LUSIFA DHIDI YA KAZI #4
LUSIFA DHIDI YA KAZI
Kama Nyoka
Lusifa kwa karne amekuwa akiwachochea watu
Kwenda kinyume na malengo makubwa ya kazi, na mashine. Lusifa anajua amri ya
Mungu inawataka watu kufanya kazi kwa siku sita, na siku ya saba kupumzika.
Huwezi pumzika bila kufanya kazi, kazi imepewa kipaumbele kwa asilimia zaidi ya
85% katika maisha ya mwanadamu. Mwanadamu anapofanya kazi, ndivyo anavyozidi
kuishi bora kiuchumi, na kiafya. Mwanadamu anapovunja tu sheria hii, huwa
hatiani kwa kila aina ya matatizo.
Lusifa huwajia watu na triki ya kuwasaidia
wapunguze kazi kama namna bora kabisa ya maisha. watu bila kujijua hukimbilia
sana kazi rahisi, ambazo huwa zimerahisishwa na watu wachache sana waliofanya
kazi ngumu sana. Kwa kupenda mitindo rahisi kimatumizi ya misuli, utokaji wa
jasho, hatari za changamoto, watu huisi wanaweza kukimbia Laana ambayo Mungu
aliitoa Edeni kwa wazazi wetu wa kwanza, lakini madhara yake hujikuta wakipatwa
na matatizo makubwa zaidi hata ya Laana ile rahisi sana ya kutokwa na jasho, na
kupambana na miiba, au kuzaa kwa uchungu.
Mashine zimetapakaa katika ulimwengu wa
ubinadamu, lakini ajabu ni kuwa, mashine hizi nyingi hazitumiki kuwasaidia
wanadamu wengi zaidi, bali kuwainua binadamu wachache sana. Teknolojia na
taaluma kubwa za mashine zipo chini ya nchi kubwa sana zilizoendelea, ambapo
huficha taaluma hizo na kuwafanya wengine kuwa wateja wa bidhaa zao, na
kuchukua nafasi za vijana wao, viwanda vimesheni silaha za kuhatarisha maisha
ya watu, idadi kubwa ya teknolojia zinawaondoa watu toka mazingira yao ya
asili, na kuwaingiza katika mazingira mapya hata kifiziolojia. Watu wamekuwa
sio wakufikiria tena nje na wanavyoviona, maana kazi wanazozishuhudia nyingi ni
kazi za watu, zilizojaa siri nyingi na historia pana sana.
Kwa kawaida Ubongo huwa unakimbia matumizi
ya kazi ‘’Procrastination’’, ili kutunza nishati yake. Na ndiyo maana mwili
huwa unapenda kula na kulala au kubebwa, na haupendi kazi, kuoga na kufikiri.
Mwili haupendi kazi, ila unaihitaji kazi ili uweze kuwa imara. Na sasa basi,
Lusifa hutumia huu udhaifu kuwatriki watu wengi. watu wengi wangependa kazi za
kukaa tu chini, au kutumia nguvu kidogo sana.
Matumizi ya Roboti ‘’Robotics’’, na Akili
za kisasa ‘’Artificial intelligence’’, yamezidi kushamiri, watu wakiwa hawataki
hata kufikiria. Wakiamini wanaweza kupata majibu ya matakwa ya akili zao kwa
kuuliza tu. Lakini kila kilichomo katika mashine hizi, ni taarifa iliyokwisha
kuwepo, mwanadamu anapaswa kusogea mbele kila wakati, ni lini mwanadamu huyu
ataenda mbele kama kila anachotazamia ni kilichokwisha fanyika. Lusifa
anatambua anapaswa kumrudisha mwanadamu kwa gharama yoyote ile, kurejea katika
upumbavu wake wa awali. Wanafunzi hawajichoshi tena kusoma historia kama
zamani, wengi wapo juujuu sana kimaarifa. Hata hawaelewi Mashine hizi
zimetengenezwa kwa ajenda maalumu. Majibu mengi kutoka mashine hizi huwa na
falsafa za ukana Mungu, na itikadi za ukoloni wa kiakili. Zimetengenezwa kuchochea uabudu wa mifumo, serikali, na watu
baadhi, kuliko maarifa ya kweli, na Mungu na watu wake.
Watu wa kawaida wengi huona Fahari sana
kumiliki magari ya kifahari, ndege, silaha, mashine za kisasa na thamani, n.k.
lakini wengi wao ni wapumbavu sana hata kushindwa kujua kuwa dhumuni la mashine
hizo sio kubadilisha matumizi ya viungo kutoka kutumika, hata kutulia, bali ni
kusaidia pale viungo vyao vinapokuwa vimefikia kikomo cha uwezo wa kutembea.
Yaani, dhumuni la gari, ni kukusaidia utakapokuwa umeshatembea vyakutosha hata
kushindwa kuendelea zaidi, lakini bado unahitaji kufika mbali zaidi. Gari lipo
kukuwezesha kufika miguu yako itakaposhindwa, sio kutumika pale ambapo miguu
ingepaswa kutumika. Lusifa amezidi kuathiri watu kwa kuwafanya kuhisi thamani
za mashine zao, ni uwezo wao mkubwa wa kiuchumi wa kuweza kuzilimiliki, na sio
dhumuni la kuwasaidia kufikia malengo yao. Na hapa ndipo utakuta mtu mmoja akimiliki magari 100, huku majirani
zake wakiwa hawana hata baiskeli. Huyu kwake magari, ni Fahari. Matajiri wengi wamekuwa wakiishi maisha ya
hovyo kabisa, wakiwa hawana amani kama walivyo tu watu wasio na uhakika wa
kupata mlo hata mmoja kwa siku. Lusifa amewavisha mavazi ya heshima na utukufu
kwa nje, lakini kwa ndani amewajaza maumivu, mateso na majuto.
Lusifa ameondoa ukweli juu ya dhumuni la
kazi. Kazi ipo kwa lengo la Ibada, kila mtu anapofanya kazi, anarejea kazi ya
siku sita za Mungu za uumbaji. Kazi inaleta Faraja na furaha, mwili huzalisha
Dopamine kila kazi inapokamilika. Kazi ipo kujenga afya, mwili huvunja kila
mafuta hatarishi, maji na damu huimarisha mzunguko wake kwa kila kazi
inapofanyika, kazi hujenga familia na ushirikiano kwa asili yake ya
ushirikiano. Kazi ni msingi wa ukuaji, mwanadamu hufunguka kimawazo na kiuchumi
kila anapofanya kazi. Lakini Lusifa ameifanya kazi kuonekana ni mateso, ambayo
watu wenye mafanikio huifanya kuwa ndogo hata kutoifanya kabisa. Lusifa
ametengeneza kazi kuonekana ni uwanja wa Vita na mashindano. Watu wanafanya
kazi ili kuonekana, au kuwa juu zaidi ya wenzao. Kazi imeonekana ipo kwa ajili
ya kuishi, na sio kuishi kwa ajili ya kazi. Mwanadamu hakuumbwa na kazi, ila
mwanadamu ndiye aliyeumba kazi zake baada ya kuishi. Leo hii kuna kazi nyingi
ambazo zamani hazikuwepo, hii ni kwa kuwa kama mwanadamu aishivyo, ndivyo
hutengeneza kazi mpya kila siku.
Kama Joka
Lusifa kama joka huwamaliza wote aliowafanya kuichukia kazi. Lusifa huwafanya wanaume kuwa kama wanawake, na wanawake kama wanaume kupitia kazi. Mwanaume tangia akiwa mdogo sio kiumbe wa kukaa chini, na ndiyo maana hana uwezo wa kuvumilia kukaa kwa muda mrefu. Kitaalamu mwanaume ana ‘’BMR’’ kubwa, akiwa na misuli mikubwa, na mafuta kidogo. Lusifa amewaweka wanaume wenye sifa nzuri za kiume katika kiti kwa miezi mpaka miaka, sasa wamekuwa na mafuta mengi tumboni, amewafanya kuwa na pumzi ndogo sana za kustahimili nyakati za ukakamavu, amewafanya kukesha usiku na mianga ya taa za umeme na kuwashushia homoni za kiume kama ‘’testosterone’’, sasa wanaume sio wenye maamuzi magumu tena kama zamani.
linganisha mwanaume wa picha ya awali, na wanaume wa picha ya chini.
unaweza tabiri hali za uanaume baina ya tabia zote katika picha hizo.
Maelfu ya watu wanashida zinazotokana na mitindo yao ya kazi. Wapo ambao maisha yao yameshamiri katika mitambo inayowafanya kufanya kazi ambazo zinatumia sana aina moja tu ya misuli, hata kudhoofisha sehemu zingine za miili yao. Wapo wafanyakazi ambao hawana kazi kabisa za misuli yao kama ambavyo wangepaswa, na ugumu wa ratiba zao, wengi wa watu hawa hata muda wa mazoezi huwa hawapati. Lusifa amewafanya watu kuwa na stress nyingi makazini mwao, wengi wao makazini hutumia vyakula dhaifu kabisa kwa afya zao. Kazi nyingi sana zimezidi kuwa za kusaidia utendaji kazi wa mashirika, kuliko kazi ambazo zina maslahi ya moja kwa moja kwa watu. Lusifa anajua hii ni namna bora zaidi ya kuwafanya wafanyakazi hawa kuwa watumwa wa mashirika yake, na serikali.
Lusifa anajua kadri anavyowakusanya watu
wengi katika mitindo yake ya kazi, sehemu kubwa sana ya watu watakosa kazi. Hii
imepelekea dunia nzima kuwa na kilio cha upungufu wa kazi, lakini wakiisema
kazi kama ajira. Lusifa alishajua tangia awali, kama watu hawatajua msingi wa
kazi tangia awali, wengi hawatajua lengo la kazi lilikuwa ni kushea nguvu na
maarifa, na sio kujikusanyia. Kama kila mtu atakuwa akijikusanyia, baada ya
muda lazima watu wengi watakosa. Hebu chukulia mfano huu, kama Nchi nzima
inamzunguko wa kiasi ‘’XXX/=Tsh’’ kwa watu wote, na katika mzunguko huu, watu
kadhaa wakawa na nguvu ya kujikusanyia zaidi ya wengine, nini kitatokea baada
ya muda? Bila shaka haiihitaji hisabati kujua baada ya muda, wengi wa watu
watabakiwa na kiwango kidogo sana cha thamani, na kadri siku zinavyoenda,
ndivyo hata duniani tunavyozidi kushuhudia familia chache tu zikizidi kuwa na
Nguvu zaidi kiuchumi, na tena, zikiwa na nguvu hata kisiasa. Hili lilikuwa
lengo la Lusifa la kuja kuua kabisa mfumo wa kazi kwa binadamu.
Malengo ya Lusifa yalikuwa ni kuhakikisha
anafanya watu wengi zaidi katika jamii kushindwa kufanya kazi. Maana hawana
pakufanyia kazi, hali za maisha na hewa zinazidi kuwa ngumu, wengi hawana nafasi katika mashirika na serikali.
Lusifa anazidi kuchochea hisia za ukaidi, ukatili, hasira, na hata unyang’anyi
kwa vijana hawa waliochini, Lusifa anajua wakati mbele kidogo atainua Chuki
kubwa ndani yao, na atatumia ghadhabu yao dhidi ya mifumo iliyojuu yao
kutengeneza migogoro mikubwa ya amani, na amani haitakwepo tena mpaka Yesu
atakaporudi.
Mafanikio ya Lusifa ni makubwa sana katika
kazi. Asilimia kubwa ya vijana waliokuwa wanahitaji kazi, sasa hawana kazi.
Idadi kubwa ya mazingira ambayo watu hawa wangeweza kutengeneza kazi, hawawezi
tena kuwepo, wala kuyamudu. Maana Lusifa ameshachochea uharibifu mkubwa kabisa
wa mazingira kama tutakavyoona mbeleni kidogo.



Join the conversation