Jipatie maarifa kutoka vitabu bora vilivyoandikwa na Dr Brighton shoo kuusu imani, sayansi, afya, teknolojia, asili, malezi, saikolojia na mazingira

LUSIFA NA TRIKI YA ''HEGELIAN DIELECTRIC'' #10

MTAALAMU WA TRIKI YA MUDA & SANAA YA KAMALI YA AKILI

                                              ‘’HEGELIAN DIELECTRIC’

Hegelian dielectric

Nina uhakika kuwa, Lusifa hana mbinu yenye mafanikio zaidi ya hii. hii ndiyo mbinu ambayo Lusifa amekuwa akifanikiwa kwayo kwa miaka mingi sana. Kwa ufupi sana, kuelewa maana ya sanaa ya kamali ya akili, ambayo nimetumia neno hilo kumaanisha sanaa inayoitwa kwa Kiingereza ‘’Hegelian dielectric’’, unaweza elewa kwa kutumia mfano ufuatao.

‘’natengeneza ajenda yangu kuwa, Watu wanahitaji Uhuru wa kuamua lolote lile wanalolitaka ‘’hii inaitwa -thesis’’. Na kisha baada tu ya muda nasema kuwa, au hata mimi bila kusema itaonekana kuwa, ‘’Uhuru bila mipaka ni hatari sana’’, na hii sasa tayari inaitwa -antithesis’’, au ukinzani. Na hivyo sasa, baada ya hii ‘’antithesis’’, sasa ndipo naibua ajenda yangu ya msingi ambayo nitasema, ‘’tunahitaji uhuru lakini chini ya sheria kadhaa ambazo nitakuwa nimekwisha ziandaa’’, hii ndiyo inaitwa ‘’new thesis’’. Hii falsafa imetumiwa sana hata na kina Karl Marx ambao walikuwa ndiyo wapinga Kristo wakubwa kabisa kutokea Duniani, falsafa hii japokuwa huonekana kugunduliwa na mwanafalsafa wa Kijerumani ‘’Friedrich Hegel’’  miaka ya karne ya 19, lakini tayari ilikuwa imekwisha kuanza kutumika na Lusifa kwa miaka mingi sana.

                                             UTANGULIZI

Lusifa hajawahi kufanya kazi akiwa yeye kama yeye, hata nitakapokuwa nikisema Lusifa, ninachomaanisha ni namna Lusifa anavyowasilisha Mawazo yake, na akili zake za uharibifu kupitia binadamu, au viumbe  wake. Kuelewa namna Lusifa anavyoweza kuingiza Mawazo yake moja kwa moja kwa binadamu, unaweza Kwenda kusoma kitabu changu cha sanaa za mazingaombwe, uchawi, na sayansi ya ubongo. ila nitajaribu kugusia baadhi ya hoja za msingi hata kwa sehemu hii. katika sura hii tutatazama kiundani namna ambavyo Lusifa huwa akitumia watu kukamilisha hila zake kwa kutumia mbinu ya kwanza ambayo ni triki ya muda, na kamali ya akili ‘’hegelian dielectric’’.

Kwanini Lusifa hawezi Kutenda moja kwa moja yeye kama yeye, zipo sababu kadhaa, awali nilishasema kuwa Lusifa ana mipaka ya utendaji katika sayari hii ambayo inahitaji utendaji wa mwili, lakini pia lusifa anataka kumuonyesha Mungu kuwa ni viumbe wake yeye mwenyewe wanaomchukia kwa udhalimu wake, lakini pia Lusifa anataka kuwateka kwa kuwalaghai ili hatma yake asibakie hata mmoja mwenye haki. Na ndiyo maana nilisema pia awali kuwa, Lusifa ana motisha kubwa sana ya kuwadanganya wanadamu na kuwalaghai ilihali anajua kuwa alishashindwa kuwazuilia Wokovu wao kwasababu mbili, kwanza anahisi kama ataweza kuwaangusha wanadamu wote wenye haki, ataweza kuharibu mpango wa Yesu wa kurudi mara ya pili, maana hakutakuwa na mwenye haki hata mmoja, na hivyo atachelewesha wakati wake wa kuangamia, lakini pia, kwa kuwa Mungu amekwisha muwekea mwisho wake, basi kadri tunavyoelekea mwisho wake ndivyo mwisho unavyomvuta zaidi, kwa kuwa mwisho wake ni Kifo, na chanzo cha Kifo ni uovu ‘’mshahara wa dhambi ni mauti’’, basi Uovu wake unasukumwa zaidi ili hatma yake itimie.

SAYANSI YA TRIKI YA LUSIFA KATIKA MUDA

Katika Injili ya sayansi Q1 nilieleza kuwa Lusifa amekaa katika sayari ya Dunia kwa miaka mingi sana, karibia 6000, huku binadamu wakidumu kwa wastani wa miaka 70-100 tu. Lusifa hasahau taarifa, huku binadamu wakihitaji kurejelea kumbukumbu zao kila wakati, na mwisho, Lusifa anaweza kuwepo katika maeneo mengi sana kwa wakati mchache, huku mwanadamu akiwepo katika eneo moja tu, kwa wakati mmoja.

Faida hizi humpatia Lusifa uwezo mkubwa sana wa kumchezea akili mwanadamu. Sasa basi, hoja ya kutambua hapa ni kuwa, wanadamu kwa kawaida hubadili mitindo yao ya Maisha, au hata falme hubadilika toka kuwa juu, mpaka kurudi chini kabisa, walahu kwa wastani wa kila baada ya vizazi kumi, kumbuka kizazi kwa wastani ni miaka 25-30 kwa mujibu wa toka Watoto wanazaliwa, mpaka na wao wanazaa. Ukiweza kukaa kwa kipindi cha miaka 250-300, utagundua kuwa dunia huwa inabadilika moja kwa moja na kuwa ya tofauti kabisa. Sasa basi, kwa kuwa binadamu huishi kwa asilimia kama 25% tu ya wakati huu, basi wengi wao hujikuta wakiingia katika mtego bila wao kujijua.

Mfano, kipindi serikali mbovu inapokuwa madarakani, na viongozi wake wakiwa wala rushwa sana, wengi wa mafisadi hujikusanyia sana mali, wakiwakandamiza watu wa matabaka ya chini, bila wao wenyewe kujali, huku wakiona kawaida sana, lakini kumbe, wakati Huo Lusifa huwa anatumia hiyo faida kukamilisha mabadiliko ambayo ameyalenga miaka kadhaa tu mbeleni, na unaweza kuta, mwaka tu baada ya kizazi cha mafisadi hawa kupita, jamii hiyo ikibadilika kabisa, wenda kwa vita, falsafa, Imani, mapinduzi, n.k. lakini uwezo mdogo wa binadamu wa kuweza kuishi kwa muda mrefu, humfanya kuwa mpumbavu mbele ya faida ya lusifa ya kuweza kushuhudia muda ukiwa chini yake.

KAZI KUBWA YA LUSIFA YA KUIMALIZA DUNIA KUELEKEA 2031±

Mara zote ninapotumia 2031, huwa namaanisha ni kipindi kizuri cha makadirio ambacho dunia inaenda kukamilisha miaka 6000 ± na hivyo, ni kipimo kizuri sana cha utendaji wa kiumbe mkubwa kama Lusifa kwa kipindi cha milenia zote sita ambazo zimepita chini yake.

                      ZAMA ZA KWANZA ZA LUSIFA

Hatua ya Kwanza ‘’ 0-313 AD’’

Hiki ni kipindi chote tangia Yesu anazaliwa, anakamilisha misheni yake, na anawaachia kazi mitume yake, hiki kipindi kilihusiana na maendeleo makubwa sana ya Ukristo katika Dunia. Lusifa hawezi kukubaliana na Ukristo kama tulivyoona katika sura iliyopita. Katika Biblia hiki ni kipindi ambacho katika vipindi vya makanisa saba ya Ukristo, ni kipindi cha kanisa la Efeso, na Smirna. Kipindi hiki, sehemu kubwa sana ya Dunia ilikuwa na Upagani. Na Ukristo ulikuwa na Nguvu sana, hii ni kutokana na nguvu ya ukweli ambayo ilikuwa imeubeba, na Nguvu ya Mungu ambayo pia, uliambatana nayo.

Lusifa alitumia mbinu ya Maumivu, na maangamizi ya damu ya wakristo ili kuwamaliza. Mbinu hii Lusifa huitumia marazote pale anapoona maadui zake ni wachache. Lusifa hutumia mbinu ya Uongo pale maadui zake anapoona ni wengi. Katika Historia ya Dunia unaweza kugundua kuwa kipindi hiki kilihusiana na Umwagaji sana wa damu za wakristo, mfano, kuanzia mwaka 303 mpaka 313 inafahamika kuwa ni kipindi cha Miaka kumi ya mauaji makubwa ya wakristo chini ya mfalme Diocletian wa Kiroma.

Diocletian Aliona Ukristo unakua sana, na unasukumwa na watu wachache sana, na unahatarisha dola yake ambayo tayari ilikuwa na idadi kubwa sana ya Wapagani. Hivyo akaona ili aiunganishe dola yake, maamuzi mazuri kabisa, yatakuwa awamalize hawa wakristo. Kumbuka hata kabla ya kipindi hiki, tayari kuanzia enzi za mitume ambao wote waliuwawa na waroma, ukristo ulikuwa unalengwa kumalizwa kabisa. Na ndiyo maana unaweza kuona hata kabla Paulo hajauwawa, alikuwa akikutana na vipingamizi vingi sana.

Hoja ya msingi ambayo nataka kuieleza hapa siyo Historia, nataka kuonyesha mchezo au triki ya kamali ya akili. Mwanzo kabisa, Lusifa anataka kuwamaliza wakristo wote, hili tunaweza liandika kama:

Tatizo la Kwanza ‘’thesis’’: Kuwaua wakristo wote

Lakini Lusifa kumbuka sio kwamba ana akili nyingi sana, naye ni Mpumbavu tu. Lusifa anatumia faida ya taarifa na uzoefu kama nilivyoelezea awali, katika mbinu yake ya kwanza ya kutengeneza tatizo la kwanza, anafeli, kwa kuwa huwezi kuwaua watu wote wa Mungu, sio kuwa Mungu atazuia, ila watu wa Mungu wana haki ya kupewa ahadi ya ulinzi sawa na mapenzi ya Mungu. Na pia, Saikolojia ya wanadamu kwa namna ilivyo, kadri ambavyo unavyowaua watu, ndivyo wengine wanavyojifunza zaidi kuhusu hao watu, na kwa hivyo, utajikuta unachochea zaidi ajenda zao. Na kwa hivyo basi, Lusifa hakuwa na namna zaidi ya kutumia mbinu ya pili, ambayo hii sasa inakuja kama Ukinzani wa ajenda yake ya kwanza ‘’anti-thesis’’

Hatua ya Pili ‘’313-karne ya 9’’

Ukinzani ‘’anti-thesis’’; Tuungane na Wakristo na kuwapa uhuru

Hii unaweza kuiona kipindi cha miaka kuanzia 313, ambapo unamkuta sasa mfalme wa Roma ‘’Constantine’’ akijifanya kuwa naye ni Mkristo, na hapa sasa ndipo unapokutana na kukua kwa Upapa, huku Upapa ukipatiwa mamlaka na Dola ya Rumi. hazikuwa ni hatua za moja kwa moja, lakini ajenda kuu zilizokuwapo hapa, zilikuwa ni kuibua hisia za Umoja sasa, na kupingana na uhasama dhidi ya Imani ya Ukristo.

Lusifa anahama katika mbinu ya kwanza ya Kuua ‘’Joka’’, anaingia katika kudanganya ‘’nyoka’’, hii ni baada ya kugundua kuwa amefeli, na hawezi kuwamaliza wakristo. Anawezaje sasa kudanganya, anacheza na falsafa ileile, kwa mtu ambaye alikuwa hana uhuru, alikuwa hatiani kuangamizwa, anaposikia kuwa sasa anaweza kukubalika, kuheshimika, na hata kulindwa na Imani yake. Huwa anakuwa dhaifu sana kuweza kupingana na mithili ya nafasi hii.

Wakristo wengi sana wanajikuta wakiungana na mfumo wa kiroma, ambao unawapa uhuru wa kuamini, lakini uhalisia wake, unawachochea tena kuingia katika matatizo mengine.

Kumbuka, zama hizi zote zipo katika kipindi kingine kabisa cha kanisa la Mungu, zama za kanisa la smirna, Pergamo, na Thiatira. Na zama hizi hutambulika pia kama za Giza, ‘’Dark ages’’, ambapo hunukuliwa pia kuanza mwaka 538AD, mpaka miaka ya 1798. Katika zama hizi, Dola ya Rumi katika miaka ya 476AD, inagawanyika katika pande kuu mbili, mashariki, na magharibi. Huku magharibi ikianguka kabisa hata kutawanyika katika makundi mbalimbali ya makabila ya kijerumani ‘’germanic tribes’’, na ndiko huko hakukuwahi kamwe kuwa na utulivu, hata kupelekea baadaye kuibuka mataifa kadha wa kadha. upande wa mashariki ambao ndiyo uliokuwa ukishikilia pia nembo ya Ukristo, ulidumu kidogo ili kutengeneza taswira ya kielelezo cha Nguvu ya ukristo huu mpya ambao umepokelewa, lakini hata hivyo, nao haukudumu sana.

Zama hizi kunaibuka pia dola ya uislamu, kuanzia miaka ya 600’S, na Uislamu unakua hata baadaye kuunda dola ambayo inasambaa na kuteka maeneo mbalimbali, kuanzia Afrika, mpaka Sehemu kadhaa za Ulaya. dola ya uislamu inasambaa ikiwa pia na ajenda ya dini mpya ya Uislamu.  Kumbuka mwisho wa karne ya tisa, hata na dola ya uislamu pia inaelekea katika kuishiwa nguvu zake katika kuendelea kusambaa zaidi, lakini tayari ikiwa imeshasambaa maeneo mengi sana ambayo Ukristo ulikuwa umekwisha sambaa awali.

Triki ya Akili ya Lusifa

Watu wengi huchelewa kujua lipi lilikuwa lengo kuu la Lusifa enzi za zama za giza. Lusifa alikuwa na adui yake mkubwa sana, na ndiye adui yake wa nyakati zote, ambaye ni Kristo, na wafuasi wake. Sasa Lusifa hapa lengo lake lilikuwa ni kutumia chapa ya Ukristo, kuipatia Nguvu chapa yake, na kisha kuuruhusu Ukristo kuendelea kukua lakini yeye akiendelea kuwamaliza wakristo wakweli. Ambao sasa watakuwa wamebakia wachache sana, maana sehemu yao kubwa imekwisha chukuliwa.

Kutumia chapa ya Ukristo ilikuwa kupitia kuifanya Rumi kuwa imebatizwa, ilihali bado imejaa upagani. Kuipatia nguvu ilikuwa kupitia kuukabidhi mamlaka Upapa, na kutumia dola yake kusambaza zaidi dini hii mpya ambayo tayari upagani upo tayari kuipokea, kwa kuwa inasehemu kubwa zaidi toka kwao. Na mwisho, kuruhusu Ukristo kukua huku ukiendelea kuangamiza wakristo wakweli, hii ilikuwa kupitia njia ifuatayo;

Hakuna Fundisho lenye msingi wa Imani ya Ukristo zaidi ya kuwa, Kristo ni Mungu, na ndiye Njia, kweli, na Uzima, na alikufa, na akafufuka ili kumkomboa mwanadamu.

Mafundisho hayo unapotoa, au kupooza, hata moja tu, huo sio ukristo tena. Lusifa akilijua hili, katika zama hizi, anatumia mbinu mbili ili kufanikiwa;

Kwanza, Anaibua dini ya Ukristo wa Roma ambao anajua kabisa, katika Njia, anawekwa kiumbe mwingine yeyote yule, ila siyo Yesu, mfano, kila unaposikia, Mama maria utuombee, maana yake njia, au ‘’mediator’’, sio Yesu tena. Hii imeshaua Ukristo. Unapoweka kweli nyingine yeyote tofauti na maneno na Maisha ya Kristo moja kwa moja, mfano, unaposema Sabato ni jumapili, ilihali amri za Mungu zinaitambua kama Jumamosi, tayari unaweka kweli nyingine. Mfano wa mwisho, unaposema watu wanapokufa huenda katika sehemu yeyote ile, unamaanisha watu hawafi, maana yake unapingana na kauli ya Mungu aliyosema, Utakufa. Lusifa alimpinga Mungu kwa kumwambia Eva, hakika hautakufa. Na unaweza kumgundua Lusifa hapa, huweka Uongo, husema kuwa, Hautakufa, utaenda Mbinguni, au, utaenda kwenye mateso ‘’toharani’’, hii ni sawa na kupinga kuwa hata Yesu hakufa! Hoja yangu siyo kuzichambua dini hizi, lengo langu ni kugundua namna ambavyo triki hizi za akili zinavyofanya kazi.

Pili, Kuibua kwa dini ya Uislamu. Ijapokuwa wengi huwa hawachunguzi ukweli huu kiundani sana, maeneo mengi sana ambayo awali yalikuwa yameshamiri sana Imani za Ukristo, kama maeneo ya Afrika magharibi, na kaskazini, na hata maeneo kadha wa kadha ya nchi za asia na ulaya, yalikuja baadaye Kujawa na Imani mpya za uislamu. Hoja kubwa kuhusiana na Imani ya uislamu siyo kuwa ina mafundisho hatarishi, bali inajenga Imani kuwa Yesu siyo Mungu, wala Yesu siyo njia, kweli na uzima. Ijapokuwa anatambuliwa vizuri sana, lakini hoja ya msingi ya kutambua ni kuwa, kwa zama hizi zote za Giza, jamii nyingi sana ambazo zilikuwa zimekwisha kupokea Nuru ya Ukristo wa kweli, zikawa zikizidi kuipoteza, hii ni kutokana na kuwepo na kushamiri kwa makundi mengi sana ambayo yote, hayana nuru ya kweli ya ukombozi wa mwanadamu.

Hitimisho katika zama hii ya Ukinzani ni kuwa, Lusifa anatumia mbinu ya kutengeneza hatarishi nyingi sana katika dunia, zama hizi zinahusiana na hofu kubwa sana katika jamii za watu. Makundi kama makabila ya Goths, yaani ‘’Visigoths, ostrogoths’’, hawa walikuwa ni watu wa mapambano mfululizo, nao wakishindana na makundi mengine ya ‘’Huns’’, ambao hawa walikuwa ni majitu ya vita, na farasi, na walikuwa wakatili kwelikweli, walipelekea makabila mengi ya goths kusogea sana roma, na kuchochea zaidi dhiki, inakasemwa pia makundi haya ndiyo yalichochea sana hata kuanguka kwa dola ya roma, kulikuwepo pia makundi kama ya Vandals, ambao hawa walishindana sana na roma ya mashariki ‘’bryzantine empire’’, hawa walikuwepo mji wa Carthage, maeneo ya Tunisia, hata maeneo ya kuzunguka kanda yote mpaka miji ya spain. Dola za uislamu kuanzia kwa zama za ‘’Umayyad caliphate’’, mpaka ‘’Abbasid Caliphate’’, zilikuwa ni zama za dola kupambana, na kujitanua kivita.

Lengo, dhiki hizi zilitosha kuwasahaulisha watu ukristo wa kweli, na namna pekee ya kuendelea kuipeperusha bendera ya ukweli wa ukristo ilikuwa kupitia dola ya rumi ya mashariki, ambayo ilikuwa na ukristo wa roma. Na huko ndiko ulikwepo Uhuru, na Umoja katika kumwabudu Kristo. Lakini bahati mbaya, tayari ulikuwa ni mtego wa akili.

Hatua ya Tatu ‘’ karne ya 9 mpaka karne ya 14’’

Utii kwa Sheria ya Ukristo ‘’Upapa’’ ‘’new-synthesis’’

Hii ilikuwa ni mbinu mpya kwa zama hizi kwa serikali za roma, na upapa, lakini ilikuwa ni gemu ya akili ya Lusifa. alishatambua kwa idadi ya vizazi ambavyo vitakuwa vimeshapita, tayari atakuwa na kila uwezo wa kuikamilisha. Mpaka hatua hii dola ya Upapa ilishakuwa imepata nguvu mpaka mwisho. Na pia, dola ya upapa ilishakuwa imechukua nembo ya Ukristo kwa dunia nzima. Sasa dunia haikuwa na chapa inayoweza tambulika tena ya Ukristo zaidi ya Upapa. Na Lusifa alivyo mjanja hapa, akaweka mtazamo wa akili za wengi uwe aidha Ukristo ambao ndiyo Upapa, au Uislamu. Na ndiyo maana, katika zama hizi, kulikuwa na migogoro mingi sana kati ya wakristo, na waislamu, hasa katika kupambania ardhi iliyosemwa takatifu, ya mji wa Yerusalemu. Vita vingi sana vilipiganwa, huitwa pia ‘’Crusades’’, na pia kulikuwa na migogoro mingi sana, ambayo yote ingetosha kutomfanya mtu kukumbuka kuwa, Ukristo wa kweli ulikwisha kuwa umepotea mpaka hatua hii.

Mtego wa akili wa Lusifa

Lusifa anatumia Dola ya ukristo wa Roma kukubalika katika maeneo na jamii mbalimbali kama mjumbe wa haki, na anapata sana Nguvu huko. Kadri anavyopata zaidi Nguvu, huku akiwa juu sana kimamlaka, analazimisha jamii zote kutii na kukubaliana na mamlaka yake ambayo ina sura ya kidini, au wokovu wa kiroho. Kwa nje anapozidi kukubalika kutokana na dhiki ambazo watu wamekwisha choshwa nazo, basi yeye anachochea zaidi dhiki kwa kugandamiza zaidi watu, sasa  mpaka kiroho.

Unaweza kuelewa hili kwa namna ambavyo dola hii sasa hata Biblia tu kitabu cha Kristo mwenyewe hakitumiki, watu wakiagizwa kutumikia taasisi za kidini, wakihesabiwa haki kwa msamaha ambao kwa vipindi kadhaa iliwagharimu hata kugharamia kwa fedha, dola hii ilishindana sana na makundi waliyopingana nayo, na iliwaadhibu kwa adhabu kali sana hata kifo. Haikutenda kama Ukristo wa mitume, haikuvaa kama wakristo wa mitume, haikusema pia, ila ilijitambulisha kwa sura hiyo.

Unategemea kwa ukandamizaji huu wa upapa ambao vitabu kadhaa vimeandikwa kuelezea tu zama hizi za giza, mfano, ‘’The Two Powers: Upapa, Ufalme, na mapambano dhidi ya Uhuru ya karne ya 13’’ kimeandikwa na ‘’Brett Edward Whalen’’ kuna ‘’A short history of Papacy in Middle Ages’’ kimeandikwa na Walter Ullman’’’, kuna ‘’The Great Controversy’’, kimeandikwa na Ellen G. White. Kuna mamia ya vitabu wenda msomi mdogo anaweza Jifunza zaidi katika maktaba za historia za dunia, hasa zama za giza, mpaka kuinuka kwa marekani. ukandamizaji ulikuwa mkubwa sana, na matokeo yake, watu wengi sana wakaanza kuuchukia Ukristo.

Mpaka hapo watu wanauchukia Ukristo, na kumbe hata haukuwa Ukristo ambao kimsingi ulikuwa ukiwatesa. Hii ndiyo mitego ya akili ya lusifa. kwa mara ya kwanza anafanikiwa kutumia Hegelian Dielectric kutengeneza Chuki kuhusiana na Ukristo, huku bado hata Ukristo wenyewe ukiwa bado hauonekani.

Unajifunza nini kuhusiana na muda?

Kwa vizazi visivyozidi 50, kwa wastani wa miaka 30 kwa kizazi, au kama utatumia wastani wa miaka 70, basi unavizazi visivyozidi 20 tu, Dunia imeshaingia katika hatua mpya kabisa, ya Kuuona Ukristo kama ni Ukandamizaji, wakati awali Ukristo ndiyo ulikuwa Ukandamizwaji. Hii ni mbinu ya Lusifa ya mafanikio sana. Lakini hata hivyo, bado hili halikuwa lengo lake, hebu tuangalie hatua inayofuata.

                                            ZAMA ZA MWISHO ZA LUSIFA

Hatua ya nne ‘’ karne ya 14 mpaka 1798’’

Tatizo la kwanza ‘’thesis’’ : Hakuna Uhuru

Hapa Lusifa ameshacheza mchezo wake, anajua kwa kizazi hiki jamii ya watu lazima itaanza tena kuutafuta Uhuru. Kiukweli ni kuwa, watu hawawezi kuwa tena na historia kwa kipindi cha zaidi ya milenia hata wakaweza kujua awali ilikuwaje, na hivyo wote wanaozaliwa katika zama hizi, wanachojua ni kuwa Dunia haina Uhuru kutokana na mifumo yake, hasa ya dola ya Upapa. Na watu hawa wanajua kuwa ni ngumu sana kwa dola hii kuweza kutoka katika mamlaka yake, na ndivyo ambavyo marazote huwa inakuwa, awali dola huwa kama vile haziwezi anguka, lakini hapo ndipo hatua ya kuanza mzunguko mwingine huwa inaanza.

Katika zama toka karne hii ya 14, kuna ibuka matatizo mengi sana ambayo yanatokana na jamii kutaka kujitoa katika giza la ugandamizaji wa kimwili, na kiroho. Na hapa ndipo Dunia inaingia katika zama zinazoitwa zama za Nuru ‘’Enlightenment stage’’. Katika zama hizi, kunatokea mapinduzi yafuatayo.

Kwanza, mapinduzi ya Kifikra. Dunia inaanza Kujawa na watu wenye uhuru wa kifikra, ambao wanaamua kutumia akili zao katika kutaka kujifunza wenyewe, bila kuambiwa cha kujifunza, au kuaminishwa na mamlaka. Na hapa ndipo wanapoanza wanasayansi wakwanza kabisa wakubwa, kama vile kina Corpenicus, Keppler, Galilei, Newton, n.k. kiufupi hawa wote utakuta wakipingana na kweli nyingi sana ambazo awali zilikuwa zikiaminishwa katika taasisi kubwa hasa za dini. Mfano, hapa kunaibuka sayansi ambayo inathibitisha Dunia ni mviringo, ndiyo inayoizunguka jua, sayansi za afya ambazo zinasema Ukifa umekufa hakuna popote unapoenda, utakuta Isaac Newton akimtambulisha Papa kama mpinga Kristo, sayansi za ubongo zinazosema hakuna roho ya mtu iliyo nje ya ubongo, haya na mengine yote ni matokeo ya kuanza kwa nuru mpya ya maarifa, ambapo yanakuja kwa namna nyingine ya injili, ambayo unaweza iita sayansi.

Mapinduzi hayaishii hapa tu, watawa kadhaa kama Martin Luther kati ya miaka ya 1517 wanaanza kugundua Biblia ilivyo na Habari njema, ukweli ambao ulifichwa kwa karne nyingi sana. Anatafsiri Biblia na kuchochea tafsiri ya Biblia kwa lugha kadha wa kadha na kuzisambaza, haya yote yanachochea hisia za kugundua hata Mungu anataka Uhuru wa watu.

Triki baada ya kufeli kwa Lusifa

Lusifa mpaka hatua hii alikuwa amefeli kwa hatua kubwa sana. Maana malengo yake yalikuwa dunia iishi katika Dimbwi la Ujinga na upumbavu kama ilivyo asili yake kwa milele yote, lakini hakujua kuwa ilikuwa ni ahadi ya Mungu kuwa Nyakati za mwisho maarifa yataongezeka. Na Lusifa ilimgharimu sana kufikiria namna ambayo anaweza kushindana dhidi ya jamii hii kubwa sana ya watu ambao mpaka wakati huu walikuwa hawawezi kudanganyika.

Awali alifikiria kuwaua kama alivyofanya kwa Galilei aliyeuwawa kwa kufungwa na Waroma, au alivyoelekea kuwaua Wafuasi wengi sana wapinzani wake, au Waprostentanti, kuanzia wafuasi wa John huss, john Wycliffe, martin luther, john Wesley, john calvin, n.k. lakini marazote hubadili triki baada ya kuona kuwa hawezi kuikamilisha, na hapa ndipo alipofikiria njia zifuatazo ili kuzitumia kutengeneza hoja ya ukinzani.

Kuchochea Ukandamizaji wa Rumi mpaka mwisho makusudi

Unapoelekea karne ya kumi na saba, ambapo hizi ndizo zama ambazo katika Biblia lilipita kanisa la Mungu la Sardi. Kipindi hiki kilikuwa na ukandamizaji mkubwa sana wa kanisa la Roma maeneo ya Ulaya. Watu wengi huwa hawajui kwanini zama hizi zilikuwa na ukandamizaji uliovuka mipaka, kiufupi huu ukandamizaji ulikuwa ni makusudi, hii ni kwa kuwa, ulikuwa umelenga ajenda zifuatazo.

Kwanza, Ulilenga kuumaliza Uprostentanti ambao huo ndiyo ulikuwa adui mkubwa wa Lusifa ambaye alikuwa hataki kabisa Yesu ahubiriwe tena. Maana uprostentanti ulikuwa na kichwa cha ‘’Haki kwa imani, inayotolewa bure kwa neema, itokayo kwa Yesu Kristo aliye ni Bwana na Mwokozi wa Ulimwengu, yaani Mungu’’. Hivyo kutumia Nguvu mpaka mwisho kulilenga zaidi Muda, yaani, Lusifa alishajua mapinduzi ya maarifa yanayoenda kutokea yatakubaliana na Uprostentanti kama atachelewa au kuuachilia kukua katika vichwa vya watu. Na hivyo basi, akatumia nguvu zote kabla ya wakati mfupi ambao na katika Biblia ulishatabiriwa kuwa ni kipindi cha miaka 1260 tu, au miezi 42 tu, au toka 538-1798 ambapo atapewa mamlaka juu ya watu wa Mungu katika zama za giza.

Hivyo mateso makubwa, mauaji makubwa ya waprostentanti, tena wakati mwingine kuyachanganya hata na mauaji ya wachawi ‘’witch trials’’ kama ya salem, yote na hila zote zililenga tu kuwamaliza wakristo wa kweli. hili lilikuwa lengo lake kubwa sana la wakati. Na alifanikiwa kwa kiwango kikubwa sana, lakini hata hivyo bado hakumshinda Yesu, hivyo Lusifa alikuwa na mbinu ya pili hapa.

Ilikuwa ni kuwakera sana wanasayansi na watu wa maarifa wapya wa zama za nuru, kwa kuufanya Ukristo kuonekana na dini ya ukandamizaji, ukatili, na inayoshikilia mafunzo yasiyo na uhalisia. Na kwa mantiki hii, wasomi wengi sana ambao hawakuweza kujifunza Ukristo wa kweli ambao waprostentanti waliokuwa wameubeba walikimbia, waliishia kuchukia Imani ya kikristo, wengine wakiichanganya na falsafa mbalimbali za kubuniwa, kumbuka Ulaya ilishakuwa na vyuo vingi kuanzia miaka ya 1100, na kuendelea vyuo kama Oxford, Cambridge, n.k.

Kadri wasomi wengi walivyozidi kuuchukia Ukristo, au Upapa, ndipo walipoanza Kujawa na tamaa ya kutamani Uhuru wa kifikra, bila kubanwa na hisia zozote zile za kuambiwa kuabudu Mungu.

Mafanikio ya Lusifa

Katika kitabu cha Historia na Kiini cha Magonjwa, na kitabu cha ‘’Ubongo wa mtu mweusi’’ nimeonyesha namna jamii nyingi za ulaya zilivyoanza kuendelea sana, toka mwanzo wa shughuli za kilimo, hata kiviwanda. Mafanikio makubwa yalitokana na dhiki ambazo zilitengenezwa na jamii nyingi sana nyuma yao, na hata teknolojia nyingi zilikuwa sana kutokana na mitindo yao ya Maisha, ambayo ilichochewa na shughuli zao za kimaisha, na hata tabia zao za nchi za kijiografia. Hoja ni kuwa, Lusifa alifanikiwa sana kuchochea Heshima kubwa sana kuhama toka kwa viongozi wa dini ambao walikuwa wake, na aliwachafua, hata kuhamia kwa wanasayansi na wanateknolojia wengi, ambao hajawatengeneza, ila amewatengenezea mazingira ya wao kuwa upande wake bila wao kutaka.

Na hii ndiyo sababu utakuta wasomi wakubwa wengi sana wa awali, wanaanza na Imani za kutoamini Mungu, huku wakichochea sana hisia za  kutaka Uhuru. Wengi wao ilikuwa ni haki yao kutamani Uhuru. Na Uhuru ndiyo tatizo la kwanza katika zama za mwisho za Lusifa kama kichwa cha sehemu hii kinavyosema.

Lengo la mwisho la makusudi kabisa katika hatua hii ya kwanza, Upapa uliongeza Nguvu makusudi, ili kuchochea Kukua kwa taifa la Marekani. Taifa la marekani lilijengwa kwa misingi ya Uhuru wa kiuchumi na kidini. Taifa hili ambalo ndilo lilionekana kama tumaini pekee la waprostentanti waliokuwa na matumaini hafifi sana kwa ulaya, lilianza kuchochewa kwa safari nyingi sana za watafuta Uhuru kulielekea, lilipata Uhuru zama hizihizi. Lusifa alikuwa amepanga mbinu kubwa sana kupitia taifa hili, alipanga kupitia taifa hili awakusanye waprostentanti wote, kiwe ndicho kitovu cha uprostentanti duniani, halafu katika ardhi mpya sasa, awamalize wote hatua kwa hatua kupitia teknolojia na falsafa mpya ambazo, atazifanikisha kupitia kikundi cha wafuasi wake anaoshirikiana nao katika uharibifu. Unaweza kusoma pia Q4 kuelewa namna teknolojia na falsafa za ukana Mungu zilivyosambaa sana katika nchi ya marekani hata kuathiri kabisa maadili, lakini hata hivyo lengo kamili bado lusifa hajakamilisha, ila mpaka mwisho wa sura hii, tutaona ameshakaribia kabisa kulikamilisha.

Hatua ya tano ‘’ 1798- karne ya 20

Ukinzani: Uhuru wa Kifikra, hakuna Mungu

Hili ndilo lilikuwa lengo la Lusifa katika kipindi hiki cha wakati. Alichotaka Lusifa ionekane hakuna Mungu, na kuwa, Mungu gani angeweza kushughulika na wanadamu katika namna ya Hovyo kama mamlaka za dini zilivyokuwa zinafanya kama huyo Mungu alikuwa na mamlaka kubwa kabisa ya kimaarifa.

Lakini mafanikio makubwa sana ya jamii za watu katika hali zao za uhuru bila Imani kwa Mungu, huku jamii za wenye Imani ambazo zikitumika kama kielelezo cha Imani zikionekana dhaifu kabisa, kulichochea wengi kudhihaki Imani za Mungu kama hali dhaifu kabisa za kimaendeleo ya kiakili. Jamii kubwa za watu wanaoheshimika kama wanasayansi, wanafalsafa, waandishi, matajiri, wafalme, n.k. wote wanasukumwa zaidi katika ukana Mungu wakiwa na Nuru mpya ya wokovu toka kisima cha Ugandamizaji wa uhuru wa kifikra na kimwili.

Kumbuka Ufalme wa Kipapa ulipigwa chini kwa Nguvu kubwa sana ya mapinduzi ya ufaransa ya Napoleon, aliyefanikiwa kumteka papa mpaka kufa miaka ya 1798. Zama hizi ziliambatana na mapinduzi katika nchi nyingi sana, kama mapinduzi ya marekani, Serbia, spania, filipino, n.k. dunia ilipitia zama za mabadiliko makubwa sana. Ufaransa ilikuwa kitovu cha Uhuru wa kifikra toka kwa upapa, na hii ni kutokana na kuwa, ndiyo iliyokuwa imempokea papa kwa nguvu kubwa zaidi.

Mapinduzi haya hayakuwa kweli yakimaanisha kuwa ndiyo ulikuwa mwisho wa ukandamizaji, na falsafa za kipapa!! La hasha, ilikuwa tu ni namna ambayo jamii ilibadilishwa toka katika mfumo mmoja, Kwenda mfumo mwingine. Na ilikuwa ni namna ambayo mamlaka ya papa ilipaswa kugharamia nguvu kubwa sana jambo ambalo lilihusisha migogoro iliyopelekea hata kuuwawa kwa papa.

Kipindi hiki sasa Marekani ikawa ikizidi kukua kiuchumi na kiteknolojia, hasa ikifyonza sana kutoka kwa Ulaya. Marekani ilikuwa ni kiini cha demokrasia, au uhuru kwa dunia yote. Marekani yenyewe inatambulika kabisa kuwa ilichochewa sana na taasisi nyingi sana za siri ambazo zilikuwa zikihusiana moja kwa moja na mamlaka ya upapa. Lakini bado sura na umbile la uhuru lilikuwa ni namna ya kucheza na muda na nyakati ikivuta akili za wakimbizi wengi ambao walikuwa wamechoka.

Kumbuka sio kana kama Lusifa hakuwa na shughuli kubwa sana na mataifa ya mashariki, na Afrika. La hasha, Lusifa anajua siku zote ukimpiga Mchungaji, Kondoo lazima watatawanyika. Lusifa aliwekeza sana kwa kila sehemu ambayo waprostentanti waliweka kambi, lusifa asingepoteza muda na jamii kama za wahindu, au wabuddha, au wapagani, au hata waarabu, ambao kwao hao wote, tayari misingi mikuu ya Ukristo ilishapotezwa. Alihangaika sana Ulaya na marekani ambapo hata teknolojia nayo ilikuwa ndiyo iko katika kilele. Kumbuka hata maendeleo makubwa sana ya kisasa ya teknolojia ya viwanda, yalianzia Uingereza, kisha ulaya, na baadaye  marekani. Inatambulika China kuwa na teknolojia kubwa sana mpaka karne ya 14, lakini haikudumu kwa kuwa haikuwa na falsafa za Kikristo, na uhuru, kama zilivyokuwa nchi za ulaya. Na hata migogoro kama falme za Mongoli zinaaminika kuidhoofisha sana china kwa zama zake za awali za maendeleo.

Miaka ya karne ya 19 inaanza na kuisha na jamii kuanza kutumia mitaala ya elimu ambayo haimtambui Mungu. Wanasayansi wakubwa kama Einstein wanaibuka kuelekea karne ya 20 wakiwa na Mungu wao katika Imani ya kipagani ‘’Pantheism’’, ambapo ni sawa tu na kutoamini Mungu. Falsafa za ujamaa na mapinduzi ya Urusi yanachochea zaidi ukana Mungu, huku kuanzia miaka ya 1920’s na kuendelea shule zikianza kufundisha kutokuwepo kwa Mungu. Nadharia kama za Charles Darwin za miaka ya 1859 zikianza kufundishwa mashuleni, na nadharia nyingine nyingi ambazo unaweza kuzisoma vizuri katika kitabu cha injili ya sayansi Q3, zote zinaonyesha dunia sasa ikijawa na ukana Mungu, na Yesu akipotezwa kabisa kwa namna ya kisasa sana.

Lengo la Lusifa

Lusifa alitambua kuwa katika mfululizo wa kinabii wa Biblia, wa kitabu cha Danieli, wa miaka 2300, na makanisa saba ya kitabu cha ufunuo wa Yohana. Yote iliishia mwaka 1844, na kufanya miaka baada ya wakati huu kuwa ndiyo wakati wa mwisho kabisa wa ulimwengu. Na kwa mantiki hiyo, alijua kuwa ijapokuwa atawafanya watu wengi sana kuwa Pamoja naye kwa mantiki ya ukana Mungu, au ukinzani dhidi ya uprostentanti wa kweli, lakini hataweza kuzuia mpaka mwisho ukweli huu. Hivyo njia ambayo aliitumia, ni kutumia hatua hii kujiandaa na hatua yake ya mwisho kabisa. Na hapa anatumia njia zifuatazo:

Kukandamiza Mpaka mwisho Ukristo

Lusifa kupitia sera zake za Uhuru na Demokrasia, anawachochea watu kuamini wanaweza Kutenda lolote lile bila mipaka ya maadili. Na huu ndiyo msingi wa kuanzishwa kwa chama kama cha ‘’Domecratic’’ cha Marekani, ambavyo hivi, huruhusu kila tendo na hisia ya tendo la mtu, endapo tu, halimuathiri mwingine moja kwa moja. Kwa hawa matendo kama ya Ushoga ‘’LGBTQ’’ sio changamoto, ukahaba, mapenzi kabla ya ndoa, lugha za matusi, matumizi ya pombe, sanaa za uchafu, n.k.

Lengo la lusifa hapa lilikuwa tu ni kuwaumiza wakristo wengi wa kweli, ambao hata wanapokuwa pia wakienda katika taasisi za elimu, bado hudhalilishwa kuwa ni watu wenye uelewa mdogo zaidi kifikra. Mafundisho ya kuwa hapo zamani binadamu alitokana na sokwe, au ujiuji wa volcano, n.k. huchochea sana hisia za maumivu kwa wakristo wengi. Lusifa amekuwa akifanya hivi makusudi akilenga hatua ifuatayo ambayo tutaiona.

Pia hatua hii ilihusisha vikundi mbalimbali vya watu maarufu ambao wanaheshimika, na wana mafanikio sana kwa nje, lakini wana ajenda nyingi za kuwafundisha watu kuwa hakuna Mungu. Unaweza kuona hili kupitia wasomi wakubwa wa maarifa ya sayansi kama kina ‘’Neil de grasse Tyson, carl sagan, lawrence krauss, brian cox, sam smith, Richard Dawkins, michio kaku, Richard feynamn, ‘’n.k. pia wasanii wengi maarufu wa miziki ya vizazi vipya huwa ni wenye makufuru sana, wakifanya machukizo mengi sana kimaadili ya kikristo, kiufupi Lusifa aliye nyuma ya taasisi karibia zote za burudani huwahi kuonyesha uchafu wake ili kutengeneza chuki kwa wakristo, lakini haya yote ni malengo ya mchezo wake huu  wa akili.

Lusifa katika zama hizi pia anafanikiwa kuanzisha Uhuru wa vikundi vingi sana ambavyo navyo vinajitambulisha kwa sura ya ukristo, lakini havina hata nukta ya ukristo, au wakati mwingine vikiwa vya ukristo lakini vina nukta nyingi sana za upagani. Lengo la lusifa ni kupiga miluzi mingi ili kumpoteza mbwa, huku akiwa na lengo la kuwakusanya wapiga miluzi wengi zaidi katika mwisho wa wakati.

Kufeli kwa Lusifa

Lusifa katika karne ya 19 miongoni mwa vitu alivyofeli sana ilikuwa ni ukoloni. Lengo lake la awali lilikuwa ni kutawala dunia, huku akiuchafua zaidi ukristo kwa kuutumia kama mbinu njema ya kuwafikia watu, na baadaye kubadilika na kuonyesha ukandamizaji wa kikoloni. Lakini matokeo yake, ukoloni ulifungua nuru kubwa sana ya maarifa, na Mungu aliutumia sana Ukoloni kuwafungua waafrika wengi kimaarifa ya teknolojia, na Mungu wa kweli. huu ni miongoni mwa mfano ambao lusifa alifeli kwa kiwango kikubwa sana, njia ambayo Lusifa alibakiwa nayo, ilikuwa ni namna nyingine ambayo tutaiona, namna hiyo ndiyo huitumia zaidi kwa kuwateka waafrika wengi kiakili kama alivyofanikiwa.

Hatua ya sita ya Lusifa na ya mwisho ‘’2015-2031±’’

Utii kwa Sheria ya Kikristo ‘’upapa’’ -New synthesis’

Lusifa anatambua huwezi kutetea uhuru kuwa watu wanapaswa kufanya lolote katika mahakama ya haki na maarifa, utaonekana tu ni mpumbavu. Na Lusifa anatambua kuwa kama ataendelea kuruhusu uhuru huu wa watu kuamua kuwa mashoga, au kuwa wakristo wa kweli, baada ya muda mfupi watakaobadilishwa wengi zaidi ni mashoga, kwa kuwa Maarifa yana Nguvu kuliko upumbavu. Hivyo basi, namna pekee ambayo anaweza kufanikiwa hapa, ni kutengeneza upande ambao utaonekana ukishikilia maadili, kama ilivyokuwa kwa Upapa wa rumi ya awali, lakini sasa upande huu uwe kisiasa zaidi.

Na huu ndiyo mwanzo wa kutengeneza vyama kama vya ‘’Republicans’’ vya marekani, ambavyo ni kopi ya Republicans ya Rumi za zamani. Vyama hivi vina ajenda ya kufanya maamuzi ya kimaarifa, yanayosimamiwa na watu wachache wanaoaminika na jamii, watu wenye elimu na sifa njema, wenye kumjua na kumuamini Mungu, na watu hawa sasa ndiyo husimamia moja kwa moja maamuzi wakiwakilisha nchi zao, kwa mujibu wa sheria, na wakitumia mamlaka za nchi.

Mpaka mwaka 2024 unapoishia, unaweza kuona uchaguzi wa marekani ambao unawakutanisha Donald Trump wa Republicans na Kamala Harris wa Democrats, ukidhihirisha kabisa mtego wa Lusifa. Kamala anasapotiwa sana na wasanii wengi ambao wanaonekana watu wa hovyo, wasio na maadili, hawana heshima kwa Mungu, na hata chama chao ndicho kinachoonekana kuhusiana sana na kutetea haki za mashoga. Lakini kwa upande wa Trump unaweza kuona akisapotiwa na watu wengi wa maarifa na kuheshimiwa, kama Ben carson, Elon musk, viongozi wengi na wakristo wengi sana, na hata Trump mwenyewe baada ya Kupita anaonyesha moja kwa moja kutokubaliana na tabia za Ushoga, hata kutoitambua jinsia ya ushoga. Watu wengi huishia kuhisi wenda Trump ana ajenda za ukristo, lakini ufuatao ni mtego wa akili wa lusifa.

Kumbuka awali tuliona kuwa jamii kubwa za watu zilichoshwa na mwongozo wa dunia isiyo na maadili, dunia iliyojaa migogoro kama vita ya kwanza ya dunia, na ya pili. Mapinduzi yasiyo na mwisho, mabomu ya nyuklia, milipuko ya magonjwa, kukosekana kwa amani, kukithiri kwa ujambazi na wizi, kushamiri kwa mauaji ya Watoto na ndoa na mimba za utotoni, na kila aina ya matatizo. Mfumo wa uhuru usio na maadili unaonyesha kuwa na kero kubwa sana kiasi hata cha kuonyesha kuwa sababu kwa migogoro kwa baadhi ya nchi kama za Russia, ambazo zinaonyesha zikipambana sana hata kuingia katika vita ili kutetea maadili yao. Mabadiliko ya hali ya nchi na majanga ya asili yanaonekana kuchochewa sana na dunia isiyo na kiongozi wa maadili, hasa kutokana na watu kutupilia mbali ukristo, na kuukandamiza.

Haya na mengineyo mengi sana, yanapelekea sasa jamii kubwa sana ya watu kuinuka na kukubaliana na ajenda za kuuinua tena Ukristo juu, tena katika dunia ya kisasa zaidi. Na hapa ndipo tulipofikia mpaka mwaka 2025, jamii za wakristo zinazidi kupata nguvu huku zikizidi kuungana na kutengeneza umoja mmoja ambao una nguvu kutokana na kupatiwa ulinzi na mamlaka toka katika mamlaka kubwa kabisa.

Kosa kubwa sana wanalofanya watu wengi ni kusahau kuwa hii ni hatua ya mwisho ya mzunguko uleule ambao tulikwisha kuuona mwanzoni.

Lengo la Lusifa

Kuunganisha jamii zote za wakristo kwa mara nyingine tena. Na mara hii kiongozi wake akiwa tena papa kama ilivyokuwa awali, lakini kwa mgongo wa kisiasa za marekani inayoungana na nchi za ulaya, ambapo itaonekana kana kama nguvu za mamlaka ya upapa zinatokana na maamuzi ya watu wenye busara ambao wanachochewa na wakristo wenyewe moja kwa moja, na watu wenye mapenzi mema na sayari ya dunia, wanaotaka kuilinda dunia, na kulinda tamaduni njema za kila jamii.

Ajenda ya mwisho ya Lusifa

Ajenda ya mwisho ya Lusifa ni kuwaunganisha tena wakristo wote, na wanadini wengine wote ulimwenguni bila kujali Imani zao na itikadi zao. Na kisha kuwashawishi kuwa inapasa jamii yote ya wanadamu kulenga kuikoa dunia dhidi ya majanga ya asili, majanga ya kimaadili, na majanga ya kiuchumi. Na hili litafanikiwa kupitia kuwa na siku moja ya kuabudu ya Jumapili, ijapokuwa ni kana kama ni hoja nyepesi sana, lakini Lusifa anatambua kuwa kwa kutumia siku ya jumapili ili kuilinda sayari na kuabudu, tayari ameshabadilisha siku ya kweli ya kumwabudu Mungu, na anacholenga ni kuwa, kwa siku sita Mungu aliumba, na hivyo basi, kama unaweza kuamini Kuwa Mungu  ni mwumbaji, basi unapaswa kuabudu siku ya sabato, ambayo Biblia inaitamka kama ‘’Alama ya watu wa Mungu’’ rejea Ezekieli 20:20.

Kwa kutoabudu siku ya sabato ya kweli, maana yake aidha hawaabudu kabisa, au wanaabudu katika siku isiyo sahihi. Haimaanishi kuwa wasioabudu sabato hawako katika macho ya Mungu, lakini yapo maarifa ili kuwafundisha wabadili baada ya kujua, maana neema ya Mungu ipo wazi kwa kila mwenye kuamini baada ya kujua, kutambua hili tayari ni neema, na hata kabla ya kutambua Mungu alishatupenda ndiyo maana akatufundisha. Lakini hoja hapa ni kuwa, Lusifa analenga ibada ya jumapili kwa wote duniani, siyo wote waende kanisani, ila wote wapumzike au wafanya ibada zao.

Unaweza jiuliza kwanini Jumapili? Awali nilisema Lusifa anaumwa ‘’OCD’’ akitamani sana ibada. Kwake anatambua watu wanapoabudu sabato wanamwabudu Mungu. Na hivyo kwa kuwa anatamani sana ibada, suluhisho kwake ni kutengeneza siku ambayo haitakuwa siku ya Mungu ya ibada, na kila atakaye fanya ibada hiyo, ibada itaelekea kwake yeye. Hii unaweza thibitisha kwa asili ya siku ya jumapili, ambayo ni siku ya kwanza ya juma, ambayo zamani ilitumiwa na wapagani kuabudu Jua, na Lusifa kwa kuwa hajabadilika, bado malengo yake ni yaleyale, ila amekuwa tu akibadilika namna ya kuyafikia.

Akilini mwa Lusifa

Anachojua Lusifa na wafuasi wake ni kuwa, kwa namna ambavyo sheria hii ya jumapili inaenda kupitishwa kama ilivyoanza kujadiliwa katika bunge la marekani, watu wote itawapasa kukubaliana na agizo hili jipya. Watu wengi huisi wenda kutakuwa na ukinzani mkubwa sana toka jamii za wayahudi, na waislamu. Lakini wengi wao hawataamini, kwa kuwa tayari kuna uhusiano mkubwa sana kati ya jamii hizi zote. Wayahudi wengi waliopo palestina ni mithili ya Watoto wa marekani kwa wanaofahamu historia wote, lakini pia wanahistoria wengi sana hutambua mkono mkubwa sana wa rumi juu ya uislamu tangia awali kabisa miaka ya karne ya saba, ni mithili ya mbegu huru lakini ina matunda yaliyopangiliwa awali sana, ukiondoa fundisho la Kristo siyo Mungu, wala hakufa na kufufuka kama inavyoaminiwa na wakristo, sehemu kubwa sana ya waislamu huwa hawapishani sana na wakristo, na hasa, pale wakristo wanapofunika Biblia, na kuongezea vitabu vyao.

Jamii kama za buddha, hawa hawana Mungu Muumbaji katika Imani zao, jamii kama za wahindu, hawa ni kama wapagani wenyewe waanzilishi wa roma, tena kibaya zaidi, jamii kubwa sana ya waprostentanti wamesharejea katika mafundisho na mitindo ya awali kabisa ya Roma, ya kutopendelea kuisoma, au kuichunguza Biblia. Na hivyo basi, kwa kiwango kikubwa sana cha dhiki ambapo jamii hizi zote za kimaadili zimezipitia kwa hatua ya tano, zote zinaenda na zimeshaelekea kabisa kukubaliana katika kila ajenda kutoka mamlaka ya juu, ambayo ni mjumuisho sasa wa pande zote. Ukweli ni kuwa, ni papa ndiye mtawala hata katika hatua hii.

Lusifa anajua sasa anaenda kuwa na kundi kubwa sana la watu waliochini yake, na anajua watu hawa wote ambao watakubaliana na kuabudu Jumapili, watadharau sana hoja dhaifu kama ya kuwa walipaswa kuabudu jumamosi kwa kuwa ni siku ya saba ambayo Mungu alipumzika. Na watu hawa watadharau kwa kuwa, kwa kadri ambavyo wataangalia dhiki kubwa walizotoka, na ukilinganisha na changamoto ndogo sana ya siku ambayo haina hata mantiki, wengi wataona wapinzani wa umoja huu kama watu wenye misimamo iliyokithiri, misimamo hatarishi ‘’extreme fundamentalism’’.

Kumbuka, ni kikundi cha watu wasiozidi asilimia 0.3% tu ambao wanaamini na kuliishi neno la Mungu kama lilivyoandikwa katika Biblia, yaani kwa zote 100%. Ukisoma katika Ufunuo wa Yohana 12:17, unaweza kuwatambua watu hawa kama watu wazishikao amri za Mungu, na kuwa na Ushuhuda wa Yesu, ambapo katika sura ya 19:10, ushuhuda wa Yesu ndiyo Roho ya Unabii, ambayo huwasaidia watu hawa kuweza kumshinda Lusifa kwa kuwa huwa uwezo mkubwa sana wa kuelewa mbinu zake.

Lusifa huwachukia sana, na hata watu wengi wa duniani nao huwachukia watu hawa. hii ni kutokana na tabia za watu hawa, za kujiona kana kama wapo sahihi sana. lakini hoja ni kuwa, watu huangamia kwa kukosa maarifa. Baada ya jamii kubwa sana ya watu kuungana kwa Pamoja, mamlaka zitakuwa na Nguvu sana katika kuwagandamiza watu hawa, kwa kuwa jamii tayari itawaona kuwa ni kinyume nao. Na kumbuka, Dunia baada ya kuungana itaonekana kana kama ipo katika nyakati za amani kabisa kuwahi kutokea, lakini hapo ndipo mwisho utakuwa umefika, hii ni kuwa kuwa:

Majanga mengi sana yatakayoanza kutokea tena, yataonekana ni kana kama ni matokeo ya laana inayotokana na kikundi kile kidogo cha watu kukataa kuungana na wenzao, na hivyo jamii kubwa itaaminishwa kuwaona watu hawa kama watesi wao. Sehemu kadha wa kadha katika dunia wameanza kutumia adhabu ya kunyonga waasi kama namna bora zaidi ya kupambana na waasi waliokithiri. Lakini ukweli ni kuwa, adhabu kali zitaanza kutolewa na jamii za watu dhidi ya makosa makubwa yanayofanywa na watu baadhi walio kinyume na sheria, na jamii.

Biblia katika kitabu ambacho watu huwa hawakisomi kabisa cha ufunuo wa Yohana inaonyesha kuwa, kutaambatana na majanga mengi sana ya asili ambayo yatakuwa ni mapigo saba ya Mungu, hakitakuwa kipindi kirefu sana, maana kadri mapigo haya saba yatakapo kuwa yakishuka, lengo halitakuwa kuwaadhibu watu, lengo litakuwa ni kuwa, kwa kuwa mliungana mkisema dunia ina majanga mengi ya asili, ilihali majanga yenyewe mliyatengeneza nyie wenyewe, na mkawatesa watu wa Mungu kuwa ndiyo chanzo cha majanga hayo, sasa myapate mliyoyataka.

Dunia itakuwa ikipitia nyakati hatari sana na hasira za watu wote zitawaelekea kikundi kile kidogo cha watu wanayoitii kweli yote, jamii itasukumwa kuwamaliza kabisa, na jambo hilo litachochea sana dhiki, kipindi hiki huitwa pia dhiki kuu. Na katika kipindi hiki, watu wengi hata ambao hawakujua ukweli wa Mungu wote, watajifunza kwa kasi sana, na wataelewa hata kujikuta na wao wakiingia tena katika dhiki hii. zipo hatua kadha wa kadha katika zama hizi, lakini hatma yake ni kuanguka kwa falme kubwa, na hata jamii kuunganishwa tena kuelekea kuwamaliza kabisa watu wa Mungu, jambo ambalo litaishia kwa Ujio wa Moja kwa moja wa Yesu.

Lengo la kuandika sehemu hii ni kuonyesha kuwa, ni mithili ya nadharia za kufikirika ‘’conspiracy theory’’ kuhusu ujio wa yesu, lakini nadharia za kweli za kufikirika ndizo zilizojaa upande wa pili wa wasioamini, kama ujio wa Aliens, au wafu waliofufuka. Hoja ya msingi  ni kuwa, Lusifa yupo katika hatua yake ya mwisho ambayo anatumia tena mbinu ileile kama ilivyofanyika awali.

HITIMISHO

Sehemu hii yote imelenga kuonyesha mbinu kuu ya kwanza ya Lusifa ya kucheza na akili za watu, kwa kutumia faida yake katika muda, na udhaifu wa wanadamu katika muda. Lakini pia, kutumia triki yake ya Hegelian dielectric kucheza na akili za watu. Lusifa ametumia mbinu hii mara ya kwanza akafanikiwa, na mara ya mwisho akiitumia mpaka hatua ya mwisho kabisa aliyofikia, na nimeelezea hatua aliyoifikia, anapoelekea, na itakavyokuwa. ili kila mmoja akutane na neema hii ya maarifa baada ya kusoma sura hii.

Sehemu zinazofuata tunaenda kuangalia mbinu nyingine kubwa sana za lusifa za kucheza na akili za watu, na kuweza kuwa na mafanikio makubwa sana mpaka hatua hii ya wakati tuliyoifikia.