuka mpaka mwisho.
Na ndiyo maana wenye busara huwa na uvumilivu sana kuzuia hisia kuwa na nguvu
juu yao, hata wakashindwa kutawala misuli ya mikono, miguu, na midomo yao.
Popote pale panaposhamiri
hisia za uadui, na kuibuka migogoro. Tamaa huwa zimejaa. Kadri unavyopanda
ngazi za kimamlaka, ndivyo uadui na ugomvi huongezeka zaidi. Mpaka sasa msomaji
anaweza kuelewa kwanini? ni kwasababu tamaa huongezeka toka hatua ya kwanza,
mpaka hatua ya pili na tatu.
WIVU NA HUSUDA ‘’emulations &
envy’’
Kwanza wivu kwa kuutafsiri tu,
ni tamaa ya kuzidi wengine, au tamaa ya kuwa bora zaidi. Wivu huwa ndani ya mtu
ukiwa haujioneshi, lakini inapoonekana mazingira ya kuwa kuna aliye juu zaidi,
wivu hujidhihirisha kwa hali ya kutotulia kiakili, au kuumia, au kutaka ashuke
mpaka chini.
Husuda ni sawa na wivu?
Husuda huwa ni namna ya wivu
ambayo tofauti yake na wivu moja kwa moja, ni kuwa Husuda hulenga zaidi hisia
za chuki kwa kuona mafanikio ya wengine. husuda huwa hailengi mwenye wivu
kutamani yeye kuwa juu. Mwenye husuda huumia kwa mafanikio ya wengine, lakini
haleengi hata yeye kuwa juu.
Sayansi ya wivu
ubongo hulenga kumfanya mwenye
wivu awe juu. hivyo kwanza, huchochea hali ya kutotulia ya kiakili kutokana na
hisia za ubongo za ‘’sympathetic nervous system’’. ambazo huambatana na stress,
kwa lengo la kumchochea mwenye wivu aongeze bidii, ili aweze kuwa juu. Hapa
ndipo utakuta mwenye wivu akipambana sana ili kurejea kwenye hali yake ya awali
ya kuwa juu.
Pili, mwenye wivu huwa na
kiwango kikubwa sana cha homoni za stress, na hata homoni za dopamine, ambapo
hizi na saketi zingine nyingi za ubongo huelekezwa katika kumfuatilia mpinzani
wake, kwa lengo la kumuangusha, ila ubongo wake uweze kuzalisha homoni za
serotonins, na endorphins nyingi, uweze kuburudika sasa. Hapa ndipo mwenye wivu
huchanganyikiwa sana kisaikolojia, maana huteswa na kumbukumbu za mpinzani wake
aliye juu, huteswa na mafanikio ya wenzake, na njia pekee ya kukabiliana na
hali hii ya mateso ya kisaikolojia, huwa ni kubuni mbinu za kujituliza. Na hizi
huwa ni kumfelisha mpinzani wake pale anapoweza, pili huwa ni kumchafua
mpinzani wake pale anaposhindwa, na mwisho, huwa ni kutomfatilia mpinzani wake
pale anapoona hakuna matokeo.
Je Wivu ni Hatari?
Kwa wenye wivu huwa ni hatari
sana, maana idadi kubwa sana ya wenye wivu, huwa na tamaa, na tamaa huwafanya
kuwa makini sana na wenye wivu wenzao. Bila takwimu unaweza gundua wenye wivu wengi
huwa makini zaidi na wenye wivu wenzao. Hatari kubwa zaidi ya wivu ni kwa
mwenye wivu, maana hushindwa kunufaika kwa Habari njema anazopatiwa, au watu
wakubwa anaokutana nao. Kipindi Yesu anazaliwa, badala ya Herode kunufaika kwa
Habari njema za ujio wa Kristo, anapata wivu wa kutaka kumuua, kwa kuhisi
atachukua sifa au nafasi yake, na madhara yake akafeli yote.
HASIRA ‘’wrath’’
Hasira yenye matokeo makubwa
sana kisaikolojia, hutumia neno hilo ‘’wrath’’. Mara nyingi watu walio na afya
ya kiakili, huwa na msukumo wastani wa hasira, hii ni kwa kuwa, kama zilivyo
hisia zingine, zinapovuka uwezo wa kujitawala, huchochea udhaifu. Hasira ni
hisia za kukerwa kutokana na matokeo ambayo yanaonekana kuwa na madhara ya
kimwili, au kisaikolojia. Mfano, kuvunjiwa heshima, kuumizwa mwilini, n.k.
Sehemu hii hasira haipo katika
mantiki ya hisia zinazotokana na mifano hiyo juu, maana hasira ni muitikio wa
asili wa mwili wa kujilinda. Hakuna asiye na hasira pale anapofanyiwa vitu
hatarishi kwa mwili wake na akili yake. Mwili lazima utazalisha homoni kama
adrenaline, cortisol, glutamate, noradrenaline, n.k. hizi na neva nyingi za
fahamu huchochewa kusukuma muitiko wa haraka wa mwili wa kujilinda, ikiwemo
kutumia nguvu za mwili kwa haraka na ustadi ili kujilinda, kwa kupambana, au
kujiepusha.
Hasira kama tamaa?
Watu wenye hasira kupindukia,
wote huwa na mfanano mmoja. Wote hutamani kuogopwa, kuheshimiwa kupindukia,
kuwa na urahisi wa kulazimisha matakwa yao, na wengine hutaka hata kuabudiwa.
Hasira za watu hawa huwa ni matokeo ya kisaikolojia, aidha kwa kujitengenezea,
au kwa kutengenezewa, kama ambavyo huwa kwa wagonjwa wa ‘’post-traumatic stress
disorder’’, yaani, watu ambao waliwahi kutendewa jambo ambalo liliwaumiza sana.
Kiufupi lazima watu watambue, hali hii ya hasira ni hali ya tamaa ya kufikia
hali ya amani ya kimwili, lakini kwa kupitia kuwafanya wengine wadhaifu, hii
haina tofauti sana na zilivyo tamaa nyingine kama za wivu, na uchawi.
FITINA, FARAKA & UZUSHI ‘’strife, sedition & heresies’’
Fitina
Sifa kubwa ya mtu mwenye
fitina, huwa haisi kama anaweza kukubaliana na hali Fulani. fitina ni hisia
zinazosukuma hali ya upinzani, ndani ya kikundi, hata wakati mwingine ndani ya
mtu binafsi. Fitina ni tawi la tamaa ambalo wakati wowote hujidhihirisha kwa
kuleta matokeo hasi kwa nje. Mwenye wivu hutofautiana kidogo sana na mwenye
fitina, wote huchukia hali zilizopo juu yao, tofauti yao ni kuwa, mwenye fitina
huwa na hisia za ukinzani zinazotokana na sababu nyingi, wakati mwingine,
mitazamo yake binafsi. Mfano, mwenye fitina anaweza kuwa marazote tu akimchukia
mtu Fulani, kwa kuhisi tu mtu huyo anasifa Fulani mbaya.
Kwanini fitina ni tamaa?
Marazote wenye fitina huwa
hawawezi kukinzana na hali yao ya chuki dhidi ya wapinzani wao, kwa kuwa sababu
zao huwa hazitokani na sababu za nje ambazo wangeweza kuzitatua, huwa
zinatokana na sababu zao za ndani za tamaa. Sababu za kutamani wapinzani wao
wadhalilike, au wafeli, ili wao waweze kuwa na nafasi, au amani.
Faraka
ni hali ya kuibua hisia za
ukaidi dhidi ya mamlaka, au mfumo Fulani uliopo. Mfano, penginepo mwenye fitina
angeweza kuibua hisia za kuwa, mwandishi wa kitabu hiki ni mkaidi, na
anachochea chuki dhidi ya mifumo yenye nguvu. lakini ili maana ikamilike ya fitina,
lazima tuangalie dhumuni la hoja ya ukaidi. Mwandishi wa kitabu hiki
angeonekana akiwa na lengo la Upendo, na kuikoa jamii kwa upendo, na amani,
bila hasira, uadui na ugomvi. Lakini mwenye fitina huwa na dhumuni la Tamaa, la
kuchafua hali iliyopo, ili aweze kupata nafasi ya kuwa juu ya wengine.
Wenye fitina wengi sana
utawagundua kwa namna huwa hawana taarifa za kutosha kuhusiana na hoja
wanazozichafua, wengi wao huwa hawana kiasi, waropokaji, hii yote ni kwa kuwa,
hisia za fitina zinatokana na matatizo ya kisaikolojia. Na fitina huambatana
moja kwa moja na hisia za uadui, na hisia za ugomvi.
Uzushi
Uzushi unatokana na hali za
kuzusha. Kuzusha kunamaanisha kuibua. Kuibua kunamaanisha kutoa toka sahihi, na
kupindisha. Kwa kiingereza unaweza tumia neno ‘’deviate’’. Wazushi ni watu
ambao huibua hoja zao toka kwenye ukweli, na kuzipaka rangi na kuzizusha. Wapo
ambao hufanya makusudi wakijua, lakini wapo ambao hufanya wakiamini wamegundua
udhaifu uliokwepo.
Kwanini uzushi ni tamaa?
Marazote wazushi hutamani
kupata heshima, na sifa, toka kwa watu, kama wao ni watu makini kuweza kugundua
udhaifu uliopo. Wazushi huwa na tamaa ya kuwa nje na mifumo yao, ili kuonekana
wao wapo makini zaidi, au wenda, wao wana uwezo mkubwa zaidi.
Wazushi wote hawana kiasi,
wazushi wote hutumika sana kuchafua mamlaka na mifumo safi kabisa. Wazushi
wengi huwa wasaliti, na wengi wao huwa ni wagonjwa wa kisaikolojia.
Saikolojia ya fitina, faraka & uzushi
Wote wenye sifa kati ya hizo
juu tatu, huwa na tatizo moja kubwa. Huwa hawana uwezo wa Kuzingatia na
kutawala hisia zao. Wengi wao ni wadhaifu wasio na uhuru wa kifikra ‘’open
mindedness’’. Huweza kupata ukweli, lakini kwa kuogopa kubadilisha misimamo yao
kwa kufatilia kwa kina, hupuuzia. Wengine hawana hata uwezo wa kufatilia mambo
kwa umakini sana hata wakayaelewa, na hujikuta wakizusha tu.
Wenye fitina wengi huwa na
namna ya tofauti kidogo ya wivu, na hushindwa kutatua changamoto zao kwa hisia
za uadui, na huishi Maisha feki ya chuki kwa majirani wao, huku wakiwatamania
mabaya. Haya yote ni makundi ya tamaa.
ULEVI ‘’drunkenness’’
Unaweza soma kitabu cha Q4
kuelewa kiundani madhara ya afya ya ulevi, na madhara ya pombe kuanzia tumboni,
katika ini, mpaka katika ubongo. lakini unapozungumzia ulevi, unazungumzia
madhara ya kupoozesha, au kulewa, au kuzubaisha akili, kwa kutumia vileo,
ambapo hasa zaidi ni pombe. Zipo namna nyingi za vitu vya kulevya, kuna madawa
ya kulevya, kuna bangi, shisha, n.k.
Kwanini ulevi ni tamaa?
Tofauti ya mlevi na mchawi, ni
kuwa mchawi akishalewa anazungumza na mapepo, lakini mlevi akilewa anarudi
nyumbani. Wote kwa Pamoja wanakimbia uhalisia wa Maisha yao ya kawaida. Mlevi
anaamini akishakunywa pombe, ataingia katika hali ya utulivi wa kiakili, na
katika namna mbalimbali walevi hujikuta wakishakuwa waraibu, hii ni kutokana na
matatizo ya ubongo katika sensa, au ‘’receptors’’ za ubongo, kama ‘’GABA, na Glutamate’’,
na hata ‘’Dopamine’’, unaweza soma Q4 kuelewa kiundani uraibu wa pombe
‘’withdrawal syndrome’’.
Ulevi ni tamaa ya kuwa huru
toka katika uhalisia wa Maisha ya kawaida. Watu wengi ambao huchochea ulevi, huchochea
hali za kiburi, za kutowaza, za kutojali. Wasomi wengi hawajui madhara ya pombe
huanza hata kabla ya pombe, wengi huanza na kiburi na kujipa hisia za kutojali
hata kabla ya kunywa, na hapo ndipo unapoweza kuthibitisha hisia za tamaa, za
kutaka kuwa nje ya mfumo wa akili za wengine, ambapo kwa mlevi ni wote
mnaomtaka asinywe.
Hali ipo hivyo hivyo kwa
wavuta sigara, bangi, shisha, madawa ya kulevya, n.k. kiufupi matatizo huwa
makubwa sana kabla ya wengi wao kuanza, lakini short cut ya kufikia hali bora
kabisa ya kiakili kupitia ulevi ndiyo huwaathiri wengi.
ULAFI ‘’revellings’’
Ulafi ni hali ya kushindwa
kujitawala katika hamu ya chakula. Ulafi ni tamaa ya kula mpaka mwisho.
Marazote ili mtu awe mlafi, lazima mfumo wake wa ubongo wa hamu za kula, na
kuridhika kwa chakula uathiriwe ‘’disruption in orexigenic pathway’’. Na vyakula
ambavyo vinaweza kumuathiri mtu hata akaingia katika hali hii ya ulafi
nimevielezea vizuri sana katika Q4.
Kwa ufupi sana, Ulafi
hutengenezwa zaidi ya kutokea kwa asili. Watu wengi walafi hufikia hatua hiyo
kwa kula sana vyakula vyenye msisimko mkubwa sana wa Ladha, kuliko wastani wa
asili. Madhara yake mfumo wa homoni wa hamu za kula huathirika. Mfano mwepesi
ambao huwa napenda kuutumia ni kuwa, kijiko kimoja cha sukari ni wastani sawa
na mtu anayekula mita moja ya muwa, lakini mtu mmoja anayekunywa soda moja tu,
huwa na wastani unaokaribia wa vijiko kumi vya sukari. Hiyo ni sawa na kusema
mtu anayekunywa chupa moja ya soda ni sawa na mtu anayekula mita kumi za muwa,
jambo ambalo linaonyesha ni triki tu ya ubongo iliyechezwa na wazalishaji wa
bidhaa hizi.
Ulafi hukua kwa matumizi ya
vyakula vyenye vichocheo vingi kupita wastani unaohitajika, mfano, sukari
nyingi watu ambayo hutumia katika bidhaa za kisasa huwa kiundani haihitajiki
mwilini, watu wengi hula nyama kwa kiasi ambacho kiundani hakihitajiki mwilini,
mfano, kwa wiki nzima mtu mzima angehitaji nusu kilo tu ya nyama, na hapo bado
takwimu huonyesha ni nyama ambayo angebidi kuipunguza zaidi. lakini watu
hutumia maranyingi zaidi ya wastani. kiwango cha pombe ambacho mwili
ungekivunja ni kidogo sana na uhalisia wa kiwango ambacho watu hutumia hata
kulewa. Haya yote yanachochea kuwa, ulafi hutengenezwa sana kwa triki za
kiakili, ambazo nilizielezea sana katika injili ya sayansi Q4, ikiwemo kucheza
na uzalishaji wa homoni ya msisimko ya dopamine, na kuchochea tabia za ulafi.
Walafi wengi sana sio
wakarimu, hawana kiasi, hiyo yote ni kutokana na tamaa zilizokithiri za
vyakula, ambazo huwaathiri hata afya zao za kiakili.
UFISADI
Ufisadi ni neno linalomaanisha
matumizi mabaya ya mali za umma kutokana na mamlaka. Ufisadi huwa na familia
yake ya tabia, kama vile rushwa, wizi, n.k.
ufisadi moja kwa moja ni tamaa ambayo inatokana na kutamani zaidi ya
mamlaka uliyopatiwa, na kibaya zaidi, mafisaidi wengi huwa ni wasiri sana wa
wizi wao wa mali za umma.
Tofauti ya fisadi na mwizi, ni
kuwa mwizi hutambulika na husukumwa na tamaa zinazotokana na kutokidhi hali
yake, au hata tabia ya kutamani zaidi kwa njia ya kuiba. Lakini fisadi huwa ni
mtu asiye mwaminifu kwa ndani, lakini kwa nje kuvaa huusika mwingine. Fisadi ni
mnafiki kwa mamlaka anayoshikilia. Mara nyingi fisadi hupelekea madhara makubwa
zaidi ya mwizi, kwa kuwa huwa na nafasi rahisi na endelevu zaidi ya kuiba, na
hata kujilinda dhidi ya kugundulika. Watu hawa huwa wanatamaa sana, na huvikwa
roho ya ubinafsi, na ukatili, na hata uuaji kwa wanaowagundua. Mungu huwachukia
sana watu wenye tamaa hata wakafikia hatua hii.
UZINZI, UASHERATI& UCHAFU
‘’adultery, fornication, uncleanness,
lasciviousness’’
Uzinzi ni tendo la ndoa kabla
ya ndoa, kwa wasio wanandoa. Uasherati ni tendo la ndoa, kwa mwenye ndoa, na
asiye na ndoa. Uchafu ni matendo yote yanayohusiana na kufanya mapenzi katika
namna zisizo za kimaadili, au za kisasa zaidi kama utazamaji wa filamu za
ngono, na kutumia vitu, au namna zisizo za asili katika kujiridhisha kimapenzi.
Lusifa na mapenzi
Lusifa anapenda sana kutumia
tendo la ndoa ‘’sex’’ tangia zamani sana za kipagani. Lusifa hupenda sana hisia
hizi za mapenzi kwa kuwa, huwafanya watendaji kuwa dhaifu sana kiakili. Hii ni
kwasababu marazote mapenzi husisimua sana hisia kiasi cha kuzimisha kabisa
sehemu za ubongo za kutafakari, na matokeo yake ni kuwa, watu wengi huwa
hatarini sana kuvamiwa na roho chafu, au hata Kujawa na uraibu kwa kushindwa
kujitawala kihisia, pale yanapofanyika kinyume na utaratibu wa kiasili.
Marazote jamii za kipagani, na
taasisi za kiumizimu huusisha mionekano ya utupu, au hata matendo ya kiuzinzi.
Lengo hasa huwa ni kudhoofisha kabisa uwezo wa kiutambuzi wa watu. Lusifa hasa
katika mitindo ya kisasa amechochea zaidi uhuru wa tabia za uchafu wa kingono,
wengi hawajui ni nini sababu ya msingi kabisa ya kuchochea mitindo hii ya zinaa kupitia miziki, filamu, na mitandao
ya kijamii. Malengo makuu ya lusifa ni kama yafuatayo:
Kama tulivyoangalia katika Q4,
kadri watu wanavyoangalia taswira zozote zile, huwa wakijiunganisha nazo, hii
tuliona kupitia uwepo wa seli za kuiga, yaani ‘’mirror neurons’’, katika maeneo
ya juu ya ubongo kama ‘’premotor areas’’, maeneo haya huusiana na msisimko wa
mwili moja kwa moja. Kadri watu wanavyotazama taswira za uchi, ndivyo
wanavyoingia katika msisimko wa via vya uzazi, na kutamani zinaa moja kwa moja.
Hoja sio kutamani tu zinaa,
hoja ni kuwa, kadri watu wanavyoingia katika hisia za mapenzi, au ngono katika
mazingira yasiyo na utakatifu, huwa katika hatihati ya ubongo wao kuwa hatiani
kuvamiwa na roho za uchafu. Wanasayansi baadhi hujifanya hawaamini roho hizi,
lakini huamini Aliens, na wakati huohuo wengi wao huwa wanachama wasiri wa
vyama vya kishetani. Wapo baadhi ni wahanga kabisa wa Imani za ushirikina,
lakini kwa nje hujifanya hawaamini Imani za roho hizi, injili ya sayansi haina
muda wa kuhangaika na wasomi wanafiki.
Tabia za Kujisugua ‘’masterbation’’, na Pornography
Hawa wote ni kielelezo cha
ngazi ya juu kabisa ya tamaa. Yaani mtu anatamani kitu ambacho hakipo pale, na
ubongo wake unatengeneza uhalisia wa kana kama yupo pale. Hakuna mwanamke
aliyelala kwa ajli ya zinaa, lakini mtu kupitia network yake ya Ubongo, ya
‘’Default mode network’’ anamtengeneza binti kichwani, anampeleka katika sehemu
yake ya ubongo wa mbele, anamuandaa, na sehemu yake ya hisia inasisimka kiasi
cha kuchochea Ubongo sehemu ya Hypothalamus-tezi ya pituitary, mpaka via vya
uzazi vinasisimka kwa ongezeko la mtiririko wa damu mithili ya mwanaume
anayefanya zinaa halisi, mtu huyu mfumo wake wa PSNS ‘’parasympathetic nervous
system’’ husisimka na kumfanya aendeleze mhemko wa via vyake kama mtu aliye
kwenye zinaa kweli, katika Q4 nilielezea madhara wanayopata watu hawa kiafya,
lakini katika sehemu hii nalenga kuonyesha namna watu hawa mfumo wao wa ubongo
unavyoathiriwa, na kutengeneza gepu pana sana lililo wazi la roho chafu kuingia
katika sehemu zao za ubongo wa mbele, na kuwatengenezea uhalisia na uraibu, na
hata kuwatawala kabisa kifikra.
Tabia za Uchafu wa Kingono
Mara nyingi watu hawa huwa
wamejawa na roho za ngono zilizovuka wastani wa kawaida. Kwanini? ni kwakuwa
maranyingi watu wenye uchafu katika mitindo ya kingono, huwa tayari ni wahanga
wa hatua za kwanza za ngono. Wengi wao kama nilivyoeleza katika kitabu cha
‘’Ubongo wa mtu mweusi’’ huwa hawasisimki tena na utendaji wa ngono katika
mitindo ya kawaida. Wengi wao huwa hawana nguvu za kiume aidha, au huwa wahanga
wa mitindo ya zinaa tangia udogoni, hivyo huwa wakitafuta namna za kujiridhisha
zaidi, maana ubongo wao huwa na msisimko mdogo zaidi kwa njia za kawaida za
tendo la ndoa.
Utazamaji wa filamu za kisasa
zilizojaa picha, na mionekano ya kizinaa tangia umri mdogo, huathiri ukomaaji
bora wa ubongo, na uwezo wa kuwa na kiasi katika kutawala mihemko ya kimwili.
Wanaume ambao huwa na tabia za kishoga wengi wao huwa hawasisimki kabisa kwa
tendo la ndoa la asili kati ya wanaume, na wanawake. Hakuna shoga anayeingiliwa
kinyume na maumbile akawa sawa kiakili, lazima atakuwa alikuwa mwathirika wa
PTSD awali, lakini baadaye akajifunza uwendawazimu. Ukirejea kitabu cha Q5
unaweza kuelewa kiundani kabisa hoja hii yenye misingi mipana katika fiziolojia
ya ubongo.
SILAHA TEGEMEZI YA LUSIFA
Lusifa anapojua kuwa hana
namna nyingine yoyote ile ya kuwashinda watu makini wa Mungu wenye maarifa.
Hutumia njia za kuwatega kihisia kuwatega kwa tamaa za kimwili. Kiufupi hisia
za mapenzi huwa hazihusishi uwezo wa kutafakari, na kama utaweza kuwafanya watu
wasitafakari, hata wenye maarifa makubwa unaweza kuwateka katika gari la
uharibifu. Kwa wastani katika mitandao
ya kijamii, huwa kuna picha za wanawake wanaojipost 3 mpaka 4 kwa1 ya wanaume.
Hii ni kwa mitandao kama Tiktok, Instagram, na Facebook ikiwa kwa wastani mdogo
kidogo.
Watu wengi hawajui kwanini
picha nyingi zaidi huwa ni za kike, sababu ni kuwa, wanaume husisimka sana kwa
kutazama, zaidi ya wanawake. Ambapo wanawake husisimka zaidi kwa mambo
wanayoyasikia, na hii ndiyo sababu wanawake hushawishiwa sana na mienendo ya
kijamii, kama nilivyoeleza katika Q5, hata sehemu za ubongo za wanawake za
lugha zimeendelea zaidi ukilinganisha na kwa wanaume. Wanaume huathiriwa zaidi
na mitandao ya kijamii kwa kuamshwa kitamaa za ngono, huku wanawake
wakiathiriwa zaidi kwa mitandao ya kijamii, kwa kutamani Maisha ya kifahari na kuwa na wafuasi wengi.
Haya yote ni matokeo ya tamaa, na huchochea tamaa, na humtukuza lusifa.






Join the conversation